Ikiwa ni siku ya pili ya mafunzo kwa watumishi waliohamishiwa kutumika katika Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi Victoria Elangwa amewataka watumishi hao kufuata miongozo ya taasisi katika kutekeleza majukumu yao ili maamuzi yawe na mlengo wa kuinua taasisi na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Akiwasilisha mada katika darasa hilo Afisa Rasilimali Watu, Ruth Magesa amekabidhi miongozo yote inayotumika katika utendaji kazi wa mamlaka hiyo kwa watumishi hao ili waweze kuitumia kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Miongoni mwa miongozo iliyotolewa na Mamlaka ni pamoja na Sera ya Ukimwi na Magonjwa yasiyo ya kuambukiza (HIV and NCD), Muundo na Majukumu ya Mamlaka yaliyoidhinishwa, Sera ya kufichua maovu, Sera ya malalamiko, muongozo wa zawadi na ukarimu na mingineyo.
Pamoja na kugawa miongozo hiyo, Magesa amewataka watumishi hao kuzingatia mtiririko wa majukumu na uongozi katika utendaji wao wa kila siku.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani Pauline Mganga amewataka watumishi hao kuimarisha ushirikiano baina yao na kitengo hicho ili kuweza kutatua na kueleweshana namna bora ya kutekeleza majukumu kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazoisimamia mamlaka.
Amesema, kazi ya kitengo hicho katika mamlaka hiyo na nyingine ni kukagua namna idara na vitengo vinavyotekeleza majukumu yake na kuishauri mamlaka ili iweze kusimamia sheria na taratibu kikamilifu.
Akihitimisha mafunzo hayo kwa siku ya pili Kaimu Meneja wa Kitengo cha Rasilimali watu Naomi Fwemula aliwashukuru watoa mada na viongozi wakuu wa taasisi kwa elimu iliyotolewa kwa watumishi hao.
Aidha, amewashukuru na kuwatakia utekelezaji mwema wa majukumu katika vituo vyao vipya vya kazi.
Wakati huohuo Joshua Ngondya Kaimu Meneja Kanda ya Kati, akizungumza kwa niaba ya watumishi wengine ameishukuru mamlaka kwa kuandaa utaratibu wa mafunzo na kukiri kuwa wamepata mwanga wa namna ya kwenda kutekeleza majukumu yao katika vituo vyao vya kazi.
Mafunzo hayo ni ya siku tatu yaliyoanza jana tarehe 9 hadi tarehe 11 Februari ambapo leo yamehitimishwa rasmi kwa waajiliwa wageni na siku ya mwisho mafunzo yatahusisha watumishi wote wa TFRA ili kuwapa uelewa katika suala la Maadili katika Utumishi wa Umma.
No comments:
Post a Comment