KAMATI ya Sheria Maadili na Hadhi za Wachezaji leo inatarajiwa kutolea uamuzi malalamiko ya klabu ya Simba dhidi ya mchezaji wake, Hassan Kessy na klabu ya Yanga.
Simba inalalamikia klabu ya Yanga kumsajili beki Kessy akiwa hajamaliza mkataba wake Msimbazi na kwa sababu hiyo inataka kulipwa Sh. Milioni 200 ambayo ni punguzo kutoka Bilioni 1.2 walizotaka awali.
Suala hilo lilianzia Kamati ya Maadili, ambako ilishindikana kupatiwa ufumbuzi na Kamati hiyo ikaagiza Simba na Yanga zikutane zenyewe kumalizana.
Hata hivyo, mahasimu hao wa jadi katika soka ya Tanzania walishindwa kufikia mwafaka na wakakubaliana kumteua, Mwenyekiti wa zamani wa TFF enzi za FAT (Chama cha Soka Tanzania), Said El Maamry kuwasimamia katika kikao kingine cha kutafuta mwafaka.
Bahati mbaya, Simba na Yanga mbele ya Mzee El Maamry pia wakashindwa kufikia mwafaka na suala hilo linarudishwa Kamati ya Madili.
Viongozi wa pande zote mbili, Simba na Yanga wote watakutana mbele ya Kamati ya Maadili iliyo chini ya Mwenyekiti wake,Wakili Richard Sinamtwa kwa kikao cha kulipatia suluhisho suala hilo.
Kamati hiyo ilisema mapema inawapa nafasi Simba na Yanga wakamalizane wenyewe na ikishindikana, suala hili litarejeshwa Kamati ya Maadili kwa uamuzi.
Kessy alijiunga na Simba SC mwaka 2014 kutoka Mtibwa Sugar, lakini mapema tu kabla ya kumaliza mwaka wake wa kwanza aliingia kwenye mzozo na klabu hiyo akidai kutokamilishiwa yaliyomo kwenye mkataba, ikiwemo kutopewa nyumba na akagoma.
Hata hivyo, suala hilo lilitatuliwa na mchezaji huyo akarejea kazini kabla ya kurudi kwenye matatizo tena mwishoni mwa mwaka wake wa mwisho wa mkataba.
Simba ilimsimamsha mechi tano Kessy kwa tuhuma za kumchezea rafu isiyo ya kimchezo mshambuliaji wa Toto Africans, Edward Christopher.
Simba ilifungwa 1-0 na Toto Jumapili ya Aprili 17, mwaka huu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Kessy akatolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 47 kwa kumchezea rafu Edward, nyota wa zamani wa timu hiyo Msimbazi.
Lakini mapema Februari 20, Kessy alianza kupunguza mapenzi ya wana Simba kwake, baada ya kutoa pasi fupi kumrudishia kipa Muivory Coast, Vincent Angban iliyonaswa na mshambuliaji Mzimbabwe wa Yanga, Donald Ngoma aliyekwenda Yanga bao la kwanza katika ushindi wa 2-0.
Tayari Yanga imekutwa na hatia ya kumsajili Kessy akiwa ndani ya mkataba wa Simba, kwani japokuwa kisheria mchezaji anaruhusiwa kuingia kwenye mazungumzo na klabu nyingine akiwa amebakiza ndani ya miezi sita kumaliza mkataba – lakini si kuhamia timu mpya kabla ya kumaliza mkataba wa klabu aliyopo.
Ni hicho kinachowapa nguvu Simba SC ya kudai kulipwa, ingawa ni kweli wanataka kiasi kikubwa cha fedha kuliko uzito wa madai yao.
No comments:
Post a Comment