UJUMBE WA TANZANIA WAKUTANA NA MKURUGENZI MKUU WA UMOJA WA POSTA DUNIANI (UPU) - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 17, 2022

UJUMBE WA TANZANIA WAKUTANA NA MKURUGENZI MKUU WA UMOJA WA POSTA DUNIANI (UPU)


Bern, Switzerland

Ujumbe wa Tanzania Unaohudhuria kikao cha Baraza la Utawala (CA) la Umoja wa Posta Duniani (UPU) kilichoanza  tarehe 16 May, 2022 na kinachofanyika makao Makuu ya Umoja huo jijini Bern,Uswis umekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa UPU Bwana Masahiko Metoki.

Ujumbe huo umeongozwa na Bwana Mohammed Khamis Abdulla, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari aliyeambatana na Dkt Jabir Bakari, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Shirika la Posta Tanzania(TPC).

Katika mazungumzo hayo, Naibu Katibu Mkuu Bwana Abdulla amempongeza Bwana Metoki kwa kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa UPU katika Mkutano Mkuu wa Umoja uliofanyika Agosti, 2021 jijini Abidjan,Ivory Coast. 

Pia amemshukuru Bwana Metoki kwa kuwa nchi yake Japan iliiunga mkono Tanzania hadi kuchaguliwa kwenye Mabaraza muhimu ya uongozi yaani Baraza la Utawala na lile la Uendeshaji la UPU nafasi zilizoiwezesha Tanzania kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa Kamati namba mbili ya Baraza la Uendeshaji la UPU.

Sambamba na hilo alimshukuru Bwana Metoki kwa kuwa mwezi Februari, 2022 Tanzania imepokea fedha za kuboresha huduma za Posta kupitia mfuko wa Ubora wa Huduma (UPU quality of Service Fund) kwa kiwango cha dola za kimarekani 208,000.00. 

Naibu Katibu Mkuu pia alishukuru UPU kwa kuendelea kuiamini Tanzania na kuipa nafasi ya kuwa kituo cha kutegemeza Teknolojia kwa nchi za Afrika zinazoongea Kiingereza pamoja na Msumbiji kilichopo Makao Makuu ya Shirika la Posta Tanzania, jijini Dar es salaam.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TCRA alimweleza Bwana Metoki kuwa Tanzania imepiga hatua katika eneo la Anwani za Makazi ambapo Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa msukumo maalumu kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na Anwani ya Makazi ifikapo mwishoni mwa mwezi May, 2022. 

Vile vile alimuomba Bwana Metoki kuunga mkono juhudi zinazoendelea kwa kusaidia program zitakazosaidia kurahisisha na kuboresha utekelezaji na matumizi ya Anwani za Makazi. 

Sambamba na hilo ameomba kuungwa mkono katika kujengea uwezo kwa watumishi wa Posta kwa kuwa Shirika la Posta lipo kwenye mageuzi makubwa ya kidijitali. Pia aliomba UPU kuharakisha ukamilishaji wa vifaa vya kupimia ubora wa huduma ambavyo Mamlaka ilikuwa imeagiza kutoka UPU.

Kwa upande wake Bwana Masahiko ameahidi kuendelea kufanya kazi na Tanzania kwenye maeneo ya Ubunifu kuhusiana na Anwani za Makazi na Postikodi, huduma za Posta za kidijitali na uboreshaji huduma za Posta nchini Tanzania. 

Vilevile, amekubali kuongeza nguvu kwenye kituo cha kutegemeza Teknolojia kinachohudumia nchi zinazozungumza kiingereza pamoja na Msumbiji kinachoongozwa na mtaalamu wa Shirika la Posta Tanzania kilichopo makao makuu ya Shirika jijini,Dar es salaam. 

No comments:

Post a Comment