YALIYOJIRI  WAKATI WA TAARIFA YA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI NA MKURUGENZI WA IDARA YA HABARI-MAELEZO, GERSON MSIGWA KUHUSU UTEKELEZAJI WA SHUGHULI MBALIMBALI ZA MAENDELEO YA SERIKALI, FEBRUARI 13, 2022, UKUMBI WA WIZARA YA UTALII NA MAMBO YA KALE, ZANZIBAR - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, February 13, 2022

YALIYOJIRI  WAKATI WA TAARIFA YA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI NA MKURUGENZI WA IDARA YA HABARI-MAELEZO, GERSON MSIGWA KUHUSU UTEKELEZAJI WA SHUGHULI MBALIMBALI ZA MAENDELEO YA SERIKALI, FEBRUARI 13, 2022, UKUMBI WA WIZARA YA UTALII NA MAMBO YA KALE, ZANZIBAR



*ZIARA YA MHE. RAIS*
#Leo hii nitaanza na taarifa kuhusu ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan. Kama wote mnavyojua Mhe. Rais yupo katika ziara nje ya nchi, hivi navyozungumza nanyi yupo nchini Ufaransa ambako amehudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliojadili kuhusu rasilimali bahari. 

#Ameshuhudia utiaji saini wa mikataba na makubaliano kuhusu ufadhili wa miradi na shughuli mbalimbali za maendeleo hapa nchini na ametembelea kituo cha kuwezesha wajasiriamali kiitwacho Station F Start-up ambacho kinatoa fursa kwa wajasiriamali wadogo kupata elimu ya ubunifu wa kuanzisha biashara, fursa za mitaji yenye masharti nafuu na masoko ya bidhaa zao. 

#Ziara hii imebeba umuhimu mkubwa kwa nchi zetu hizi mbili yaani Tanzania na Ufaransa ambazo uhusiano wake umeanza takribani miaka 30 iliyopita. 

#Uhusiano huu umetuletea manufaa makubwa sisi Tanzania kwa sababu Ufaransa imefadhili miradi mingi na mikubwa ya Maendeleo ikianzia na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. 

#Takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka 10 tu yaani kati ya mwaka 2010 hadi 2020 Ufaransa imefadhili miradi mbalimbali hapa Tanzania yenye thamani ya Euro Milioni 590 (Sawa na Shilingi Trilioni 1 na Bilioni 538 za Tanzania) kupitia Shirika lake la Maendeleo la Ufaransa liitwalo AFD. 

#Ufadhili huu ni wa mikopo yenye masharti nafuu na misaada ambayo imeelekezwa katika sekta mbalimbali zikiwemo miundombinu (barabara, madaraja, viwanja vya ndege), maji na usafi wa mazingira, nishati, elimu (elimu ya msingi, vyuo vikuu vikiwemo UDSM na Chuo Kikuu cha Zanzibar), kilimo, maliasili, utalii na kukuza utamaduni. 

#Kuna uhusiano mzuri wa kibiashara kati ya Tanzania na Ufaranza. Mwaka 2020 thamani ya biashara kati ya Tanzania na Ufaransa ilikuwa Dola za Marekani Milioni 150 (sawa na shilingi Bilioni 343).  

#Ufaransa imewekeza Tanzania miradi 40 (katika sekta za nishati, usafirishaji na ujenzi) yenye thamani ya shilingi Bilioni 167.7 ambayo imezalisha ajira 1,885. 

#Ziara hii ya Mhe. Rais inafanyika kwa lengo la kuimarisha na kuukuza zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo. Tunataka Watanzania wanufaike zaidi na uhusiano huu. 

#Pamoja na kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliojadili namna ya kunufaika na rasilimali ya bahari, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameshuhudia utiwaji saini wa mikataba na makubaliano (6) kati ya Tanzania na Ufaransa. 

