
Na Veronica Mrema - Pretoria
Ulimwengu wa sayansi na teknolojia unasonga kwa kasi ya ajabu. Mataifa makubwa duniani yanawekeza kwenye ubunifu, utafiti wa kisayansi, na teknolojia za kisasa.
Teknolojia kama akili unde, kilimo cha kisasa na tiba za kibunifu zaidi zinabadilisha maisha katika mataifa makubwa duniani.
Karne ya akili unde [AI], roketi zinavuka anga, kuna uvumbuzi na gunduzi nyingi katika teknolojia mpya kwa kasi ambayo dunia haijawahi kushuhudia.
Mataifa makubwa yanawekeza, yanashirikiana, na yanapasha habari za sayansi kwa umma wao kwa kasi.
Lakini upande mwingine wa dunia, ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika [SADC], bado kuna pengo kubwa katika mawasiliano ya sayansi.
Watafiti wanagundua, Serikali zinafanya miradi, taasisi zinavumbua, lakini taarifa 'hazitembei' kwa kasi inayohitajika.
Bado haziwafikii vema wananchi wake, hazijengi uelewa na hazifanyi sayansi kuwa sehemu ya maisha ya kila siku.
Ndani ya SADC, bado kuna pengo kubwa kati ya maendeleo ya ki-sayansi na jinsi ambavyo taarifa hizo zinavyowafikia wananchi.
"Kwa sababu nchi nyingi za SADC bado hazina mkakati wa mawasiliano katika masuala ya sayansi,".
Yameelezwa hayo na Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Kimataifa na Afrika, Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (DSTI), Afrika Kusini Mwampei Chaba.
Ni wakati alipokuwa akifungua mdahalo wa siku moja wa waandishi wa masuala ya sayansi kutoka nchi 18 wanachama wa SADC.
Amesema kutokana na pengo lililopo katika upashanaji habari kuhusu maendeleo ya sayansi katika nchi hizo, ndiyo maana DSTI iliona vema kuwaleta pamoja waandishi wa habari na kufanya mdahalo huo.
Ni katika mkutano wa kimataifa wa waandishi wa habari za masuala ya sayansi [WCSJ2025] unaofanyika Pretoria nchini Afrika Kusini.
Akifungua mjadala huo, aliweka wazi changamoto kubwa wanazokutana nazo waandishi wa sayansi katika ukanda huu.
“Nchi nyingi katika SADC bado hazina mkakati wa ushirikiano katika mawasiliano kuhusu sayansi. Hiyo ndiyo sababu upashanaji habari za sayansi unakumbwa na changamoto nyingi.”
Ameongeza "Ukosefu wa mkakati huo unawafanya waandishi wengi kukosa ushirikiano wanaohitaji kutoka kwa Serikali zao.
"Mnashindwa kuwa karibu na watafiti, mnakosa mazingira rafiki ya kupata habari, pamoja na fursa za ufadhili au mwaliko kwenye matukio muhimu yanayohusu sayansi na uvumbuzi.
Amesisitiza "Kwa hivyo, katika nchi yako na unataka kupata ushirikiano kutoka Serikali [kuandika kuhusu habari fulani inayohusu sayansi] au unataka watambue kazi yako.
"Unataka kufadhiliwa kwa baadhi ya kazi zako. Unataka kualikwa kwenye matukio [kwa wengi wenu], itakuwa ngumu kwa kuwa hawana mkakati wa ushirikiano kuhusu hilo," amesema.
"Mkirudi nchini mwenu kafuatilieni hili kwa undani, nendeni mkaulize wizara [zinazohusika na masuala ya] sayansi, wizara za mawasiliano [iwapo] wameandaa mkakati?.
Hii ni mara ya kwanza kwa Bara la Afrika kuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa waandishi wa habari za sayansi, afya, mazingira na mambo mengine yanayohusiana na hayo.
Mdahalo huo kwa ajili ya waandishi wa habari kutoka SADC ulilenga kuwaleta pamoja kujadiliana namna gani watasukuma mbele masuala ya sayansi ndani ya nchi zao kwa upashanaji habari.
"Hii ni warsha ya mafunzo yenye umuhimu mkubwa kwetu. wazo hili lilikuja kwetu mwaka 2022 tulipoandaa Mkutano wa Sayansi Duniani (World Science Forum).
" ambao ulikuwa wa kwanza kuandaliwa barani Afrika. Kwa hivyo, tulitengeneza historia mwaka 2022 kwa kuandaa mkutano wa Sayansi Duniani barani Afrika.
"Kisha tukaamua kuwa kuleta fursa kama hii barani Afrika bila waandishi, waandishi wa sayansi kuwa kwenye chumba, kungekuwa kupoteza.
Ameongeza "Tunawezaje kuwasilisha kile tunachofanya katika mkutano, kama idara, kama serikali barani Afrika, kama taasisi zinazofanya utafiti, ikiwa hatuna uandishi wa sayansi kwenye chumba?
"Pia tuligundua kuwa waandishi wa sayansi bado hawana uwezo wa kutosha kuhusiana na uandishi na kuandika makala za sayansi.
"Hivyo basi, tuliona hitaji la kuunda ushirikiano. Na Stellenbosch alishirikiana nasi kwa kiwango kikubwa.
Amesema walianza kupanga warsha ya mafunzo, yenye vipengele vingi, ambayo itasaidia kujenga uwezo wa waandishi wa habari katika kuwasilisha kazi tunazofanya kwa ufanisi zaidi.
"UNESCO ilifadhili baadhi ya wajumbe mwaka 2022, na imeendelea kuwa mshirika wetu tangu wakati huo.
