
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka, amewataka wataalamu wa TEHAMA nchini kuwasaidia vijana kutumia mitandao kwa mambo yenye tija badala ya matumizi hasi yanayoweza kuhatarisha usalama na amani ya nchi.
Ametoa wito huo leo jijini Arusha wakati akifungua rasmi Mkutano wa Sita wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), akisisitiza kuwa TEHAMA ni nguzo muhimu ya maendeleo na inapaswa kutumika kuchochea ubunifu, ajira na ustawi wa taifa.
“TEHAMA ni kipaumbele muhimu kwa Serikali ya Awamu ya Sita, hivyo nasisitiza huduma zake zipatikane kwa haraka na kwa urahisi, lakini pia ubunifu wowote utangazwe ili wananchi waweze kuelewa na kuutumia,” amesema Balozi Dkt. Kusiluka.
Katika kuharakisha mageuzi ya kidijitali, amezitaka taasisi za umma na binafsi kutangaza mifumo mbalimbali wanayobuni, ikiwamo teknolojia ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence), ili wananchi waweze kuifahamu na kuitumia kurahisisha shughuli zao za kila siku.
Amesema ni muhimu ubunifu wa kiteknolojia unaofanywa na serikali au sekta binafsi kutangazwa kwa uwazi ili wananchi wauelewe na kuutumia ipasavyo kwa maendeleo yao binafsi na ya taifa kwa ujumla.
Aidha, amewataka wakuu wa taasisi zote kuzingatia kikamilifu Sheria ya Serikali Mtandao Namba 10 ya mwaka 2019 pamoja na kanuni na miongozo yake katika utekelezaji wa majukumu yao, sambamba na kuzifanyia kazi kwa haraka taarifa na mapendekezo yanayotolewa na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ili kuimarisha uwajibikaji na ufanisi.
Kuhusu usalama wa taarifa, Katibu Mkuu Kiongozi amezitaka taasisi zote kujisajili katika mamlaka husika ya ulinzi wa taarifa binafsi ili kuhakikisha taarifa zinahifadhiwa kwa usalama na kwa kuzingatia sheria.

Pia amesisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo watumishi wa umma kupitia mafunzo ya mara kwa mara ili waendane na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani, akionya kuwa kushindwa kufanya hivyo kutazorotesha jitihada za maendeleo ya kidijitali.
“Iwapo hamtawapa fursa za kuongeza ujuzi, wataendelea kufanya kazi kwa kutumia mifumo ya kizamani na mtashindwa kuendana na kasi ya kiteknolojia ya dunia,” ameonya.
Sambamba na hilo, ameonya vikali watumishi wanaochezea mifumo kwa lengo la kufanya hujuma au kujinufaisha binafsi kuwa hawatavumiliwa, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vinahujumu juhudi za serikali katika kufikia malengo ya maendeleo ya kidijitali.
Amesema Tanzania kwa sasa ipo miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika matumizi ya teknolojia, ambapo zaidi ya asilimia 80 ya huduma za serikali zinapatikana mtandaoni.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Benedict Ndomba, amesema wanaendelea kuhakikisha matumizi ya serikali mtandao yanakuwa salama na shirikishi licha ya changamoto ya uhaba wa wataalamu wa TEHAMA.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Serikali Mtandao Zanzibar, Dkt. Said Seif Said, amesema wataendelea kushirikiana na Serikali Mtandao Bara kuboresha huduma za kidijitali, huku Mwenyekiti wa Bodi ya e-GA, Mussa Kissaka, akieleza kuwa mkutano huo unalenga kukusanya maoni yatakayosaidia kuboresha zaidi utoaji wa huduma kwa njia ya kidijitali.
Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ni taasisi ya umma iliyoanzishwa kwa Sheria ya Serikali Mtandao Namba 10 ya mwaka 2019 kwa lengo la kuimarisha na kuendeleza utoaji wa huduma za serikali mtandao kwa taasisi za umma nchini.

No comments:
Post a Comment