AWESO AWATAKA WAKANDARASI KUKAMILISHA MIRADI YA MAJI KWA WAKATI ILI KUONDOA TATIZO LA MAJI NCHINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, January 20, 2022

AWESO AWATAKA WAKANDARASI KUKAMILISHA MIRADI YA MAJI KWA WAKATI ILI KUONDOA TATIZO LA MAJI NCHINI





Na Okuly Julius, Dodoma 

Waziri wa Maji Juma Aweso ameagiza wazabuni wa Maji kufanya kazi kwa muda na mkataba walivyokubaliana kwani Watanzania wanataka maji siyo siasa.

Aweso ametoa agizo hilo leo jijini Dodoma wakati akishuhudia utiaji saini wa mikataba ya ununuzi wa pampu za maji 310 zinazolenga kufungwa katika mikoa mbalimbali nchini.

Mkataba huo umesainiwa kati ya Mamlaka ya maji na Usafi wa Mazingira vijijini (Ruwasa) na wazabuni Wazawa kampuni 4 moja ikiwa na kandarasi mbili ambapo Sh8.89 bilioni zitatumika kununua mashine hizo.

Waziri amesema wakati uliopo si wa kuweka maneno kwenye miradi ya maji bali iwe ni vitendo zaidi ili Serikali ijivunie kufanya kazi na wakandarasi Wazawa.

"Lakini kwa upande wenu Ruwasa nasisitiza malipo kwa wakati, siyo mtu amefanya kazi halafu anaendelea kudai malipo yake wakati pochi la mama limetema, haki iende na wajibu," amesema Aweso.

Kwa upande mwingine kiongozi huyo ameagiza kuanzia Sasa pampu zifungwe katika maeneo yanayotoa maji hata kabla ya kujengwa kwa matenki ili Wananchi waanze kunufaika kuliko kusubiri ujenzi wa matenki ambao huchukua muda mrefu kukamilika.

Kuhusu miradi ya maji ametaka Sasa watupie macho mkoa wa Tanga baada ya kuwa wamemaliza Katavi, Rukwa na Songwe ambako ameshindwa kuzindua miradi yote kutokana na wingi wake na muda aliokuwa nao.


Mkurugenzi wa Ruwasa Clement Kivegalo amesema wazabuni waliopewa kazi hiyo watafanya kwa wakati kwa kuwa malipo na stahiki zote katika tenda hiyo zimekuwa tayari kinachoangaliwa ni kazi tu.

Kivegalo amesema namna ilivyo sasa kilio cha maji kinakwenda kuwa historia katika nchi hii lakini akasisitiza usimamizi wa karibu wa miradi ili iwe na ubora na thamani ya fedha.

Mkurugenzi huo amemhakikishia Waziri kuwa Ruwasa itafanya kazi usiku na mchana na karibu na wazabuni na wakandarasi bila kuchoka hadi waone wanatimiza ndoto ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mwanamke ndoo kichwani.

Akizungumza kwa niaba ya wazabuni wengine, James Masage Kutoka kampuni ya Tributa Energy amesema kwa upande wao hakutakuwa na kikwazo ikiwa watapewa malipo ya kazi zao kwa wakati.

Masage amesema fedha zilizotengwa ni nyingi kwa hiyo hawawezi kufanya vitu kinyume na makubaliano kwani nao wanatafuta kuaminiwa na Serikali katika huduma zao.

No comments:

Post a Comment