Mara baada ya kuapishwa, Rais huyo wa Serikali ya Awamu ya Tano alianza kazi kwa kutembelea Wizara ya Fedha, baadaye kuagiza Mamlaka ya Mapato (TRA) kudhibiti wakwepa kodi kabla ya kusimamisha safari zote za nje hadi kwa kibali maalumu.
Dk Magufuli amechukua hatua hizo, ikiwa ni mkakati wa kukusanya mapato na kudhibiti matumizi kwa lengo la kuijengea Serikali uwezo wa kuwatumikia wananchi, ikiwa ni pamoja na kutekeleza ahadi ya kutoa elimu bure hadi kidato cha nne ambayo inahitaji uwezo mkubwa wa kifedha.
Lakini wasomi na wanasiasa wanaona kiongozi huyo wa nchi anatakiwa kuchukua hatua zaidi kwa kuangalia maeneo mengine ambayo yatasaidia kuiwezesha Serikali kupata fedha nyingi iwapo atayazingatia.
Akiandika kwenye ukurasa wake wa facebook, kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe (pichani) alitaja mambo kumi muhimu ambayo yataisaidia Serikali ya Magufuli kuweka misingi ya mabadiliko ya kweli katika kipindi cha uongozi wa serikali.
Zitto alimtaka Rais Magufuli kuweka wazi mikataba yote ya rasilimali za nchi, kufuta posho za vikao katika mfumo mzima wa Serikali kama Mpango wa Maendeleo unavyotaka na kufuta malipo ya daraja la kwanza kwa usafiri wa anga kwa watendaji wa Serikali na wanasiasa isipokuwa Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu.
Mwenyekiti huyo wa zamani wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) pia alitaka kufuta matumizi ya magari ya kifahari, kufuta uagizaji wa sukari kutoka nje na kuanzisha miradi ya miwa, kuweka wazi taarifa ya Serikali kuhusu utoroshaji wa fedha na kufungua mashtaka kwa wahusika, kuipa Takukuru mamlaka ya kukamata na kushtaki, na kila mwenye mali athibitishe kaipataje.
”Jambo la nane ni kuweka wazi mali na madeni ya viongozi kwa umma kisha wananchi waruhusiwe kuhoji, kuruhusu mshindi wa uchaguzi Zanzibar atangazwe na akubali kufanya naye kazi na kuendelea na mchakato wa Katiba kwa kuanzia alipoishia Warioba, achana na Katiba Pendekezwa,” alisema mbunge huyo wa Kigoma Mjini.
Kama vile haitoshi, Profesa Humphrey Mushi wa Idara ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alitaja mambo mengine kuwa ni kuepuka kununua maziwa kutoka nje na badala yake nguvu iwekezwe kwenye viwanda vya maziwa vya ndani, hasa vilivyopo Tanga na Arusha. Alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza mapato ya ndani na soko la ajira nchini.
“Lakini pili, serikali inatakiwa kuachana na manunuzi ya samani za ndani kutoka China na Malyasia. Kwanza hazina ubora na gharama zake ni kubwa kwa hivyo lazima kuwekeza katika manunuzi ya samani za ndani. Hii itasaidia kupunguza matumizi ya serikali,” alisema Profesa Mushi.
Jambo jingine ambalo msomi huyo alitaja ni udhaifu katika Sheria ya Manunuzi ya Umma, ambayo alisema inatoa mwanya kwa watumishi wa Serikali kula rushwa. Alisema udhaifu huo hufanyika wakati wa Serikali inapotakiwa kulipia kiwango cha riba ya bidhaa katika manunuzi yake.
“Lakini hata kitengo cha manunuzi kimekosa watalaamu wazuri. Wananunua vifaa visivyokuwa na ubora kwa hivyo ni hasara kwa Serikali. Ni muhimu kuangalia hilo,” alisema Profesa Mushi.
Alitaja jambo la nne kuwa ni matumizi ya mitambo ya umeme kupitia kampuni binafsi kwani serikali inaweza kununua mitambo yake na kuepuka gharama. “Kwa mfano, Serikali inalipa mabilioni ya fedha katika uzalishaji umeme unaofanywa na kampuni za hapa nchini, lakini fedha hizo ingeweza kununulia mitambo yake kama ingetunza kwa miaka miwili,” alisema.
Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Lihundi alitaja mambo mengine kuwa ni matumizi ya muda katika rasiliamali watu. Alisema kila mtumishi anatakiwa kufanyiwa tathmini ya matumizi ya muda wake wa kuzalisha katika nafasi aliyopo serikalini.
“Muda ni muhimu sana. Je, anahudhuria kazini na kutoa huduma ipasavyo. Je, muda wake anaoutumia kazini unaendana na kasi ya uwajibikaji. Anazalisha kwa kiwango gani? Na matokeo ya uwajibikaji yatazamwe,” alisema Lihundi.
Lihundi alisema udhaifu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma pia uangaliwe, pamoja na matumizi ya magari ya kifahari kwa watendaji wa serikali na kuhakiki hata safari za ndani ya nchi. “Kufuta safari za nje ni sawa, lakini ajaribu kutazama safari za ndani. Kuna ubadhirifu unafanyika sana,” alisema.
“Kwa mfano watumishi wizara yote wanakwenda bungeni, lakini kila mmoja anakwenda na gari lake. Kwa nini wasitumie gari moja?” alihoji Lihundi.
No comments:
Post a Comment