Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, amesema ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchini Urusi imekuwa na mafanikio makubwa na kuibua maslahi mapya ya ushirikiano ya kimkakati kati ya Tanzania na Urusi katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Juni 7, 2026, Balozi Kombo alisema mwitikio mkubwa uliopatikana wakati wa ziara hiyo unaonesha namna Tanzania inavyoendelea kuimarisha nafasi yake katika diplomasia ya kimataifa na ushirikiano wa kiuchumi na mataifa mbalimbali duniani.
Ziara hii imefanyika katika kipindi muhimu ambapo Urusi inaendelea kutekeleza mkakati wake wa kujimarisha na kupanua ushirikiano na nchi za Bara la Afrika, hali hii inaweka mazingira mazuri kwa Tanzania kunufaika na fursa mbalimbali za uwekezaji, biashara na uhamishaji wa teknolojia, alisisitiza Balozi Kombo.
Balozi Kombo, amesema viongozi na taasisi mbalimbali za Urusi kwa pamoja wameonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika sekta za kimkakati zikiwemo nishati, madini, kilimo, elimu, afya, uchumi wa kidijitali na maendeleo ya viwanda, hatua inayotarajiwa kuongeza thamani katika uchumi wa nchi hizo mbili.
"Serikali itaendelea kufuatilia utekelezaji wa makubaliano na maelewano yaliyofikiwa wakati wa ziara hii ili kuhakikisha fursa zilizopatikana zinatafsiriwa kuwa miradi na uwekezaji wenye manufaa kwa wananchi, ili zikichangie kukuza uchumi na kuimarisha uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Urusi, alisisitiza Balozi Dkt. Kombo.
Alieleza kuwa mkutano na waandishi wa habari umelenga kuchambua na kuweka wazi mafanikio yaliyopatikana pamoja na fursa mpya zilizojitokeza kufuatia ziara ya Rais Samia, ili wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo waweze kufahamu matokeo ya ushirikiano huo wa kimataifa.







No comments:
Post a Comment