
Siku
chache baada ya kiongozi wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship
Askofu Zachary Kakobe kusema kuwa ana fedha nyingi kuliko Serikali,
Mamlaka ya Mapato nchini TRA imejipanga kuanza kufuatilia ulipaji wake
wa kodi.
Kamishna
Mkuu wa TRA, Charles Kichere amesema mamlaka yake imeipokea kwa furaha
kauli ya Askofu Kakobe na inataka kujiridhisha vyanzo vya utajiri huo.
Kichere
amesema TRA inafahamu kuwa shughuli za kidini hazitozwi kodi lakini
inataka kufahamu kama fedha hizo za Askofu Kakobe zinatokana na sadaka
pekee au kuna shughuli nyingine za kiuchumi.
"Tumefuatilia
hakuna kumbukumbu za Askofu Kakobe kulipa kodi, sasa tumeona tumfuate
maofisa wetu wakajiridhishe kama fedha hizo anazozizungumzia zinatokana
na sadaka,"
"Na
kama hana shughuli zozote za kiuchumi ikiwa ina maana utajiri huo
unatokana na sadaka ni jambo la kushtua kidogo lakini sisi tutaishia
hapo,"
Amesema
katika taarifa za mamlaka hiyo wapo watu wengi wenye fedha nyingi na
kumbukumbu zao za kodi zipo lakini Askofu Kakobe si miongoni mwao.
Kichere amemwomba Askofu Kakobe kutoa ushirikiano kwa maofisa wa TRA watakaomtembelea kwa ajili ya shughuli hiyo ya ukaguzi.
Kuhusu
kwanini uhakiki huo umekuja sasa Kichere amesema ni baada ya kusikia
ana fedha nyingi kuliko Serikali wakati anafahamika ni kiongozi wa
taasisi ya dini.
No comments:
Post a Comment