WAMACHINGA NCHINI WATAKIWA KUTUMIA TEHAMA KATIKA SHUGHULI ZAO ILI KUPIGA HATUA KIUCHUMI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, February 22, 2022

WAMACHINGA NCHINI WATAKIWA KUTUMIA TEHAMA KATIKA SHUGHULI ZAO ILI KUPIGA HATUA KIUCHUMI



Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula akizungumza na viongozi wa Wamachinga kutoka Mikoa mbalimbali nchini katika kikao kazi kilichofanyika jijini Dodoma chenye lengo la kuwakaribisha katika Wizara.


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju akielezea lengo la Wizara kukutana na viongozi wa Wamachinga kutoka Mikoa mbalimbali nchini katika kikao kazi kilichofanyika jijini Dodoma.


Kwaya ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum wakitumbuiza katika kikao kazi kilichowakutanisha Viongozi wa Wizara na Viongozi wa Wamachinga kutoka Mikoa ya Tanzania Bara jijini Dodoma.


Baadhi ya Viongozi wa Machinga kutoka Mikoa ya Tanzania Bara, Viongozi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Viongozi kutoka Wizara mbalimbali, Taasisi za Fedha na wadau wengine wakiwa katika kikao kazi kilichowakutanisha Viongozi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Viongozi wa Wanamachinga nchini jijini Dodoma.

***************

Na WMJJWM, Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula amewataka Wamachinga kutumia fursa zilizopo nchini ikiwemo Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Shughuli zao ili kupiga hatua kiuchumi.

Akifungua kikao cha kuwajengea uwezo Viongozi wa shirikisho la Wamachinga, kilichofanyika Jijini Dodoma leo tarehe Febriary 22, 2022 Dkt. Chaula amesema kwa sasa Teknolojia inakuwa kwa kasi hivyo uwezekano wa kupata masoko na bidhaa umerahisishwa ikilinganishwa na kipindi cha Nyuma ambapo Teknolojia ilikuwa duni.

Dkt. Chaula amesema, fursa nyingine zilizopo ni pamoja na amani na utulivu uliopo nchini, mikopo ya Maendeleo kutokana na mapato ya Halmashauri, pamoja na ardhi.

"Tunamshukuru Mhe. Rais kwa kuona umuhimu wa kuanzisha Wizara hii na kuipa Dhamana ya kushughulikia Makundi Maalum ikiwemo wamachinga, maana yake ni kwamba, anawasikiliza, anawatambua na kuwaelewa" amesema Dkt. Chaula.

Dkt Chaula amewataka pia, kuimarisha ushirikiano miongoni mwao, Serikali na Wadau wengine ili kukuza zaidi mitandao ya biashara zao na kuboresha maisha kwani wao wenyewe ni fursa katika kukuza uchumi wa Taifa. Pia wasikubali kutumiwa kwa namna yoyote ili kuwatenganisha.

Dkt. Chaula amebainisha kuwa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, ametoa jumla ya sh. bilioni 5 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Wamachinga hivyo Serikali itahakikisha fedha hizo zinatumika kwa ufanisi.

Awali Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju akitoa maelezo kuhusu kikao hicho amesema hadi tarehe 31 Januari usajili wa shirikisho la machinga ulikuwa umekamilika.

Mpanju amesema lengo la kikao hicho ni kuwasikiliza na kuwapa fursa ya kupata elimu ya masuala mbalimbali ili kuongeza ufanisi katika shughuli zao.

"Nia ya Serikali ni kuhakikisha kundi hili linapata Maendeleo kupitia shughuli zao hivyo kikao hiki kinawajengea uelewa wa mambo muhimu ikiwemo sheria, kanuni na taratibu za Serikali" amesema Mpanju.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Machinga nchini (SHIUMA), Ernest Matondo, wameishukuru Serikali kupitia benki ya NMB kwa kuwakutanisha kwani wana imani matokeo ya kikao hicho ni kuboreshwa zaidi kwa mazingira ya shughuli zao.

"Miundombinu kwenye masoko haijakaa vizuri, hivyo kama alivyosema Katibu Mkuu fedha hizo zitaboresha miundombinu ili Wamachinga waweze kufanya kazi vizuri zaidi, tunamshukuru pia Mhe. Rais kwa kulitambua kundi hili na kuliweka katika Wizara mahususi" amesema Matondo.




No comments:

Post a Comment