
Serikali imetangaza kuanza rasmi kwa utekelezaji wa muundo mpya wa kada ya Uuguzi na Ukunga kuanzia Juni mwaka huu, ikiwa ni baada ya zaidi ya miaka 12 ya malalamiko kutoka kwa wauguzi na wakunga nchini kuhusu changamoto za muundo wa sasa wa mwaka 2009.
Akizungumza leo Ijumaa Mei 9, 2025 mkoani Iringa, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu amesema utekelezaji wa muundo huo mpya unalenga kuongeza morali ya wataalamu wa kada hiyo na kuboresha maslahi yao ya kikazi.
Sangu alikuwa akimwakilisha Waziri wa Nchi, George Simbachawene katika Kongamano la Kisayansi na Mkutano Mkuu wa 54 wa Chama Cha Wauguzi Tanzania (Tanna) linalofanyika kwa siku tatu kuanzia leo, likihudhuriwa na wauguzi 1,500 kutoka maeneo mbalimbali nchini.
“Serikali imesikia kilio cha muda mrefu cha wauguzi na wakunga, hasa kuhusu kutotambuliwa kwa waliobobea kitaaluma, wakiwemo wenye shahada ya juu na wale wa shahada ya uzamili,” amesema Sangu.
Ameeleza kuwa kupitia ushirikiano kati ya Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais – Utumishi, Baraza la Uuguzi na Ukunga, pamoja na vyama vya kitaaluma, muundo huo mpya umepitiwa na kurekebishwa ili kuondoa changamoto zilizokuwa zikilalamikiwa.
"Mchakato umekamilika na sasa Serikali ipo tayari kuanza utekelezaji wake rasmi mwezi Juni mwaka huu,” ameongeza.
No comments:
Post a Comment