"Sekretari ya SADC pia imekuwa mshirika wetu, na tunashukuru sana michango waliyotoa kwa waandishi wa SADC kuungana nasi.
"Chama cha Waandishi wa Sayansi wa Afrika Kusini (SASJA) pia kimeungana nasi, na sisi pia tuko kwenye mshirika mkubwa katika mkutano mwingine wa kihistoria," amebainisha,
Amesema mkutano wa WCSJ2025 walioandaa mwaka huu unatengeneza historia mpya nyingine na walitaka kuwa sehemu ya historia hiyo.
Amesema Afrika Kusini waliunda mkakati wa mawasiliano na ushirikiano katika masuala ya sayansi tangu mwaka 2015 na kwamba walichelewa mno kuunda.
"Taasisi yetu ilianzishwa Juni 2004, hivyo karibu miaka 11 baadaye, tu wakati huo tu tulikuwa na mkakati wa ushirikiano wa sayansi unaotekelezwa kwa sasa, na mchakato wa ukaguzi upo.
Amebainisha "Mwaka huu SADC ilishiriki katika G20. Tulikuwa Rais wa G20 na GSTI ilipanga kile kinachoitwa Wiki ya Utafiti na Ubunifu [Research and Innovation Week].
"Pia tulipitisha hati maalumu inayoitwa Azimio la Ushirikiano wa Sayansi wa G20 (G20 Science Engagement Resolutions).
"Hati hiyo inahimiza nchi za G20 kuweka sayansi kati-kati ya jamii inahimiza kuongeza ufahamu katika jamii zetu kuhusu thamani ya sayansi, na kuwasilisha sayansi kwa njia jamii zinaweza kuelewa.
"Kwa nini tunapaswa kufanya hivyo? Ni kwa nini hii ni muhimu? Sayansi haifadhiliwi vya kutosha, na hili ni changamoto katika jamii nzima.
Amesisitiza "Ikiwa thamani ya sayansi haifahamiki, ikiwa athari ya sayansi haijulikani kwa serikali zetu, jamii zetu, wafadhili wetu na wachangiaji.
"Basi mpango wa kufafanua ni ninyi walioko hapa. Ninyi ndio midomo yetu. Ninyi ndio mabalozi wetu wa kuwasilisha sayansi kwa jamii.
"Mara sayansi itakapofahamika, mara thamani ya sayansi itakapothibitishwa kwenye hatua za vitendo, kwenye jamii, kwenye vijiji.
"Basi mna nafasi nzuri ya kupata ufadhili kutoka Serikalini, ufadhili kutoka kwa wafadhili na kadhalika.
"Kwa hivyo, jukumu lenu ni muhimu sana, na tunategemea ninyi kusaidia kuunganisha pengo," amesema na kuongeza,
"Napenda kuwahimiza kwamba katika wiki hii, mchukue fursa ya warsha nyingi zinazofanyika kuhamasisha sayansi.
"Matumizi ya data, sita-sita kusema kwamba sayansi inapaswa kuwa kati-kati ya jamii, elimu, viwanda, ili kuendesha maendeleo kwa ujumla.
"Na haiwezi kuwa katikati ikiwa ninyi hufahami jinsi ya kuwasilisha sayansi. Nami naamini hatuhitaji kuwa wanasayansi ili kuelewa sayansi.
"Sayansi inapaswa kufafanuliwa kwa mtu wa miaka 85 na mtoto wa miaka 5. Bila kutumia maneno magumu.
Amesisitiza "Ikiwa mtu hawezi kueleza, ikiwa mwanasayansi unayemhoji hawezi kueleza sayansi yao kwa njia unayoielewa, basi hawafanyi kazi nzuri.
"Na pia unapaswa kuwa na uwezo wa kuhimiza wanasayansi kuzungumza na kuwasilisha sayansi kwa njia kila mtu anaweza kuelewa.
Amehoji "Je, unajua waandishi mashuhuri wa sayansi barani Afrika? Kwa nini haingewezekana iwe wewe?
"Kwa nini haingewezekana iwe wewe?” aliuliza, akiwahimiza washiriki kuwa wao wenyewe wanaweza kuwa waandishi mashuhuri wa sayansi Barani Afrika.
“Kuna waandishi wa sayansi mashuhuri duniani kote, lakini sio barani Afrika. Afrika inahitaji sayansi kwa maendeleo zaidi kuliko kanda nyingine yoyote duniani.
"Hivyo basi, tufanye lengo letu kuwa na waandishi mashuhuri wa sayansi katika jamii zetu, nchi zetu, ndani ya SADC na barani kote.
Amesisitiza "Vinginevyo, mbona mko hapa? Kwa nini mko hapa ikiwa hatutumiwe kile tulicho nacho kuwasilisha sayansi na kuifanya iwe ‘fashionable’?”
Amehimiza waandishi wa habari kutumia vema majukwaa ya kidigitali kama fursa ya kufikisha taarifa muhimu zinazohusu sayansi kwa kundi la vijana ambalo kubwa lipo kwenye majukwaa hayo.
"Kila mtu yupo TikTok, kila mtu yupo YouTube, lakini lazima tuone maudhui ya sayansi pia kwenye TikTok au YouTube.
"Tumia majukwaa haya maarufu kuwasilisha sayansi. Tuwafikie vijana walipo kwenye YouTube, Instagram na mitandao mingine na kuwapa elimu ya sayansi kwa njia wanayoielewa.”
Picha zote kwa hisani ya DSTI



No comments:
Post a Comment