Na Okuly Julius Dodoma
Ameyasema hii leo Februari 21,2022 wakati wa ugawaji wa kompyuta 300 kwa vyuo vya ualimu 13 nchini kupitia ufadhili wa serikali ya nchi ya Canada.
Prof.Mkenda amesema serikali ya Canada kupitia mradi wake wa Teachers Education Support imekuwa na mchango mkubwa kwa Tanzania hasa katika usaidizi wa vifaa vya TEHAMA hususani Kompyuta ambapo imepunguza mahitaji kutoka wanachuo 28 kwa kompyuta moja hadi wanachuo wawili kwa kompyuta moja.
Pamoja na hayo Prof.Mkenda ameongeza pia Serikali itashirikiana vyema na serikali ya Canada katika kuwaendeleza wakufunzi wa vyuo vya Ualimu pamoja na Ufundi ikiwepo kuwapeleka baadhi ya wakufunzi nchini humo kupata maarifa ya ufundishaji katika vyuo mbalimbali nchini Canada.
Pia Prof.Mkenda amebainisha kuwa serikali itapitia upya maswala ya Mitaala inayotumika Mashuleni kwa sasa na vitabu mbalimbali vinavyotumika kufundishia wanafunzi ili kwa pamoja kuja na sera nzuri itakayoweza kusaidia kupata matokeao mazuri ya juhudi hizi za Serikali.
Aidha,ameongeza kuwa Serikali itaendelea kufuatilia uwiano mzuri kati ya wanafunzi na walimu akisema kuwa kuna baadhi ya shule ina wanafunzi wengi huku ikiwa na walimu wachache sana na kuna zingine zina walimu wengi na wanafunzi wachache hivyo serikali itashughulikia suala hilo kwa kuhakikisha kila shule inakuwa na walimu wa kutosha kulingana na wingi wa wanafunzi waliopo.
"Tutashirikiana pia na Ofisi ya Rais TAMISEMI kuona ni jinsi gani ya kuhakikisha kila shule inakuwa na walimu wa kutosha kwa sababu kumekuwa na wimbi kubwa la walimu katika shule za mijini ukilinganisha na shule za vijijini hili nalo tutalifanyia kazi kwa uangalifu"Amesema Mkenda
Prof.Mkenda amewaagiza Waakuu wa Vyuo kusimamia vyema vifaa hivyo vya TEHAMA kwa matumizi sahihi yaliyokusudiwa ili kuleta tija na matokeo mazuri kwa wakufunzi pamoja na wanafunzi watakaokuwa wanavitumia.
Kwa upande Wake Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga amesema bado kuna changamoto ya uhaba wa walimu hivyo wao kama Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia watatengeneza Sera ya kuhakikisha wanatatua changamoto hii ya upungufu wa walimu.
Hata hivyo Mh.Kipanga ameipongeza Serikali kwa namna ambavyo wamewekeza katika miundombinu ya madarasa kwa ajili ya wanafunzi kujifunza katika mazingira safi na salama.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Prof.Calorine Nombo amesema Serikali ya Canada imegharamia Jumla ya Dola za KiCanada Milioni 53 katika utekelezaji wa mradi huo ambao utakwenda kuwa tija kwa wanafunzi na wakufunzi wa vyuo vya Ualimu Tanzania.
Katika mgawanyo wa Kompyuta hizo 300 kuna vyuo Vinne (4)vimepata Kompyuta 30 huku Vyuo Tisa (9) vikipatiwa jumla ya Kompyuta 20 kila mmoja.
Vyuo vya ualimu vilivyokabidhiwa kompyuta 30 ni Korogwe,Morogoro, Mpwapwa na Butimba. Wakati vilivyokabidhiwa kompyuta 20 ni Ilonga, Kleruu,Marangu, Mtwara,Patandi,Shinyanga,Tandala,Tarime na Vikindu.
![]() |
Baadhi ya Wakuu wa Vyuo vya Ualimu nchini wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Na viongozi wengine wa Wizara hiyo. |
No comments:
Post a Comment