Ammy Ninje bwana, amfungukia Msuva, Ronaldo awatoa hofu watanzania - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, November 28, 2017

Ammy Ninje bwana, amfungukia Msuva, Ronaldo awatoa hofu watanzania



Sina shaka jina la Ammy Ninje limejipatia umaarufu mkubwa sana kwa siku za hivi karibuni baada ya kocha huyo kukabidhiwa mikoba rasmi ya kukiongoza kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kwenye michuano ya Kombe la Chalenji mwezi ujao.

Utakua unamfahamu lakini hiki ukifahamu kutoka ndani ya kinywa chake, Ninje hakuibukia tu nje ya mipaka ya bara la Afrika kama ambavyo wengi tunafahamu, bali safari yake ilianzia nchini Afrika Kusini.

Alikwenda nchini humo akiwa kama mchezaji baada ya kuambiwa na aliekua kocha wake wakati akiwa kijana mwenye damu inayochemka mwilini kuwa hakua mchezaji tu anaepaswa kuishia ndani ya mipaka ya Tanzania.

Baada ya maneno hayo kupasua ngoma za masikio yake, aliitazama miguu yake kisha akapiga konde sehemu ya juu ya kifua chake ambayo ndani yake ndipo ulipojikita moyo wa mwanadamu yeyote yule duniani na hapo ndipo alipoanza safari ya kutafuta mafanikio.

Maisha si rahisi bwana, pamoja na changamoto za hapa na pale hatimae Ninje aliibukia nje ya bara la Afrika na huko ndipo alipofanikiwa zaidi hali iliyofanya Mwaka 2017 kuchomoza kwenye ndani ya vichwa vya Watanzania.

Amedhamiria kuleta mabadiliko ya kweli ndani ya vichwa vya wachezaji wa Kitanzania, makocha, mashabiki na kila mwanafamilia wa mchezo huu wa soka ambao suala la kuibadilisha dunia lipo ndani ya uwezo wake.

Ndio maana Ninje anaamini kuwa kocha yeyote yule duniani anaeufahamu mchezo huu wa soka, ni lazima awafahamu wachezaji wake, “Kwa mwalimu yeyote yule ambae anaujua mpira kwanza ni lazima awafahamu wachezaji wote, hapo ndipo utajua utawasaidia vipi kila mmoja” anaeleza Ninje.

Alipokua huko ughaibuni, Ninje bwana alikua anaamini Watanzania hawana wanachokijua kwenye soka, ndio alikua anaamini hivyo, baada ya kufika hapa Tanzania Mwezi Julai alishangazwa sana na uwezo wa wachezaji wa Kitanzania na hapo hapo akakata shauri la kuacha kazi Uingereza, loh!

“Nimekuja hapa [Tanzania] [Mwezi] Julai, nilikua najua Watanzania hawajui kumbe Watanzania wanajua, wanajua sana, ndio sababu nikaacha kazi Uingereza.

“Tatizo Watanzania [mashabiki] tupo kwenye mtazamo hasi sana [kukosoa sana], wachezaji wetu wanajua sana inapaswa tuwaambie kuwa wanajua hawa wachezaji wetu,” hivyo ndivyo Ammy Ninje anavyoamini kua njia pekee ya kuwafanya wachezaji wa Tanzania kufikia levo kubwa hatupaswi kuwakatisha tamaa, tuwaambie kuwa wanajua.

“Juzi (Yanga ilipoifunga 5-0 Mbeya City), nilikua naangalia mchezo wa Mbeya City na Yanga, kuna kijana anaitwa Ronaldo (Idd seleman wa Mbeya City) anajua yule kijana, nilikua namsubiri nje nimwambie kuwa anajua hivyo ndivyo inavyotakiwa kuwa.”

Inasemekana kuwa hakuna kazi ngumu duniani kama kua kocha wa mpira wa miguu, Ninje alitangazwa kushika mikoba ya Kilimanjaro Stars alipanga mikakati gani ya kuiongoza timu hio kwenye michuano ya Kombe la Chalenji?

“Siku ya kwanza nilipoambiwa kuwa nakwenda kuwa kocha wa Kilimanjaro, nikaangalia video zao (wapinzani wa Kilimanjaro Stars kwenye Kombe la Chalenji), najua Libya wanapenda mpira wa pressing hio ndio sababu inayowafanya kuwa bora.”

Kuhusu kutowaita wachezaji wa kigeni wengi kwenye kikosi chake akiwemo Simon Msuva anaefanya vizuri, Kocha Ammy Ninje anasema “Unapokua na wachezaji wa kimataifa unatakiwa kuwa na akili, ni lazima uangalie ni mashindano gani unamwita, na hio ndio sababu iliyonifanya nisiwaite, tunatakiwa tuwatengeneze kina Msuva wengine.”

Tunakwenda kwenye michuano ya Kombe la Chalenji, kocha Ammy Ninje amewatoa hofu Watanzania kwani anaamini sana wachezaji alio nao wanatosha kupambana na kuleta taji nchini Tanzania.

“Watanzania wasiwe na hofu, nakiamini kikosi changu, nakijua kikosi nilichonacho, tunakwenda kushinda,” amesema Ninje na kuongeza, “Tutaondoka Novemba 30 na tutakua na mechi Disemba 3.”

No comments:

Post a Comment