#Mkataba wa Ufadhili, Maendeleo na Utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya kipaumbele kwa nchi yetu ya Tanzania. Miradi yetu mikubwa kama SGR, Bwawa la Julius Nyerere, na mingine 

#Mkataba wa Mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya Euro milioni 178 (sawa na shilingi Bilioni 464.1) kwa ajili ya kugharamia mradi wa ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka awamu ya tano jijini Dar es Salaam. Hii ni kwa ajili ya barabara ya Mandela kwenda Gongolamboto. 

#Mkataba wa Mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya Euro milioni 80 (sawa na shilingi Bilioni 208.6) kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa kifedha wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kufikia malengo ya kutoa mikopo ya muda mfupi na mrefu katika sekta ya kilimo. Wakulima wadogo watanufaika. 

#Mkataba wa msaada wenye thamani ya Euro milioni moja 1 (sawa na shilingi Bilioni 2.6) kwa ajili ya kuimarisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ili kufikia malengo ya kutoa mikopo ya muda mfupi na mrefu kwa sekta ya kilimo 

#Tamko la nia kati ya Rais wa Jamhuri ya Ufaransa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya ushirikiano katika eneo la uchumi wa Buluu na usalama wa bahari. 

#Tamko la nia kati ya Rais wa Jamhuri ya Ufaransa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya ushirikiano katika miundombinu ya usafiri na maendeleo endelevu nchini. 

*KUHUSU MUUNGANO*
#Kumekuwa na changamoto mbalimbali za Muungano lakini hatukuishiwa maarifa na majawabu ya kukabiliana nazo. 

#Tumejiwekea utaratibu wa kuwa na vikao vya pamoja vya kuzungumzia masuala ya Muungano ukiwemo utatuzi wa hoja za Muungano. 

#Tulianza jukumu hili tangu mwaka 2006 tukiwa na hoja 25, tumefanya kazi kubwa ya kuzitafutia ufumbuzi, tukazipunguza hadi mwaka 2019 zikabaki hoja 18,  na tarehe 24 Agosti mwaka jana 2021 tukaandika historia nyingine ya kuzifuta hoja 11 kati ya 18 katika vitabu vyetu kwa kuwa tayari zilikuwa zimeshapatiwa ufumbuzi. 

#Wote mliwaona viongozi wetu Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiongoza tukio hili pamoja na viongozi wetu Mhe. Hemed Abdulla, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na walifanyia hapa Zanzibar. 

#Ndugu zangu Waandishi wa Habari naomba kurudia MUUNGANO WETU NI IMARA SANA. Tunatatua hoja mbalimbali zinazohusu Muungano lakini pia tunaendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali hususani masuala ya maendeleo. 

#Ndugu zangu Waandishi wa Habari naomba kurudia MUUNGANO WETU NI IMARA SANA. Tunatatua hoja mbalimbali zinazohusu Muungano lakini pia tunaendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali hususani masuala ya maendeleo. 

#Kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii nchini (TASAF) tuna Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili. Ulizinduliwa mwezi Februari, 2020 ambapo jumla ya shilingi bilioni 112.9 zinatumika hapa Zanzibar na kazi inaendelea. 

#Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hutoa fedha za Kuchochea Maendeleo ya Jimbo kwa Majimbo yote ya Tanzania Bara na Zanzibar na fedha hizo hutumika kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye Majimbo. Kwa Majimbo ya Zanzibar kila mwaka hupokea shilingi bilioni 1.4 ambazo hutumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Majimbo 50 yaliyopo Zanzibar. 

#Nyote mnafahamu, juhudi zilizofanywa na viongozi wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi zilifanikisha kupatikana kwa mkopo nafuu kutoka shirika la fedha duniani (IMF) wa shilingi Trilioni 1.3. Kati ya fedha hizi Zanzibar imepatiwa jumla ya shilingi bilioni 230 kwa ajili ya kukabiliana na athari za UVIKO 19 ambapo fedha hizo zimeelekezwa kwenye huduma za kijamii zikiwemo afya, elimu, miundombinu na ujenzi wa masoko. 

