![]() |
Namba maalum ya kupiga bure kwenda kituo cha huduma kwa wakulima (wateja) cha Wizara ya Kilimo iliyozinduliwa leo Julai 05,2022 jijini Dodoma na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe |
Na Okuly Julius-Dodoma
Kitengo cha huduma kwa wakulima (huduma kwa wateja) itakuwa na jukumu kubwa la kutatua changamoto za wakulima ambao watakuwa wanapiga simu moja kwa moja kituoni hapo pamoja na kutatua matatizo ya wafanyabiashara wanaofanya biashara za mazao.
Akizungumza leo Julai 05,2022 jijini Dodoma wakati akizindua kituo cha huduma kwa wakulima (huduma kwa wateja) Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema kuwa serikali kwa sasa inatatatua matatizo ya wakulima moja kwa moja kwa wakati na ndio maana wameamua kuwa na kituo cha huduma kwa wakulima na kutoa namba ambao itakuwa wazi kwa masaa ishirini na nne kwa ajili ya kupokea simu kwa wakulima na wafanyabiashara wa mazao.
Amesema kuwa nchi kwa sasa inatakiwa kuingia katika soko la kimataifa la mazao hivyo kituo hicho pia kitatumika kuwashauri wakulima ni zao gani linafaa kwa wakati gani kulingana na mahitaji ya soko la dunia la mazao.
"Kituo hichi kitafanya kazi kubwa ikiwepo kutatua matatizo ya wakulima na kutoa ushauri kulingana na mahitaji ya soko la mazao la dunia ili na sisi nchi yetu iende sambamba na mahitaji ya dunia ndipo Mhe. Rais anatamani tufike, " Amesema Bashe
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde amesema kuwa kwa sasa ile maana halisi ya kilimo kiganjani au kidijitali inakwenda kuonekana kwani kutakuwa na ukaribu kati ya wataalamu wa kilimo na wakulima wenyewe jambo ambalo litasaidi kutatua changamoto kwa urahisi na kufanya kilimo kufika katika kilele cha mafanikio na kuwa kimbilio kwa watanzania.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw.Andrew Massawe amebainisha kuwa mpaka kufikia hatua hii ya kuzindua kituo hicho ni baada ya kuwa na programu ya M-Kilimo iliyofanya kazi ya kuandikisha wakulima ambapo mpaka kufikia julai 04,2022 jumla ya wakulima milioni tano laki nane themanini na sita elfu mia nne themanini na tisa ( 5,886,489) na zoezi hilo bado linaendelea.
Pia kupitia Programu ya M-Kilimo wameshasajili Exporters zaidi ya 3905 pamoja na wanunuzi wa mazao zaidi ya 4400 tangu kufunguliwa kwa programu hiyo tarehe 18, Mei 2020 na ndio chanzo cha kuanzishwa kwa Kituo hicho cha Huduma kwa wakulima (huduma kwa wateja)
No comments:
Post a Comment