
Na Mwandishi Wetu , Lindi
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Lindi, imewatoa hofu watumiaji wa barabara kuu ya kutokea Lindi kwenda Dar es Salaam eneo la Somanga - Mtama kuwa linapitika vizuri na halijakatika kutokana na mvua zinazoendelea mkoani hapo.
Meneja wa TANROADS Lindi, Mhandisi Emil Zengo ametoa kauli hiyo leo tarehe 09 Mei, 2025, katika eneo hilo ambalo linaendelea na ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 60.
Mha. Zengo amesema eneo hilo la barabara ni njia ya mchepuko ambayo inatumika sasa na magari kupita wakati ujenzi ukiendelea wa daraja kwenye barabara ya kawaida.
“Pamoja na mvua kubwa kuendelea kunyesha mkandarasi yupo site anaendelea na ujenzi na haya maji yanayoonekana kwenye video iliyosambazwa na watu sio kwamba yamekatiza barabara kwa kuzidiwa kwa daraja la hasha hii imetengenezwa mahususi kitaalam kwa kuwekwa mawe makubwa pamoja na zege na pia eneo hili limesanifiwa kwa kuruhusu maji yapite juu ya barabara yanapokuwa mengi na muda huo tunashirikiana na askari wa usalama barabarani tunazuia magari kwa muda na maji yakishapungua magari yanaendelea na safari,” amesema Mha. Zengo.

Mha. Zengo amesema ujenzi wa daraja hili utahusisha nguzo 43 na hadi sasa wameshakamilisha ujenzi wa nguzo za chini 34 zilizopo mita 12 kwenda chini, na baadaye zitajengwa nguzo kubwa tatu ambazo ndizo zitakazoonekana juu.
Hatahivyo, ameshauri wananchi kufuatilia taarifa sahihi katika mitandao ya kijamii ya TANROADS na sio kuzusha hofu kwa watumiaji wa barabara hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Lindi, SP James Makumu amesema wanahakikisha usalama wa watu na mali zao kwa kufanya doria ya mara kwa mara eneo hilo, kutokana na mvua kubwa kuendelea kunyesha.
“Sisi tumejipanga kila wakati kunakuwa na askari anayeruhusu magari hapa kila maji yanapokuwa mengi tunayazuia na baada ya kupungua tunayaruhusu ili kuondoa changamoto za foleni, na tunahakikisha hakuna kabisa msongamano,” amesema SP. Makumu.
Hivi karibuni TANROADS Mkoa wa Lindi ilitangaza kusitisha matumizi ya barabara ya Somanga Mtama kwa muda baada ya mvua kubwa zilizonyesha katika Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, kuleta mafuriko makubwa yaliyoharibu eneo la barabara iliyo kwenye njia ya mchepuko (diversion) ya ujenzi wa daraja la Somanga Mtama.
No comments:
Post a Comment