
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amezindua Kituo Mama cha
Gesi Asilia iliyoshindiliwa (CNG) ambacho kina uwezo wa kujaza Gesi
Asilia kwenye magari 1200 kwa siku huku kikifanya kazi kwa muda wa saa
24.
Kapinga amezindua kituo hicho tarehe 9 Mei, 2025 jijini Dar es Salaam
akimwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko ambapo uzinduzi huo ulienda sambamba na uzinduzi wa basi la
mfano la Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) ambalo litaendeshwa
kwa kutumia nishati ya Gesi Asilia.
Akizungumza na halaiki iliyohudhuria hafla hiyo, Kapinga amemshukuru
Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono, mtazamo na maelekezo yake
kwa Wizara ya Nishati ambayo yanaleta matokeo chanya kielelezo
mojawapo kikiwa ni uzinduzi kwa kituo hicho cha CNG.
Pia, amemshukuru Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.
Doto Biteko kwa uongozi wake ambao unapelekea upatikanaji wa nishati
ya uhakika ambayo ni rafiki kwa mazingira na afya za wananchi.
“ Hapo nyuma kumekuwa na malalamiko ya uwepo wa foleni kubwa za
ujazaji wa gesi kwenye vyombo vya moto katika vituo vya CNG ikiwemo
kituo cha Ubungo Maziwa, lakini uwepo wa kituo hiki unaonyesha jinsi
Serikali inavyotekeleza kwa vitendo ahadi inazotoa kwa wananchi za
kupunguza kero ya upatikanaji wa CNG, nampongeza Rais Samia kwa
kuendelea kutatua changamoto za wananchi na pia naipongeza Bodi na
Menejimenti ya TPDC kwa hatua hii.” Amesema Kapinga
Ameeleza kuwa, kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kujaza Gesi kwenye
magari nane kwa wakati mmoja, kuchochea ongezeko la vituo vingine vya
CNG na kuwapatia huduma ya gesi watumiaji wengine kama viwanda, shule,
hoteli n.k

Kapinga ameiagiza TPDC kuhakikisha kuwa, kituo hicho kinakuwa mfano wa
kutoa huduma bora na za viwango kwa wateja huku kikizingatia masuala
ya usalama na utunzaji wa mazingira.
Pia ameiagiza TPDC kuendelea kujenga vituo vya CNG katika maeneo
mengine ya nchi ikiwemo Lindi na Mtwara, pia kutoa ushirikiano kwa
sekta binafsi ili kuendelea kuchochea uwekezaji kwenye sekta ya CNG.
Naibu Waziri Kapinga pia ameishukuru Sekta binafsi kwa kuendelea
kuiunga mkono Serikali kwenye ujenzi wa vituo vya CNG.
Aidha, amewaasa Watanzania kuchangamkia fursa ya kuweka mifumo ya
matumizi ya gesi kwenye magari yao kwani mifumo hiyo haiharibu magari
hayo na pia watapata nafuu ya gharama za uendeshaji.
Kuhusu kampuni ya UDART ambayo kwa mara ya kwanza imezindua basi jipya
linalotumia Gesi Asilia, ikiwa ni moja ya mabasi mengi yakayotumia
gesi hiyo, Kapinga amesema kuwa ushirikiano kati ya TPDC na UDART
utaendelea kuchochea uwekezaji kwenye CNG na kuendelea kuboresha
huduma za usafiri jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando akizungumza kwa niaba ya Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, ameipongeza wizara ya Nishati kwa kazi kubwa
inayofanyika ili kupata matokeo makubwa kwenye sekta na kuahidi ulinzi
katika miundombinu hiyo ambayo ni muhimu katika kutoa huduma kwa
wananchi.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini,
Mhe.Kilumbe Ng’enda amesema Bunge limeridhishwa na hatua
zinazochukuliwa kwa kasi na Serikali katika kuendeleza Sekta ya Gesi
akieleza kuwa unapotumia gesi asilia kuendesha gari unapata unafuu kwa
asilimia 40 ukilinganisha na mafuta.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio ameipongeza
Bodi na Menejimenti ya TPDC kwa kutekeleza mradi huo kwa mafanikio,
pia ameipongeza UDART ambao watakuwa wateja wakubwa wa CNG.
Amesema mradi huo ni wa kujivunia kwani kituo hicho kilichozinduliwa
ni cha Pili kwa ukubwa barani Afrika na cha kwanza kwa ukubwa katika
ukanda wa Afrika Mashariki
Mwenyekiti Bodi TPDC, Mhe. Balozi Ombeni Sefue amesema Bodi na
Menejimenti ya Taasisi hiyo itahakikisha changamoto ya wananchi
kupanga foleni ndefu kwenye vituo vya CNG inaisha na watahakikisha
rasilimali ya gesi asilia inapatikana wakati wote kupitia huduma
mbalimbali ikiwemo ya kupikia na kuendeshea vyombo vya moto.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Francis Mwakapalila amesema kuwa
katika kuchochea matumizi ya Gesi Asilia kwenye vyombo vya moto
nchini, TPDC imeamua kuweka mkazo kwa kuwekeza katika ujenzi wa vituo
vya kujazia gesi asilia kwenye vyombo vya moto ikiwemo magari na
bajaji kwenye maeneo mbalimbali nchini na kwa sasa tayari wameanza
mchakato wa manunuzi ya vituo vitano vya CNG vinavyohamishika ambavyo
vitawejwa kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma.
Awali Mkurugenzi wa Idara ya Biashara ya Mafuta kutoka TPDC, Mhandisi
Emmanuel Gilbert alisema kuwa kituo hicho kina uwezo wa kuzalisha CNG
kiasi cha futi za ujazo milioni 4.2 sawa na kilo 120 kwa siku, kina
pampu nne zenye jumla ya nozeli nane na hivyo kukifanya kituo kuwa na
uwezo wa kuhudumia magari nane kwa wakati mmoja ambapo kwa siku
kitatoa huduma kwa magari takriban 1200.
Ameongeza kuwa, kituo kina pampu maalum tatu kwa ajili ya kujaza magari maalum ya kusafirisha CNG kwenda kwenye vituo vidogo vya kujaza gesi kwenye magari (Offline CNG Filling Stations), viwandani, taasisi na majumbani.
No comments:
Post a Comment