Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza
mtambo wa kutengenezea mbegu za pamba ulioko mkoani Mbeya, kuondolewa
mara moja na kupelekwa kwenye mikoa inayolima zao hilo huku akihoji
sababu za msingi zilizochangia mtambo huo kuwekwa huko.
Akizungumza na wadau wa zao hilo Waziri
Mkuu alitoa agizo hilo na kuitaka wizara inayohusika kuchukua hatua
mara moja huku akivitaka viwanda vya ndani vyenye uwezo wa kuzalisha
mbegu kujitokeza.
Amesema haiwezekani mtambo unaotengeneza
mbegu za pamba ukawekwa kwenye mkoa ambao haulimi zao hilo na kuhoji
kulikuwa na sababu gani ya msingi ya kuwekwa mkoani Mbeya, ndipo aliamua
kuagiza kuondolewa na kupelekwa kwenye mikoa inayolima pamba.
Hata hivyo Majaliwa alisema kiwanda cha
Quiton ambacho kimewekeza nchini kwa ajili ya kutengeneza mbegu za
pamba aina ya Quiton lakini cha kusikitisha mpaka msimu wa kilimo
unafika hakuna mbegu na hii kampuni inamilikiwa na Wazimbabwe na wao
wanalima pamba nchini kwao katika hili tutafakari.
‘’Tunataka zao la pamba liwe na
mafanikio makubwa na haya yote yanapaswa kusimamiwa na watumishi wa
serikali ili kuweza kumkomboa mkulima wa pamba, kulima kilimo chenye
tija ambacho kitawaletea mabadiliko ya kiuchumi kwani asilimia 80 ya
watanzania wanategemea kilimo” amesema waziri mkuu.
Kwa upande wake Waziri wa Chakula na
Ushirika Dk Charles Tizeba amesema katika msimu uliopita jumla ya kilo
133 milioni za pamba zimezalishwa , ambapo kwenye msimu wa mwaka huu
wanatarajia kuzalisha kilo 600 milioni za pamba huku uzalishaji wa tija
utaongezeka kwa ekari kutoka kilo 200 hadi 500.
Amesema ekari 1,100,000 zimepandwa
mbegu zisizo na manyoya ambapo lengo ni kufikia ekari 3,000,000 milioni
na kuongeza kuwa umetumika utaalamu katika upandaji ,huku akibainisha
kuwa tayari kuna chupa 4,764,000 za dawa za kuuwa wadudu zimepatikana
ambazo zitasambazwa kwa wakulima kwa awamu nne.
Awali akizungumza kwenye mkutano huo
mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack amesema jumla ya ekari 128,668
za pamba zimelimwa mpaka sasa mkoani Shinyanga, kutoka kwa wakulima
24,175 ambapo wanaendelea kutoa elimu kwa wakulima.
No comments:
Post a Comment