Mtoto Happiness Josephat (6) aliyefanyiwa upasuaji wa kupandikiza betri moyoni katika Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), amefariki dunia.
Mama mzazi wa Happiness, Elitruda Malley amesema Happiness alifariki dunia ghafla juzi mchana.
Alisema
Jumapili, mtoto huyo alikuwa mzima na walikwenda kanisani kutoa sadaka
ya shukrani kama ishara ya kumshukuru Mungu kwa mambo aliyowatendea na
wakarudi nyumbani salama.
“Jana
tumeamka vizuri lakini ghafla hali yake ilibadilika akaanza kulalamika
kuwa anajisikia vibaya, tukamkimbizia Hospitali ya Selian hapa Arusha
lakini tukiwa njiani alifariki dunia,” alisema.
Elitruda alisema kifo cha mwanawe kimemhuzunisha mno na daima atamkumbuka.
“Alikuwa
tayari amesharudi shuleni, alikuwa akiniambia kuwa atasoma kwa bidii
ili ndoto yake ya kuwa daktari bingwa itimie aweze kusaidia watu
wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali,” alisema.
Hata hivyo, alisema maziko ya Happiness yanatarajiwa kufanyika leo huko Mbulu mkoani Manyara.
Mkurugenzi
wa JKCI, ambako Happiness alifanyiwa upasuaji, Profesa Mohamed Janabi
amesema taarifa hiyo imemshtua ikizingatiwa mtoto huyo alikuwa
anaendelea vizuri.
“Sikuwa
na taarifa, nitawasiliana na mama yake tujue hasa shida gani
ilitokea, maana zipo sababu nyingi labda alipita jirani na mitambo ya
umeme au simu, hizo ni sehemu hatarishi kwa mtu aliyewekewa betri kwenye
moyo,” alisema.
Happiness
alifanyiwa upasuaji huo wa historia nchini Julai 15, mwaka huu katika
Taasisi ya JKCI wa kuwekewa betri maalumu kwenye moyo ambayo kitaalamu
inaitwa ‘pacemaker’.
Kwa mujibu wa madaktari waliokuwa wakimtibia mtoto huyo, wakati alipopekekwa hospitalini hapo, mapigo yake ya moyo yalikuwa 20.
Walisema hali hiyo kwa mtoto si ya kawaida kwa vile anapaswa kuwa na wastani wa mapigo 60 hadi 100 kwa umri wake.
Mtoto Happiness alizaliwa na tatizo hilo ambalo mara nyingi hali hiyo huwakumba watu wazima.
Moja ya ndoto za mtoto huyo ambayo alinukuliwa akiisema ni kuwa daktari bingwa wa kutibu magonjwa mbalimbali.
No comments:
Post a Comment