
Na.mwandishi Wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuongoza waombolezaji katika mazishi ya aliyewahi kuwa Makamu wa Rais wa Kwanza na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Cleopa David Msuya, kijijini kwao Usangi Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ratiba ya maombolezo leo Mei 9, 2025, Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pia Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, amefafanua kama ifuatavyo;
Leo Ijumaa tarehe 09 Mei, 2025, maombolezo yanaendelea nyumbani kwa Hayati Cleopa Msuya, Upanga jijini Dar es Salaam ambapo kesho Jumamosi tarehe 10 Mei, 2025 mwili wa marehemu utapelekwa
nyumbani kwake kwa taratibu za kifamilia.

Siku ya Jumapili tarehe 11 Mei, 2025, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwaongoza Watanzania katika Ibada ya kuombea mwili wa marehemu itakayofanyika
katika viwanja vya Karimjee, Ilala jijini Dar es Salaam kuanzia saa 3:00 asubuhi.
Aidha, amesema ibada hiyo itakayoambatana na salamu pamoja na kuaga mwili wa Hayati Msuya katika viwanja hivyo vitafanyika kuanzia majira ya saa 03 asubuhi hadi saa 07 mchana.
" Siku ya Jumatatu tarehe 12 Mei, 2025, mwili wa Hayati Msuya utasafirishwa kwa ndege kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanga mkoani Kilimanjaro kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), tunatarajia mwili utawasili na kupokelewa KIA kati ya saa 2:30 na saa 3:30 asubuhi" ameongeza Bw. Msigwa.
Baada ya kuondoka KIA, mwili wa marehemu utasafirishwa kwa magari na kupelekwa katika uwanja wa Cleopa David Msuya uliopo Mwanga ambako viongozi mbalimbali na wananchi watapata fursa ya kuuaga.
" Tunatarajia ratiba ya kuaga katika uwanja huu, itaanza majira ya saa 5:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni siku ya Jumatatu, Mei 12, 2025" ameongeza.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Msigwa ametoa wito kwa wananchi wa Mwanga na maeneo mengine wanaotaka kumuaga mpendwa wao Hayati Msuya kutumia nafasi hiyo iliyotengwa kwa ajili yao kumuaga, aidha baada ya saa kumi jioni mwili
utapelekwa kijijini kwao Usangi ambako kutakuwa na Ibada fupi ya maombolezo.
Siku ya Jumanne tarehe 13 Mei, 2025 ndiyo itakuwa siku ya mazishi ambapo ratiba itaanza kwa Ibada maalum itakayofanyika katika Kanisa la KKKT lililopo Usangi itakayofuatiwa na mazishi ya Kiserikali nyumbani kwake yatakayoongozwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ), baada ya mazishi kutakuwa na salamu za viongozi wachache akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
No comments:
Post a Comment