Kama mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema anapambana na Mrisho Gambo
ili kujijenga kwa wananchi wake, basi mkuu huyo wa mkoa ananufaika na
vita hiyo na anatarajia makubwa zaidi baada ya mzozo wa mwanzoni mwa
wiki.
Wakati Gambo akitarajia kupandishwa cheo na Rais John
Magufuli, madiwani wa jiji hilo wametangaza kususia vikao vyote hadi
viongozi wa juu wa Serikali watakapoingilia kati mgogoro uliopo.
Wawili
hao waliingia kwenye mzozo mwingine mapema wiki hii wakati Gambo
alipoalikwa kuzindua ujenzi wa hospitali ya mama na mtoto, itakayojengwa
kwa ufad kwa ufadhili wa taasisi ya Martenity Africa alipojaribu
kueleza historia ya kiwanja cha jengo hilo, maelezo ambayo Lema
aliyapinga kwa sauti kubwa na kusababisha shughuli hiyo kuvurugika.
Baada ya mzozo huo, Gambo amedokeza kuwa kuna makubwa yanafuata.
“Baada
ya hilo, simu zilikuja kibao, lakini bahati nzuri kabla sijauliza
kokote, na Mheshimiwa Rais ndio akawa ananipigia akaniambia nina full
confidence (nina imani) na wewe. Labda wafikirie promotion (kupandisha
cheo), lakini hayo mengine hayapo,” alisema Gambo akiwaeleza
wafanyabiashara wa mjini hapa kuhusu barua iliyosambaa juzi kwenye
mitandao ya kijamii kuwa Rais ametengua uteuzi wake.
“Baadaye
(Rais) akaniambia kwamba sasa ili (wafanyabiashara) wajue kwamba kweli
nimekupigia simu, niitie mmoja uliye naye karibu ili niongee naye. Ndio
(mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Arusha) akapata previledge (bahati)
naye ya kuongea na Mheshimiwa Rais.”
Iwapo Gambo atapandishwa
cheo, ambacho kwa mukhtadha wa utumishi wa umma chaweza kuwa ni
kuteuliwa kuwa mbunge na baadaye waziri, itakuwa ni mara ya pili kupanda
cheo siku chache baada ya kuzozana na Lema.
Gambo, ambaye
aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha Juni 26, alilumbana na Lema
Agosti Mosi mbele na Naibu Waziri wa Tamisemi, Suleiman Jafo.
Katika
tukio hilo, Lema alisema Gambo haheshimu mipaka ya kazi zake,
akimtuhumu kuingilia maamuzi ambayo tayari yameshajadiliwa kwenye vikao
halali vya halmashauri na kupitishwa na ofisi ya mkuu wa mkoa katika
kikao cha wakuu wa idara, maofisa tarafa, waratibu wa elimu kata
watumishi wa Mamlaka ya Maji Safi na Mazingira (Auwsa) jijini hapa.
“Nimeona
nizungumze hapahapa ili naibu waziri ufahamu hali ilivyo hapa. Kwa
mfano Baraza la Madiwani la mwaka 2008, ndilo lililopitisha kiwango cha
posho kwa madiwani kutoka Sh100,000 hadi 120,000. Jambo la kushangaza DC
ameandika barua Tamisemi na nakala kwa Takukuru ili wachunguze jambo
ambalo limeshapata baraka za Tamisemi,” alisema Lema.
Hali hiyo
ilimfanya naibu waziri kuingilia kati na kuahidi kuzishughulikia
changamoto hizo na kumpa nafasi Gambo, ambaye wakati huo alikuwa mkuu wa
wilaya, kujibu hoja hizo.
“Mheshimiwa mbunge nataka ujue mimi ndiyo
mkuu wa shughuli za Serikali hapa wilayani. Muda wowote nina uwezo wa
kuingilia kati mambo ambayo naona hayaendi sawa, hata kama yupo katibu
tawala na viongozi wengine,” alisema Gambo.
“Rais aliona ninafaa ndiyo maana akaniteua na sihitaji kujifunza namna ya kuwa mkuu wa wilaya kwa kuwa huu ni mwaka tano.”
Malumbano
hayo yaliendelea na kumuhusisha pia Meya wa Jiji la Arusha, Calist
Lazaro ambaye aliungana na Lema na madiwani wengine kupinga jambo hilo.
Baada
ya vuta nikuvute hiyo mbele ya waziri, Agosti 18 Gambo aliteuliwa kuwa
Mkuu wa Mkoa wa Arusha kuchukua nafasi ya Felix Ntibenda.
Siku
chache baada ya uteuzi huo, Gambo aliagiza halmashauri ya jiji kutafuta
fedha za kupunguza deni la walimu ambalo ni Sh154 milioni.
Mkurugenzi wa
jiji hilo, Athuman Kilamia alitangaza posho za madiwani ambazo zilikuwa
zinalipwa kinyume cha taratibu, zitumike kupunguza deni la walimu na
zikatolewa.
Mgogoro ukaibuka kati ya madiwani wa jiji hilo ambao wengi ni kutoka Chadema.
Sakata
la Jumanne wiki hii linaweza kumpa cheo kikubwa zaidi kutokana na Rais
Magufuli kumpigia simu kwa lengo la kumthibitishia kuwa yuko pamoja naye
siku ambayo barua ya kughushi ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa
mkuu huyo wa nchi ametengua uteuzi wa Gambo.
Sakata hilo
lilitokea katika uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali ya
mama na mtoto jijini Arusha ambao utagharimu Sh9 bilioni, sehemu kubwa
ya fedha hizo zikitoka taasisi ya Martenity Africa.
Mvutano huo
ulianza baada ya Gambo kusema kuwa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa
hospitali imetolewa na Taasisi ya Mawalla Fund kwa kuwa muasisi wake,
Nyaga Mawalla alikuwa na maono ya kusaidia afya ya mama na mtoto.
Kauli
yake ilikuwa ikimaanisha kuwa Mfuko wa Maendeleo wa Arusha (ArDF)
haikutoa kiwanja hicho kwa Martenity Africa wala kutafuta mfadhili.
Jambo
hilo liliwakera viongozi wa ArDF, ambayo imeanzishwa na Lema na
Elifuraha Mlowe, ambaye ni mwenyekiti.
Lema alimtaka ndugu wa wakili
huyo amsahihishe Gambo, lakini hakuna kilichofanyika, ndipo aliposimama
na kuanza kupinga kwa sauti maelezo ya Gambo.
Lema alikuwa
akisema mkuu huyo wa mkoa anapotosha ukweli kwa misingi ya kisiasa, kwa
kuwa Mawalla Fund ilitoa kiwanja hicho kwa ArDF, ambayo ilitafuta
wafadhili na kusaini nao mkataba wa ujenzi wa hospitali.
Wageni
kwenye hafla hiyo iliyofanyika Bulka walijaribu kuwatuliza wawili hao,
hawakufanikiwa kutokana na Lema kuendelea kueleza kwa sauti kuwa Gambo
anapotosha, huku mkuu huyo wa mkoa akizungumza kwenye kipaza sauti
kumtaka mbunge huyo atulie.
Shughuli hiyo ilimalizika kiutata na hivyo waandaaji wakashindwa kuendesha harambee iliyopangwa kufanyika baada ya uzinduzi.
No comments:
Post a Comment