
Na Mwandishi Wetu - Bahi, Dodoma
Jumuiya ya Wanawake wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) leo alasiri, tarehe 9 Machi, 2026 wamesambaza bure majiko banifu 300 kwa kaya zenye kipato cha chini katika Halmashauri ya wilaya ya Bahi mkoani Dodoma ambapo zoezi hilo liliongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Mhe. Joachim Nyingo.
Akizungumza wakati wa zoezi la ugawaji wa majiko hayo banifu 300 yenye thamani ya shilingi milioni 16 ambayo yametolewa wa Wanawake hao kutoka REA; Mhe. Nyingo ametoa wito kwa kaya hizo kuyatunza na kuyatumia kama kichocheo cha kuendelea kutumia bidhaa za nishati safi ya kupikia kama msisitizo wa matumizi ya nishati safi na salama kwa ajili ya kutunza na kuhifadhi mazingira.
“Ongezeko la Watu, vijijini linasababisha ukataji mkubwa miti kwa ajili ya kutengeneza mkaa na kuni ila kwa matumizi ya majiko haya banifu; ninaamini yanasaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, lakini pia yataokoa muda wa kuandaa chakula na hapo hapo kutunza mazingira” Amekaririwa Mkuu wa wilaya huyo.
“Niwaombe wanufaika wote, mkayatunze majiko hayo na mkawe mabalozi wa teknolojia za nishati safi. Naomba pia kutoa wito kwa wasambazaji wa teknolojia za nishati safi, endeleeni kusogeza bidhaa za nishati safi ya kupikia hadi huku vijijini.”
“Nawashukuru Wanawake wa REA kwa kuichagua wilaya ya Bahi na kugawa majiko hayo kwa kaya maskini ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa”. Amesema, Mhe. Joachim Nyingo.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu kutoka REA; Dkt. Joseph Sambali ambaye ni Mtaalam wa Nishati na Jinsia amesema, tukio la ugawaji wa majiko banifu bure kwa kaya hizo katika Kata tatu za Bahi; Mpamantwa na Ibihwa ni juhudi za utekelezaji wa Mkakati wa Kifaifa wa Nishati Safi ya Kupikia na unalenga hadi ifikapo mwaka 2034 zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi.








No comments:
Post a Comment