Siku takribani saba baada ya kutokea kwa vurugu za mashabiki wa Coastal kutaka kuwashambulia
waamuzi waliochezesha mchezo wa timu hiyo dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa
Mkwakwani mkoani Tanga, makubwa yameibuka juu ya kilichotokea nyuma ya pazia.
Katika
vurugu hizo, baadhi ya mashabiki wa Coastal walilalamikia maamuzi kadhaa ya
mwamuzi wa mchezo huo, ikiwemo kuwapa penalti Mbeya City dakika za mwishoni mwa
mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliomalizika kwa sara ya bao 1-1, hivyo kusababisha
amani kutoweka lakini askari polisi waliwahi kuingilia na kuchukua hatua.
Taarifa
ambazo gazeti hili limezipata ni kuwa kwa kuwa vurugu hizo zilitokea wakati
waamuzi wakiwa uwanjani hawajaingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, kuna
mashabiki waliovamia vyumba hivyo na kuvunja kisha kuingia ndani na kuiba mali
za waamuzi hao waliochezesha mchezo huo.
Baadhi ya
mali zilizoibiwa ni simu, nguo za michezo na fedha.
Mmoja wa viongozi anayeishi karibu na Uwanja wa Mkwakwani amesema:
“Ndiyo
waamuzi waliibiwa vitu vyao, uharibifu ulikuwa mkubwa, achana na ule wa kuvunja
vifaa vya waamuzi wa akiba kama ilivyoonekana kwenye runinga,” alisema kiongozi
huyo na kuongeza:
“Unajua
kuna vitu vinaendelea vingi nyuma ya pazia, naamini hata hiyo ripoti ya mwamuzi
wa mchezo huo, sidhani kama itaeleza uhalisia wa vurugu zilizotokea na kuwa
mchezo huo ulivunjika.
“Ndiyo
mchezo ulivunjika kwa kuwa mwamuzi hakupata muda wa kumaliza mchezo kwani
tayari alikuwa amevamiwa, kuna ushawishi mkubwa kutoka kwa***(anamtaja jina, ni
kiongozi wa juu wa soka) ndiyo maana hata maamuzi yatakayochukuliwa sidhani
kama yataendana na kosa lenyewe.
“We si
unaona, lile sakata la (Juma) Nyosso lilichukuliwa kwa uzito wakati hili ambalo
lilikuwa likitishia maisha kabisa ya watu linapotezewa.
“Kila
mwanasoka anajua adhabu ya timu inayohusika kuvunja mchezo, licha ya kuwa mpira
ulikuwa ukielekea mwishoni, lakini mwamuzi hakuumaliza mchezo huo.”
Alipoulizwa
Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura kuhusiana na vurugu hizo alisema:
“Tumeipata ripoti lakini kwa kuwa ni suala la kinidhamu tumepeleka suala hilo
kwa Kamati ya Nidhamu, waulizeni TFF au kamati husika juu ya nini
kinachoendelea.”
Alipoulizwa Katibu Kuu wa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa, alisema: “Hiyo barua haijafika mezani
kwangu, kwa hiyo siwezi kulizungumzia.”
SOURCE: CHAMPIONI
No comments:
Post a Comment