Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli, jana tarehe 26 Novemba, 2016 ametunuku Kamisheni kwa Maafisa Wanafunzi 194 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kundi la 59/15 katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Hii ni mara ya kwanza kwa Maafisa Wanafunzi wa JWTZ kutunukiwa Kamisheni nje ya Chuo Cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli kilichopo mkoani Arusha, na ni mara ya kwanza kwa Maafisa Wanafunzi wa JWTZ kutunukiwa Kamisheni ndani ya Ikulu.
Maafisa hao ambao
168 ni wanaume na 26 ni wanawake, wametunukiwa Kamisheni katika cheo cha Luteni
Usu na sasa wamekuwa Maafisa Wapya wa JWTZ.
Kabla ya kutunuku
Kamisheni, Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli alikagua gwaride
rasmi lililoandaliwa na Maafisa wanafunzi wa JWTZ na baadaye akashuhudia
uhodari wa askari kutoka kikosi cha maadhimisho cha JWTZ waliofanya onesho la
gwaride la kimyakimya.
Akizungumza baada
ya chakula cha mchana katika ukumbi wa Ikulu, Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt.
John Pombe Magufuli alimpongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange,
Makamanda na Askari wote wa JWTZ kwa jukumu kubwa wanalolitekeleza la
kuhakikisha nchi ipo salama na amesema Serikali itahakikisha inaboresha zaidi
maslai na mazingira ya kazi kwa Jeshi hilo na vyombo vingine vya ulinzi na
usalama.
Aidha, Rais Magufuli
alisema ameamua tukio hili la kutunuku Kamisheni lifanyike Ikulu Jijini Dar es
Salaam kwa lengo la kutoa heshima kwa Maafisa wa JWTZ kama ambavyo Viongozi
wengine Serikalini wamekuwa wakipata heshima ya kuapishiwa Ikulu.
"Kwamba
Mawaziri tunapotaka kuwaapisha tunawaapishia hapa, Wakuu wa Mikoa tunawaapishia
hapahapa, Makatibu Wakuu tunawaapishia hapahapa, kwa nini hawa Maafisa wa Jeshi
tusiwaapishie hapahapa kwenye nyumba yao? Nyinyi ndio mnalinda nchi, nyinyi
ndio mnasimamia usalama wa nchi hii, lakini nikiuliza hapa inawezekana wengine
mpaka wamekuwa Mabrigedia Jenerali hawajawahi kukanyaga Ikulu, wakati hapa ni
kwenu" alisema Rais Magufuli.
Sherehe za
kutunuku Kamisheni kwa Maafisa Wanafunzi hao zilihudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe.
Kassim Majaliwa, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi
na Wakuu wa Jeshi la Ulinzi wastaafu na Majenerali wastaafu wa JWTZ.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
No comments:
Post a Comment