KAMATI YA WANAWAKE YA HUDUMA JUMUISHI ZA FEDHA WATAKIWA KUTOA ELIMU YA FEDHA HUSUSANI KWA WANAWAKE WAISHIO VIJIJINI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, April 25, 2022

KAMATI YA WANAWAKE YA HUDUMA JUMUISHI ZA FEDHA WATAKIWA KUTOA ELIMU YA FEDHA HUSUSANI KWA WANAWAKE WAISHIO VIJIJINI.


NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango Mh Hamad Hassan Chande Mb akizungumza wakati wa uzinduzi wa kamati ya wanawake ya huduma jumuishi za fedha Aprili 25,2022 jijini Dodoma
Gavana wa Benki ya Tanzania,Prof.Florens Luoga akizungumza wakati wa mkutano wa uzinduzi wa kamati ya wanawake ya huduma jumuishi za fedha Aprili 25,2022 jijini Dodoma.
Gavana wa Benki ya Tanzania,Prof.Florens Luoga akizungumza wakati wa mkutano wa uzinduzi wa kamati ya wanawake ya huduma jumuishi za fedha Aprili 25,2022 jijini Dodoma.
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango Mh Hamad Hassan Chande Mb akikata utepe kuashiria kuzinduliwa kwa kamati hiyo.

Na Okuly Julius Dodoma 

NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango Mh Hamad Hassan Chande Mb Ametoa wito kwa kamati ya wanawake ya huduma jumuishi za fedha kutekeleza kikamilifu program ya kutoa elimu ya fedha ya mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026 kwa wanawake hususani waishio vijijini ili waweze kunufaika na huduma na bidhaa za fedha .

Ameyasema hayo wakati akizindua kamati ya wanawake ya huduma jumuishi za fedha na kuongeza kuwa kamati hiyo ina kazi kubwa ya kuendelea kutoa elimu kwa wanawake katika masuala ya fedha katika kila ngazi hapa nchini.

Mhe.Chande amewahakikishia kuwa serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi kupitia baraza la taifa la huduma jumuishi za fedha itaendela kuwa bega kwa bega na kamati hiyo yenye wajumbe 22 kutoka wizara mbalimbali za Serikali ,Taassi na Asasi za kiraia inayolenga kuongeza idadi ya wanawake katika sekta ya fedha.

Amesema,suala la kuinua wanawake kiuchumi kwa kuongeza ushiriki wao katika sekta ya fedha ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapindunzi ya mwaka 2020, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 -2025/26) na Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa mwaka 2020/21-2029/30.

"Kamati hii ni muhimu na inajukumu kubwa katika kubuni, kuchochea na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mikakati inayolenga kuongeza idadi ya wanawake katika kuzifikia na kuzitumia huduma rasmi za fedha na hatimaye kunyanyua kipato cha mwanamke;

Ni matumaini yangu kuwa, baada ya uzinduzi wa leo mtahakikisha lengo la Serikali la kupunguza utofauti ulipo katika upatikanaji na utumiaji wa huduma za fedha kati ya mwanamke na mwanaume utapungua kwa zaidi ya asilimia 90,"amesema Naibu Waziri huyo wa fedha.

Vilevile amesisitiza kuwa azma ya kumnyanyua mwanamke kiuchumi ifanyiwe kazi ipasavyo, kwa kushirikana na Kamati ya ushauri ya Kitaifa ya Utekelezaji wa ahadi za Nchi kuhusu Kizazi chenye Usawa na kuongeza kuwa utakapofanyika utafiti mwingine wa kisekta, baada ya utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa mwaka 2018-2022, idadi ya watanzania watu wazima wanaotumia huduma rasmi za fedha itakuwa imeongezeka mpaka asilimia 75 mwaka 2022.

"Ninategemea kuona mbali na kutekeleza malengo mtakayokuwa mmejiwekea kupitia Kamati hii yanayohusu masuala ya fedha, pia mtatekeleza mikakati yenye kuhamasisha wadau wa huduma za fedha kutoa elimu ya masuala ya fedha kwa wanawake hasa waishio vijijini ili waweze kunufaika na huduma na bidhaa za fedha,"amesisitiza

Mbali na hayo ameeleza kuwa elimu ya fedha ni muhimu ili kuwaondolea hofu wanawake walio wengi katika kutumia huduma hizo ikiwemo mikopo na kwamba bado kuna umuhimu wa kuwafundisha wanawake namna ya kusimamia mikopo na kujitetea kisheria pale panapokuwa na uporaji wa fedha zao za mikopo dhidi ya wenzi wao ili wasipate changamoto yakufanya marejesho.

"Kuna umuhimu kwa wanawake kupewa elimu ya namna ya kuweka akiba, kufanya uwekezaji, kukata bima na kujiandaa na maisha ya uzeeni,ipo haja ya kuwahamasisha wadau wa sekta ya fedha kupendekeza mikakati itakayoongeza upatikanaji wa takwimu za kijinsia hasa kutoka kwa sekta binafsi ili zitusaidie kufanya maamuzi ya kisera kwa kuzingatia usawa wa kijinsia,"amesema.

Kwa upande wake Gavana wa Benki ya Tanzania,Prof.Florens Luoga amesema Tanzania imekuwa ikitekeleza Mpango wa Pili wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha (2018-2022), ambao unalenga kuongeza idadi ya watu wanaotumia huduma rasmi za fedha kutoka asilimia 65 mwaka 2017 hadi asilimia 75 mwaka 2022.

Amesema Mpango huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi kupitia Baraza la Taifa la Huduma Jumuishi za Fedha, ambalo lina wajumbe 22, kutoka Wizara mbalimbali za Serikali, taasisi na asasi zisizo za Serikali.

"Mpango huu wa Taifa unasisitiza kuongeza idadi ya wanawake inayofikiwa na kutumia huduma rasmi za fedha, umeelekeza, kuundwa kwa Kamati ya Wanawake ili kuratibu shughuli zote zinazohusu wanawake nchini katika Sekta ya Fedha pamoja na kushauri njia bora ya kutatua changamoto zinazowakumba wanawake katika kufikia na kutumia huduma rasmi za fedha,"amesema.

Ametaja lengo la mpango huo kuwa ni kuhakikisha idadi kubwa ya wanawake wanaofikiwa na kutumia huduma rasmi za fedha inaongezeka, kutoka asilimia 61 mwaka 2017 hadi asilimia 73 mwaka 2022, pia kupunguza pengo la uwiano wa kijinsia katika utumiaji wa huduma rasmi za fedha kati ya wanawake na wanaume kwa asilimia 90.

No comments:

Post a Comment