MH.JENISTA MHAGAMA,,,TUJIVUNIE WATAALAMU WETU WANAWEZA. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, March 24, 2022

MH.JENISTA MHAGAMA,,,TUJIVUNIE WATAALAMU WETU WANAWEZA.


Waziri wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh.Jenista Mhagama


Na Okuly Julius Dodoma

Waziri wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh.Jenista Mhagama amesema kuwa Mfumo wa Kielektroniki wa Tathmini ya Hali ya Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma umesanifiwa na kujengwa na Wataalamu wa ndani ya Ofisi hiyo hivyo ni jambo la kujivunia.

Mh. Mhagama ameyasema hayo wakati akizindua Mfumo huo leo Mtumba Jijini Dodoma katika ofisi za Wizara hiyo na kuongeza kuwa kama sio Wataalamu wa ndani basi serikali ingeweza kuingia gharama kubwa katika kusanifu na kujenga Mfumo kama huo kwa kutumia Wataalamu au Washauri Waelekezi na pengine wa kutoka nje.

Amebainisha kuwa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ina majukumu mengi ya Kisera na kiutendaji yanayotekelezwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali inayolenga kuimarisha usimamizi wa Rasilimaliwatu tangu mtumishi anapoajiriwa mpaka atakapostaafu.

Ameongeza kuwa ni muhimu kusimamia vizuri Rasilimaliwatu ndio inayoweza kuzifanya rasilimali nyingine ziweze kuleta maendeleo hapa nchini.

" Nimekuwa nikisisitiza suala hili mara kadhaa kwamba bila kuisimamia vizuri Rasilimaliwatu basi hizo rasilimali nyingine zote tulizonazo haziwezi kutuletea maendeleo tunayokusudia,"Amesema Mhe,Mhagama

"Niseme mapema na kwa dhati kabisa kuwa wote tunaona juhudi anazozifanya mama yetu Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwenye Sekta mbalimbali katika kuiletea maendeleo nchi yetu na watu wake," Ameongeza

Ameahidi kuendelea kumsaidia Mh.Raisi Samia Suluhu Hassan kufanikisha juhudi hizo katika kutekeleza jukumu la kuimarisha usimamizi na utendaji wa Rasilimaliwatu nchini Ili kufikia azma hiyo pamoja na mambo mengine ni kusanifu na kujenga mifumo na taratibu mbalimbali zikiwemo za kuwezesha kuwa na Watumishi wa Umma wenye sifa stahiki kwa wakati sahihi.

Katika kutekeleza majukumu yaliyopangiwa, Ofisi itahakikisha inazingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2030; Ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 2025; Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Awamu ya Tatu 2021/22 – 2025/26 pamoja na maono ya Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuhusu Utumishi wa Umma wa kidijtali na unaofanya kazi kwa uadilifu, kwa bidii, unaotenda haki, unaowajibika kwa hiari na unaozingatia uzalendo wa kitaifa.

"Ni jukumu letu sisi Viongozi na Watumishi wote wa Umma kuchapa kazi kwa utalaamu, ubunifu na weledi wa hali ya juu ili kuhakikisha kuwa Dira ya Maendeleo ya Taifa na maono na azma ya Kiongozi Mkuu wa Nchi yetu yanatimia," Amesema Mh.Mhagama

Pia amewashukuru wataalamu pamoja na wote waliosimamia mpaka Mfumo huo kukamilika hivyo jukumu kubwa linabaki katika kutunza, kusimamia na kuulinda Mfumo huu ili uweze kufanya kazi iliyokusudiwa ipasavyo.

Waziri Jenista Mhagama amesema mara baada ya kusanifiwa na kujengwa kwa Mfumo huo, Ofisi ya Rais - UTUMISHI iliupeleka kwa Waajiri wote waliopo kwenye Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara katika Utumishi wa Umma (HCMIS) ili kuingiza taarifa na takwimu sahihi kuhusu idadi na mgawanyo wa watumishi kulingana na huduma zinazotolewa na taasisi za Umma.

Kwa taasisi zilizo nje ya Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara katika Utumishi wa Umma (HCMIS) zilipelekewa nyenzo ya kukusanya taarifa ambazo zitaingizwa kwenye Mfumo wa Kielektroniki kwa ajili ya kuchakatwa zaidi.

Mfumo uliozinduliwa utawezesha ukusanyaji, uchakataji na uchambuzi wa taarifa za Watumishi kwa njia ya kisayansi ili kubaini mahitaji halisi ya Watumishi katika Wizara na Taasisi za Umma.

"Zoezi hili litatusaidia katika kutathmini hali halisi ya Watumishi waliopo na wanaohitajika katika taasisi zote za umma ili kuweza kuwapanga kwa kuzingatia mahitaji halisi ya kila taasisi. Kwa kufanya hivyo, Serikali itakuwa na taarifa na takwimu sahihi kuhusu watumishi waliopo, mahitaji ya watumishi wanaohitajika katika kutekeleza majukumu ya kuwahudumia wananchi,"Amesema

Aidha, matarajio ya zoezi hili ni kuweka msawazisho wa Watumishi wa Umma katika taasisi za Umma,Kwa tathmini iliyopo inabainisha kuwa utoshelevu wa mahitaji ya watumishi kwa taasisi za Umma upo kati ya asilimia 52 hadi 90,hata hivyo, zipo baadhi ya taasisi ambazo zina watumishi wa ziada katika baadhi ya kada.

Taarifa za kwenye Mfumo uliouzinduliwa leo zimebainisha kuwa zipo Taasisi zilizofanya vizuri na ambazo hazijafanya vizuri katika kuingiza taarifa kwenye Mfumo. Kwa mfano, Taasisi 10 bora zilizofanya vizuri ni pamoja na Shule ya Sheria Tanzania (97%); Tume ya Ushindani (97%); Chuo cha Ardhi Morogoro (97%); Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala (96%); Ofisi ya Rais Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa (95%); Sekretariet ya Mkoa wa Iringa (95%); Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (95%); Mamlaka ya Serikali Mtandao (95%); Taasisi ya Utafiti wa Wanyama Pori (95%); na Wakala ya Mafunzo ya Menejimenti ya Elimu (94%).

Pamoja na hayo Mfumo pia umebainisha Taasisi takribani 94 ambazo hazijafanya vizuri katika kuingiza taarifa kwenye Mfumo kwa sababu bado zipo chini ya asilimia 50 ya utekelezaji wa zoezi hili (Orodha imeambatishwa).

Pia Mh.Mhagama amewasitiza na kuwaagiza waajiri wote wawasimamie Wakurugenzi au Wakuu wa Idara/Sehemu zinazosimamia Rasilimaliwatu katika taasisi zao ili wakamilishe zoezi ifikapo tarehe 31 Machi, 2022 hivyo kwa taasisi ambazo hazitakamilisha zoezi hili zitakuwa zimekiuka maelekezo ya Serikali na hatua stahiki zitachuliwa.

No comments:

Post a Comment