NA Okuly Julius-Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh.Jenista Mhagama amesema kuwa hatamuonea huruma mtumishi mzembe, mwizi na mbadhirifu wa mali za umma badala yake atachukua hatua kali kwa kuzingatia kanuani za maadili katika utumishi wa umma.
Mhe.Mhagama ameyasema hayo leo Mei 26,2022 Jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa wakuu wa Idara za utawala na rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kutoka taasisi za umma.
Amewataka kusimamia Rasilimaliwatu kwa kuzingatia Kanuni za Maadili katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2005 ambazo ni; Kutoa Huduma Bora, Utii kwa Serikali, Bidii ya Kazi, Kutoa Huduma Bila Upendeleo, Kufanyakazi kwa Uadilifu, Kuwajibika Kwa Umma, Kuheshimu Sheria na Matumizi Sahihi ya Taarifa.
Pia amewahakikishia kuwa , Serikali kupitia Ofisi yake inaendelea kuimarisha mifumo ya uwajibikaji ili kuhakikisha kwamba Viongozi na Watumishi wa Umma katika ngazi zote wanakuwa na malengo yanayopimika na yanayotekelezeka.
"Kama mnavyofahamu Ofisi yangu inafuta mfumo uliokuwepo wa kupima utendaji kazi kwa wazi ulikuwa ukifaamika kama OPRAS kutokana na changamoto mbalimbali zilijitokeza wakati wa utekelezaji wake"Amesema Mh.Mhagama
Na Kuongeza kuwa "Badala ya Mfumo huu, Ofisi yangu inakamilisha maandalizi ya Mfumo mpya wa Usimamizi wa Utendaji Kazi wa Watumishi wa Umma wa Kielektroniki ujulikanao kama (PEPMIS)"
Hivyo mfumo huu utasaidia kuondoa baadhi ya changamoto kama vile tabia iliyojengeka ya kujaza fomu za OPRAS kulingana na matukio, utawezesha utoaji alama zinazoakisi utendaji halisi kwa kuzingatia kiwango cha utekelezaji wa malengo na shabaha za mtumishi, fomu za utekelezaji wa mfumo kuzingatia kada tofauti na mazingira ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi na kuwezesha kuoanisha utendaji wa watumishi na utendaji wa Taasisi za Umma kwa kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi wa Taasisi za Umma (PIPMIS).
Utekelezaji wa mfumo wa PIPMIS utakuwa na manufaa katika kuongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa Sera, Mikakati na Vipaumbele vya Taasisi, Sekta na Taifa kwa ujumla; kuboresha utoaji huduma kwa umma; kuimarisha utamaduni wa utendaji unaojali matokeo; na kuleta matumizi bora ya rasilimali za Umma.
Mhe.Mhagama amewaagiza wakuu wa Idara ya rasilimaliwatu kuhakikisha wanasimamia Mifumo ya kuboresha utendaji kazi Serikalini ukiwemo Mfumo wa Wazi wa Upimaji wa Utendaji Kazi na Mkataba wa Huduma kwa Mteja ili kuhakikisha watumishi wote wanawajibika na kulipwa mishahara kwa kazi zenye matokeo na tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment