WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli imetoa kipaumbele kikubwa katika kuboresha sekta ya elimu nchini.
Amesema
hatua imejidhihirisha kwenye bajeti ya mwaka 2016/2017 ambapo Serikali
imetenga sh. trilioni 1.3 kwa ajili ya Sekta hiyo.
Waziri
Mkuu alitoa kauli hiyo Ijumaa, Novemba 25,2016 kwenye harambee ya
kuchangisha fedha kwa ajili ya uboreshaji wa shule nchini iliyofanyika
katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Saalam.
Akizungumza
katika harambee hiyo iliyoandaliwa na Taasisi ya Hassan Maajar Trust,
Waziri Mkuu aliwahakikishia wananchi kwamba bajeti ya Sekta ya elimu
itaendelea kuongezeka kadri uwezo wa Serikali utakavyokuwa unaimarika.
“Kama
mnavyofahamu, Serikali iliamua kuanza mara moja, utekelezaji wa Ilani
ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 ambayo inaelekeza Serikali kutoa elimu
bure kwa watanzania wote kuanzia shule ya Msingi hadi Sekondari,” alisema.
Alisema
uamuzi huo ulikuja na changamoto mbalimbali, ikiwemo upungufu wa
madawati kufuatia ongezeko kubwa la wanafunzi waliodahiliwa.
Alisema
kufuatia hali hiyo, tarehe 15 Machi, 2016 Serikali iliwaagiza Wakuu wa
Wilaya na Mikoa kuhakikisha tatizo la madawati linatafutiwa ufumbuzi wa
kudumu kwa kuwashirikisha wananchi na wadau mbalimbali wa ndani na nje
ya nchi.
“Napenda
kuwaarifu kwamba, jitihada hizo zimeanza kuzaa matunda kwani baadhi ya
mikoa tayari imemaliza tatizo hilo kwa shule za msingi na sekondari,
wakati Mikoa mingine ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji,”.
“Hadi
sasa Mikoa ambayo imekamilisha zoezi hilo kwa shule za msingi na
sekondari na kubaki na madawati ya ziada ni Arusha, Iringa, Kilimanjaro,
Manyara, Mbeya, Mtwara, Njombe, Pwani, Shinyanga, Singida na Tabora,” alisema.
Waziri
mkuu alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi na wananchi wa Mikoa hiyo
kwa kushiriki kikamilifu katika kumaliza kadhia hiyo kwa wanafunzi
ambao walikuwa wanakaa chini. “Huo ndio uongozi tunaoutaka, uongozi wa kusimama bega kwa bega na wananchi na kutatua kero zao”,.
Wakati
huo huo aliipongeza taasisi hiyo kwa kutoa mchango mkubwa katika
kumaliza upungufu wa madawati katika baadhi ya Mikoa nchini kupitia
harambee mbalimbali.
Alisema
kati ya mikoa 13 iliyopata ufadhili kutoka ya Taasisi ya Hassan Maajar
Trust, mikoa 10 kati yake imefanikiwa kumaliza tatizo la madawati kwa
shule zote za msingi na sekondari.
Mikoa hiyo ni pamoja na Njombe, Rukwa, Singida, Pwani, Shinyanga, Lindi, Mbeya, Iringa, Mtwara, na Kilimanjaro.
“Hii
inathibitisha kwamba jitihada za pamoja kati ya Serikali na asasi
zisizokuwa za Kiserikali zinaweza kuleta ufumbuzi wa changamoto nyingi
zinazolikabili Taifa letu,” alisema.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa taasisi ya Hassan Maajar Trust Fund,
Balozi Mwanaidi Maajar, alisema tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo miaka
mitano iliyopita imefanikiwa kuwainua watoto takribani 30,000 kutoka
sakafuni kufuatia kampeni ya Dawati kwa Kila Mtoto.
No comments:
Post a Comment