#Mamlaka yetu ya vitambulisho vya Taifa (NIDA) inaendelea kutekeleza jukumu la kutoa vitambulisho kwa Watanzania wa pande zote mbili. Napenda kuwajulisha kuwa mpaka tarehe 31 Januari NIDA imesajili Watanzania 22,802,296. Vitambulisho vya Taifa vilivyozalishwa kwa Nchi nzima Tanzania bara na Visiwani kuwa 10,643,154 na Vitambulisho vilivyogawiwa kwa wananchi ni 9,860,894. 

#Kwa hapa Zanzibar, Watu   806,197 wamesajiliwa sawa na asilimia 88% ya lengo la kusajili watu 919,117 ifikapo Machi 2022. 

#Jeshi la Polisi linaendelea kutekeleza majukumu yake ya usalama wa raia na mali zao, ambapo pamoja na jukumu hilo, Jeshi letu hili linayo miradi kadhaa ya maendeleo hapa Zanzibar ikiwemo Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Polisi Daraja B Mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo shilingi 340,282,500/= zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo hicho,  kinachotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Februari, 2022. 

#Serikali imelipatia Jeshi la Polisi Zanzibar shilingi 200,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za kuishi Askari Polisi eneo la Mfikiwa Mkoa  wa Kusini Pemba na shilingi 150,000,000/= kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa nyumba nne za kuishi askari Polisi katika eneo la Kaskazini Pemba na rest house moja ya Jeshi hilo. 

#Idara ya Uhamiaji Zanzibar imeendelea kutoa Visa kwa wageni kwa njia ya Mtandao (e-Visa) pamoja na Visa zinazotolewa kwa mgeni anapowasili nchini (Visa On Arrival) ambapo e-Visa 126,352 zimetolewa kati ya mwezi Machi 2021 hadi Januari 2022. 

#Katika kipindi cha kati ya Mwezi Machi 2021 hadi mwezi Januari 2022 Uhamiaji Zanzibar imeweza kutoa jumla ya Vibali vya Ukaazi 711 kwa wageni walioingia na kuishi nchini kwa madhumuni mbalimbali kwa mchanganuo ufuatao :- Vibali vya Ukaazi Daraja ‘A’ (wawekezaji) ni 146, Vibali vya ukaazi Daraja ‘B’ (Wataalam) ni 385 na Vibali vya Ukaazi Daraja ‘C’ (Wengineo) ni 180. 

#Serikali imetoa nafasi za ajira kwa Askari 170 kwa Idara ya Uhamiaji Zanzibar kati ya nafasi 820 zilizotolewa na Serikali kwa Idara ya Uhamiaji Bara na Visiwani. 

#Kuanzia mwezi Machi 2021 hadi Januari 2022, Idara ya Uhamiaji Zanzibar imefanikiwa kukusanya Shilingi Bilioni 36,399,382,315.52 kutokana na huduma mbalimbali zinazotolewa na Idara ya Uhamiaji. 

#TANESCO imeendelea kuihudumia Zanzibar vizuri kupitia njia za umeme zilizovushwa baharini. Tuna njia ya kutoka Kunduchi kuja hapa Zanzibar ambapo kuna laini mbili za msongo wa kilovolti 132 (marine cable) ya kwanza ina uwezo wa megawati 50 na ya pili megawati 100. Njia hizi ndizo zinaleta umeme hapa Unguja ambapo mahitaji yake ni megawati 93.4 mpaka sasa. 

# Kutoka Tanga kuna njia ya msongo wa kilovoti 33 (marine cable) kwenda Pemba yenye uwezo wa megawati 20 ambapo matumizi makuu hadi sasa kwa upande wa Pemba ni megawati 13. 

#Kwa kuwa Mhe. Rais Hussein Ali Mwinyi amekuja na msisitizo wa uchumi wa Buluu ambao utahitaji matumizi makubwa ya umeme kwa ajili ya viwanda na shughuli nyingine za uzalishaji, tayari tumeshaanza kuona dalili za kuongezeka kwa matumizi ya umeme Zanzibar. 

