- OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, November 12, 2016

 

Benki ya Standard Chartered Limited ya Hong Kong (SCB-HK) imefungua maombi Mahakama Kuu ikitaka, pamoja na mambo mengine, Shirika la Umeme (Tanesco) lizuiwe kuilipa kampuni ya uzalishaji nishati hiyo ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Badala yake, SCB-HK inaomba malipo hayo yahifadhiwe mahakamani hapo hadi Tanesco itakapolipa dola 148 milioni za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh320 bilioni) kwa benki hiyo kama Mahakama ya Kimataifa ya Utatuzi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) ilivyoagiza mwezi Septemba, tofauti na ilivyokuwa wakati wa mgogoro wa Tanesco na IPTL wakati fedha zilipowekwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Katika uamuzi wake uliotolewa Septemba 12, 2016, ICSID iliamuru Tanesco iilipe SCB-HK dola 148.5 milioni, pamoja na riba ya asilimia 4, kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Septemba 30, 2015, hadi malipo yote yatakapokamilika.

Uamuzi wa ICISD ulikuja takriban miaka mitatu baada ya Serikali kuidhinisha malipo ya takriban Sh306 bilioni kutoka akaunti ya escrow iliyofunguliwa na Tanesco kwa kushirikiana na IPTL kusubiria uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu mgogoro wa malipo ya tozo ya uwekezaji.

Mwaka 2005 SCB-HK, ilinunua deni ambalo benki ya Danaharta ya Malaysia ilikuwa ikiidai IPTL baada ya kampuni hiyo kukopa dola 101.7 milioni za Kimarekani ili kununua mtambo wa ufuaji umeme wa Tegeta wenye uwezo wa kuzalisha megawati 100. Lakini wakati fedha hizo zilipotolewa, ililipwa kampuni ya Pan African Power Solutions (PAP), jambo lililofanya SCB-HK kufungua kesi hiyo ICSID ikidai ndiyo iliyostahili malipo hayo, kesi ambayo benki hiyo ilishinda.

Umuzi huo wa ICSID umeshakubaliwa na kusajiliwa na Mahakama Kuu Tanzania kupitia maombi namba 687, ya mwaka 2016, yaliyofunguliwa na SCB-HK, na hivyo unatambulika kama uamuzi wa mahakama hiyo.


IPTL inafua umeme ambao unauzwa kwa Tanesco.

Lakini SCB-HK imewasilisha maombi kwa hati ya dharura ikiomba mahakama iizue Tenesco kuendelea kuilipa PAP, ambayo inamiliki IPTL na badala yake pesa hizo ziwe zinahifadhiwa mahakamani hapo hadi deni hilo litakapolipwa lote.

Benki hiyo inaiomba mahakama isikilize upande mmoja bila Tanesco kuwepo na iamuru fedha za malipo hayo ya uwekezaji yanayofanywa na Tanesco kwa PAP, ziwe zinalipwa mahakamani hapo kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa maombi hayo.

Kwa mujibu wa hati ya dharura iliyoambatanishwa na maombi hayo, wakili wa SCB-HK, Gaspar Nyika anataka maombi hayo yasikilizwe kwa dharura akidai kuwa benki hiyo ndiyo ina haki na malipo hayo kulingana na uamuzi wa ICSID.

Pia anasema kama malipo hayo hayatahifadhiwa mahakamani kusubiri uamuzi wa maombi hayo, SCB-HK itaathirika kwa kupata hasara ambayo haiwezi kufidiwa.

Wakili Nyika anadai kuwa benki hiyo ilipewa haki dhidi ya mali na shughuli zote IPTL, baada ya kampuni hiyo kushindwa kurejesha mkopo iliouchukua kutoka benki ya Danaharta ulionunuliwa na SCB-HK mwaka 2005.

Katika uamuzi wake, ICSID ilieleza kuwa kwa mujibu wa Mkataba wa Mauziano ya Umeme (PPA) baina ya  benki hiyo na Tanesco, SCB-HK ndiyo yenye uhalali wa kisheria wa shughuli zote za IPTL.

Hivyo anasema fedha zilizolipwa kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow hazikuliondolea Tanesco wajibu wake kwa SCB-HK kwa mujibu wa PPA na hivyo hayawezi kupunguzwa kutoka katika kiasi inachodaiwa na benki hiyo. Pia ICSID ilisema kuwa malipo yaliyolipwa kwa IPTL/PAP tangu Agosti 2013, hayondoi  wajibu wa Tanesco kwa SCB-HK chini ya PPA na hivyo hayawezi kupunguzwa katika deni la SCB-HK, chini ya PPA.

Pia ICSID ilisema kuwa kuchotwa kwa pesa zilizokuwa kwenye Akaunti Maalumu ya Tegeta Escrow ( na kampuni ya Pan Africa Power Solution PAP inayodai kununua hisa zote za IPTL) hakukuiondolea benki hiyo haki katika kampuni hiyo ya IPTL.

Uamuzi wa ICSID uliwasilishwa Mahakama Kuu Oktoba 11, 2016 ili usajiliwe kwa ajili ya utekelezaji.

Hata hivyo siku hiyohiyo, Tanesco ilifungua maombi namba 686, ya mwaka 2016, ikiomba kusimamishwa kwa usajili na utekelezaji wa uamuzi huo, kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa  maombi yake ya kusimamishwa kwa utekelezaji wa uamuzi huo katika ICSID.

By James  Magai,



No comments:

Post a Comment