Watumishi wapya BRELA wahimizwa kujituma - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 17, 2022

Watumishi wapya BRELA wahimizwa kujituma



Na Mwandishi wetu Dar-es-salaam 

Watumishi wapya wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) wametakiwa, kujituma na kujifunza kwa haraka jinsi mifumo ya BRELA inavyofanya kazi ili kuwahudumia wadau kwa ufanisi.

Rai hiyo imetolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw.Godfrey Nyaisa wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tano kwa waajiriwa wapya yanayofanyika katika Kituo cha Mafunzo kwa njia ya Mtandao, ambacho kiko chini ya Chuo Cha Utumishi wa Umma, jijini Dar es salaam.

Bw. Nyaisa amewataka watumishi hao kutoa huduma bora na kwa haraka zaidi ili kukidhi matarajio ya wadau.

Bw. Nyaisa amesisitiza kuhusu suala la nidhamu mahala pa kazi, kuwa ni jambo la muhimu hivyo ni vyema kila mmoja akajitambua na kujua lengo la taasisi ni kuwahudumia wananchi.

"Nidhamu katika kazi ni jambo ambalo linapaswa kuzingatiwa na bila kusahau weledi katika kazi, maana lengo letu ni kutoa huduma bora zaidi, hivyo mfanye kazi Kwa bidii," amesema Bw. Nyaisa

 Amefafanua kuwa watumishi wote ni sawa, hivyo ni vyema kufanya kazi kwa kuheshimiana ili BRELA iendelee kuwa sehemu bora ya kufanya kazi.

Alisisitiza pia kuwa mtumishi yoyote anapofanya kazi ni kwa ajili ya nchi na anamuwakilisha Rais, hivyo ni vyema kufanya kazi Kwa weledi ili kuleta picha nzuri kwa Taifa 

Pia watumishi hao wamesisitizwa kuhusu maadili ya utumishi wa umma ili kutoa huduma zenye viwango vya juu, kuzingatia muda, na kuheshimu watu wanao wahudumia.

 Ameongeza kuwa kufanya kazi Kwa weledi ndiyo msingi katika utumishi wa umma, huku utunzaji wa kumbukumbu ulio sahihi ukihimizwa kwa watumishi hao

Kwa upande wake mwezeshaji kutoka Kituo cha Mafunzo kwa njia ya Mtandao cha Chuo cha Utumishi wa Umma, Bw. Faraja Mbwiro amesema kuwa utumishi wa umma unatakiwa kufanywa kwa weledi na kuzingatia sheria, ili kufikisha huduma bora kwa wadau.

 Mafunzo haya yaliyoanza tarehe 16 Mei, 2022 ni mwendelezo wa mafunzo mbalimbali yanayotolewa na BRELA ili kuwajengea uwezo wa kiutendaji watumishi wake.

No comments:

Post a Comment