#Na ili kuendana na juhudi hizi za Mhe. Rais, TANESCO na ZESCO zimeanza mchakato wa haraka wa kuongeza laini nyingine (marine cable) kutoka Kunduchi mpaka Mtoni Zanzibar itakayopitisha megawati 200.


#Utalii una mchango mkubwa katika uchumi wetu. Takwimu za mwaka 2019/2020 zinaonesha utalii ulichangia asilimia 17.2 katika pato la Taifa la Tanzania Bara na asilimia 27 upande wa Zanzibar. 

#Tumepata changamoto ya janga la ugonjwa wa Corona (Uviko-19) ambapo sekta hii imeathirika na kusababisha idadi ya Watalii kushuka kutoka 1,527,230 waliotembelea Tanzania mwaka 2019 hadi 620,867 mwaka 2020. 

#Hata hivyo juhudi tulizozifanya za kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa  UVIKO-19 kuwavutia zaidi Watalii tumefanikiwa kuanza kuongeza idadi ya Watalii ambapo katika Mwaka 2021 idadi imeongezeka hadi 922,692. 

#Serikali kupitia Wizara ya Afya, inatekeleza Mpango wa II wa kuziwezesha Hospitali za Rufaa za Mkoa nchini kuanza kutoa huduma ya dialysis. 

#Tayari Hospitali 15 zimeshafanyiwa uhakiki wa kuanza kutoa huduma hiyo. Hivi navyoongea nanyi wataalamu wetu wapo katika mafunzo ya jinsi ya kutoa huduma hizi kwa maana ya mafunzo ya kutumia vifaa vya dialysis, na pia ukarabati wa majengo unaendelea. 

#MSD imeshanunua mashine 161 ambazo zitasimikwa kwenye Hospitali hizo za Rufaa za Mikoa, kila Hospitali itafungiwa mashine takribani 10, pamoja na mashine moja ya kusafisha maji. 

#MSD imeajiri wataalamu wa vifaa tiba 9 ambao wamekwishapata mafunzo ya kufunga, kufundisha na kufanyia matengenezo mashine hizo, na wataalamu hao ndio watatumika kufunga, kutoa mafunzo sambamba na kuzifanyia matengenezo. 

#Kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanyika Bandari ya Dar es Salaam wa kuongeza kina cha gati na upanuzi wa njia ya kuingia bandarini,  pamoja na uboreshaji mkubwa wa huduma, imeendelea kuvunja rekodi na kupelekea  ongezeko kubwa la meli  zinazoshusha na kupakia kutoka Bandari hii. 

#Kwa sasa Bandari hii inahudumia Meli 65 kwa mwezi, awali tulikuwa tunahudumia meli 50 hadi 55. Uboreshaji wa huduma na kuzingatia sheria na taratibu za kimataifa kumeifanya bandari yetu kuwa kimbilio la wafanyabiashara wengi wa nchi zisizopakana na bahari. 

#Kwa mara ya kwanza Bandari ya Dar es Salaam tarehe 3/01/2022 tulipokea na kuhudumia meli ya Shaba MV PAPA JOHN ambayo ilipakia Tani Elfu Arobaini na Moja (41,000) ndani ya siku kumi (10). 

#Kwa upande wa mapato TPA imevunja rekodi tena kwa kukusanya Bilion 94.8 kwa mwezi wa Januari, 2022 ikilinganishwa na Bilioni 92.2 zilizokusanywa mwezi Desemba, 2021. 

#Kumekuwa na upotoshaji wakati Fulani ningependa kusisitiza kuwa mapato yanayokusanywa na TRA hapa Zanzibar hubakishwa hapahapa Zanzibar kwa ajili ya kutumika katika maendeleo ya Zanzibar. 

#Kwa kipindi cha kuanzia Julai 2021 hadi Januari 2022 fedha zilizokusanywa na TRA na kubakizwa hapa ZANZIBAR ni shilingi Bilioni 193. 

*Imeandaliwa na Idara ya Habari - MAELEZO*

No comments:

Post a Comment