WIKI YA UBUNIFU (MAKISATU) KULETA UFUMBUZI WA CHANGAMOTO ZA KIUCHUMI NA KIJAMII - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, May 16, 2022

WIKI YA UBUNIFU (MAKISATU) KULETA UFUMBUZI WA CHANGAMOTO ZA KIUCHUMI NA KIJAMII




Na Okuly Julius-Dodoma

Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman amesema kuwa Maadhimisho ya Wiki ya Ubunifu (MAKISATU) Kitaifa na Maonesho ya mwaka huu yataibua zaidi ubunifu na teknolojia zitakazo kwenda kujibu na kuleta ufumbuzi wa changamoto za kiuchumi na kijamii Inazokabiliana nazo katika shughuli za kila siku.

Amezungumza hayo wakati akifungua rasmi wiki ya Ubunifu jijini Dodoma Mei 16,2022 na kusema kuwa wiki hii itaonesha bunifu mbalimbali ambazo zimebuniwa na Watanzania yote hayo ni kwa ajili ya kurahisisha shughuli za kila siku.

Aidha,ameongeza kuwa Serikali itaendelea kujenga mazingira na kutoa fursa ya kuweza kuibua wabunifu zaidi na kuwaendeleza kwa lengo la kuchochea kasi ya maendeleo na kuimarisha maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii.

"Serikali inatambua umuhimu wa wiki hii na ndio maana maonesho haya yanafanyika ili kuendelea kuibua na kukuza vipaji tunapaswa kufanya maonesho naamini itatusaidia kuongeza kasi ya maendeleo kwa taifa" Amesema Mhe.Othman

Amesema kuwa Mbali na kusaidia ukuaji wa uchumi kwa taifa ununifu pia itatoa mchango mkubwa katika upatikanaji wa ajira pamoja na kuvutia wawekezaji wa kigeni kuweza kutoa fursa za ajira kwa wenyeji kutokana na ujuzi walionao.

"Kwa hivyo, na sisi tutachukua kila hatua kuona malengo yetu ya kuhamasisha ubunifu na teknolojia yanafanikiwa"Ameongeza

Ameongeza kuwa Serikali zote mbili zimeazimia kujenga uwezo wa ndani kwa kuendelea kuwekeza katika rasilimali watu, miundo mbinu na vifaa vya kisasa vya utafiti na ubunifu pamoja na kuimarisha mahusiano kati ya Taasisi za Sayansi na Teknolojia pia sekta ya viwanda.

"Matunda ya jitihada za Serikali, katika utekelezaji wa malengo hayo na hatua zinachukuliwa yote yanabainika kupitia Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu"Amesema

Katika kuhakikisha ubunifu na elimu ya Sayansi na Teknolojia inawekezwa kwa vijana ili kupata wataalamu wa fani mbali mbali, kwa upande wa Zanzibar wameanzisha Mradi wa kujenga vituo 22 vya ubunifu wa Sayansi Unguja na Pemba. Vituo hivyo, vimeanza kutumika ambao ni mradi uliogharimu USD Milioni 35 zikiwa ni Mkopo kutoka Benki ya Dunia.

Vile vile, jitihada za kuimarisha vituo vya mafunzo ya amali kote nchini zinaendelea ili kuwapatia vijana mafunzo ya ufundi wa fani mbali mbali kwa lengo la kupunguza changamoto ya ajira.

Pia Mhe.Othman ametoa pongezi kwa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa jitihada zao katika kusaidia usimamizi wa tafiti mbali mbali nchini na kuzishauri Serikali zetu kuhusiana na masuala yanayohusu Sayansi, Ugunduzi na Teknolojia kwa maendeleo endelevu ya Taifa letu.

"Serikali itaendelea kuijengea uwezo wa kifedha na kitaalamu COSTECH, ili iweze kusaidia zaidi shughuli za utafiti na ubunifu nchini kwa faida ya wananchi wa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,"amesema Mhe.Othman

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda amesema Taasisi tofauti tofauti 50 pamoja na wabunifu 26 ambao bunifu zao zimefikia hatua ya kuingia sokoni na kuanza kutumika zimeshiriki katika maeonesho hayo.

Ambapo amesema wabunifu 862 walijisajili kwa mwaka huu na wabunifu 86 bunifu zao zitashindanishwa ili kupata washindi.

Maonesho ya Wiki ya Ubunifu Kitaifa kwa mwaka huu wa 2022  inaongozwa na kauli mbiu isemayo "Ubunifu kwa maendeleo endelevu" yatafikie kilele chake tarehe 19 Mei 2022.

No comments:

Post a Comment