Na Oscar Assenga,MKINGA
WAKULIMA wa Mwani Katika Maeneo ya Boma Subutini Kata ya Boma wilayani Mkinga mkoani Tanga wameitaka Serikali kuona namna ya kuzibiti uvuvi wa kokoro ambao ndio chanzo kikubwa cha kuathiri viumbe hai wa bahari na mazao ya mwani.
Walitoa wito huo mwishoni mwa wiki katika mdahalo wa wavuvi na wakulima wa mwani katika Kata ya Boma wilayani Mkinga ikiwa ni muendelezo wa mradi wa kujenga uwezo kwa matumizi ya rasilimali za bahari ngazi ya kata.
Mradi huo unaendeshwa na Shirika la Umoja wa Wasaidizi wa Sheria wilayani Mkinga (Uwashem) ukifadhiliwa na Shirika la 4H Tanzania pamoja na We World ambapo kwa sasa utasaidia kuwaweka kwenye hali ya amani ili waweze kushirikiana kwa pamoja kufanya kazi bila kuwepo mvutano wowote.
Akizungumza katika mdahalo huo Mwaita Miraji alisema kwamba uvuvi wa kutumia kokoro umekuwa kikwazo kikubwa kwa ustawi wa viumbe vya baharini lakini pia kuharibu zao la mwani jambo ambalo linapelekea kuwarudisha nyuma kimaendeleo.
Alisema kwamba wanaishukuru Serikali kwa kuzibiti na kutokomeza uvuvi haramu katika maeneo mbalimbali hapa nchini lakini hivi sasa wanawaomba waelekeze nguvu kwenye kutekeleza uvuvi wa kokoro ambao nao umekuwa ukileta athari kubwa.
“Tunaiomba Serikali itumie mbinu walizotumia kutokomeza uvuvi haramu wautumie kutokomeza wa Kokoro ambao umekuwa ukileta athari kubwa hususani katika mazao ya mwani yaliyopo baharini”Alisema
Aidha alisema kwamba uvuvi wa kokoro sio mzuri kutokana na kwamba unachangia kuharibu mazalia ya bahari pamoja na kuadhimia kwa pamoja uvuvi huo unaathiri ustawi wa viumbe wa bahari na hivyo kupelekea mazao ya bahari kuadimika .
“Tunaomba ikiwezekana uvuvi wa kokoro ubadilishwe jina na kuitwa uhalifu wa Kokoro lengo likiwa kuhakikisha unatokomezwa kwenye jamii lakini Serikali iwekeze nguvu zake katika mapambano ya kutokomeza uvuvi huo “Alisema
Naye kwa upande Gonda Mwaita ambaye ni mkulima wa mwani alitaka Serikali iweke sheria kali za kuwadhibiti wavuvi wanaokamatwa wakivua kupitia kokoro kutokana na kwamba umekuwa ukichangia kuharibu mazalia ya bahari ikiwemo mashamba ya mwani na hivyo kurudisha nyuma juhudi za wakulima hao.
“Lakini pia kuwepo na faini kubwa mtu akikamatwa analipa laki tano kama faini wakati huo tayari unakuwa umeshaharibu mashamba ya mwani baharini huo ni uhalifu hivyo iongezwe kwa lengo la kudhibiti uendelee”Alisema
Awali akizungumza katika mdahalo huo Afisa Mtendaji wa Kata ya Boma Hadija Mganga alisema uwepo wa elimu hiyo itawasaidia wakulima wa mwani kwani wamekuwa hawana amani na ukulima wao unakuwa wa kuzorota kutokana na kuathiriwa na uvuvi wa kokoro na kupelekea mtu mmoja moja kushindwa kujimudu katika uchumi.
Alisema kwamba jambo hilo wakishirikiana na watendaji wa vijiji na kata kusimamia kwa kupewa nguvu ili kuweza kuwatoa kwenye hilo jambo kwa sababu Kata ya Boma ndio kitovu cha shughuli za Mwani na uwepo wa kiwanda kidogo cha ukaushaji wa mwani ili kudhalisha.
Hadija alisema kwamba kwa kuharibu mazao hayo kunarudisha nyuma na kuwavunja moyo hivyo wanalishukuru shirika la uwashem kutoa elimu na wananchi wametoa mapendekezo ya Kamati za BMU zijengewe uwezo na zisimamie hasa majukumu yao.
Alisema mwingiliano wa wavuvi na wakulima wa mwani yakitokea wakibishana na kugombana mwisho wa siku wanaumizani na mwisho wa wiku sio jambo nzuri kwa Taifa na Kamati ngazi ya kata wapo tayari kushirikiana na vyombo vya ulinzi kuweza ktoa taarifa za kina kuhusu hali hiyo chanzo ni nini na wanaamini wakishirikiana kwa pamaoja na kuwa agenda yao kubwa kwenye vikao vyao na hivyo kuweza kupiga vita vitendo hivyo.
Hata hivyo alisema kwa upande wake Mratibu wa Uwashemu Salehe Sokoro alisema kwamba anaamini changamoto ambazo zimeelezwa katika mdahalo huo zimechukuliwa na zitakwenda kufanyiwa kazi ili kukomesha vitendo vya namna hiyo kwenye maeneo husika

No comments:
Post a Comment