PROF. MKUMBO: SEKTA BINAFSI NI MUHIMU KUFANIKISHA MPANGO WA NNE WA MAENDELEO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, March 9, 2026

PROF. MKUMBO: SEKTA BINAFSI NI MUHIMU KUFANIKISHA MPANGO WA NNE WA MAENDELEO

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Serikali inatarajia zaidi ya asilimia 70 ya fedha za utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano zitatoka katika sekta binafsi kupitia uwekezaji na mifumo ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP).

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa kongamano la kujadili nafasi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi lililoandaliwa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), Waziri wa Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema serikali inalenga kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Amesema Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano unaotarajiwa kuanza kutekelezwa mwaka wa fedha 2026/2027 umeweka malengo mbalimbali ikiwamo kuimarisha uthabiti wa uchumi, kuboresha miundombinu ya usafiri na kuongeza tija katika sekta za uzalishaji.

Profesa Mkumbo amesema Tanzania pia imejiwekea malengo makubwa ya kukuza uchumi katika kipindi cha miaka 25 ijayo kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuongeza ukubwa wa uchumi hadi kufikia zaidi ya dola trilioni moja za Marekani.

Amesema kufikia malengo hayo kunahitaji mabadiliko ya kimfumo na ushiriki mkubwa wa sekta binafsi, kwani serikali pekee haiwezi kutekeleza shughuli zote za kiuchumi.

“Jukumu la serikali ni kuweka sera, sheria na kusimamia uchumi kwa ujumla, lakini shughuli nyingi za kiuchumi zinaweza kutekelezwa kwa ufanisi zaidi na sekta binafsi,” amesema.

Ameongeza kuwa tayari Tanzania imeanza kutekeleza miradi kadhaa kupitia mfumo wa PPP katika sekta mbalimbali ikiwamo usafiri, miundombinu na huduma za biashara, huku mingine ikiwa katika hatua tofauti za maandalizi.

Hata hivyo, amekiri kuwa kasi ya utekelezaji wa miradi ya PPP bado ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya miradi iliyopangwa, hali inayolazimu serikali kuendelea kuboresha mifumo ya kisheria na kiutendaji ili kuongeza ufanisi.

Amesema serikali pia inaendelea kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji pamoja na kuhamasisha taasisi za umma kutumia mfumo wa PPP pale ambapo miradi inaweza kutekelezwa kwa ufanisi zaidi na sekta binafsi.

Profesa Mkumbo amesema kongamano hilo ni jukwaa muhimu kwa wadau kubadilishana mawazo na kutoa ushauri kwa serikali kuhusu namna bora ya kutumia ubia wa sekta ya umma na binafsi ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), David Kafulila, amesema jukumu la taasisi hiyo ni kuratibu ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inayoweza kutekelezwa kwa ubia inafanyika kwa ufanisi.

Amesema kongamano hilo ni mwanzo wa majadiliano ya mara kwa mara yatakayokuwa yakifanyika kila mwezi kwa lengo la kuwakutanisha wadau mbalimbali wakiwamo wanazuoni, wataalamu wa uchumi, sekta binafsi na taasisi za serikali ili kujadili masuala ya maendeleo ya uchumi na utekelezaji wa miradi ya ubia.

Kafulila ameongeza kuwa majadiliano hayo yatatoa fursa kwa wadau kutoa mapendekezo na ushauri kwa serikali kuhusu namna bora ya kutumia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi ili kuimarisha uchumi wa taifa.

No comments:

Post a Comment