Na Immaculate Makilika – MAELEZO, Mbeya
Serikali imeendelea kuboresha sekta ya elimu nchini kupitia mradi wake wa Ujenzi na Ukarabati wa Vyuo vya Elimu ambapo kwa kushirikiana na Serikali ya Canada ilitoa fedha kwa lengo kuboresha miundombinu ya kujifunza na kufundishia katika Chuo cha Ualimu Mpuguso.
Akizungumza leo chuoni hapo katika mahojiano maalum na Afisa wa Idara ya Habari – MAELEZO, Mkuu wa Chuo cha Ualimu Mpuguso, Steven Mgimba amesema “Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na serikali ya Canada ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 9.9 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya chuo hichi kwa lengo la kuwajengea wanachuo na watumishi mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia”
Akifafanua zaidi, Mkuu huyo wa Chuo amesema ujenzi wa mradi ulianza mwaka 2016 ambapo sehemu ya kwanza ya mradi ulikamilika mwaka 2018 na sehemu ya pili ulikamilika mwaka 2021 na kwa ujumla mradi huo umehusisha ujenzi wa maktaba, madarasa, mabweni, maabara, ukumbi wa mihadhara na nyumba za wakufunzi.
“Kabla ya mradi huo madarasa yalikuwa katika hali mbaya, mabweni yalikuwa katika kiwango cha chini na tulikuwa na wanachuo 400 tu kiujumla hali ilikuwa mbaya, lakini sasa hivi hali ni nzuri sana na tuna idadi ya wanachuo 625 japo tukiwa na mabweni zaidi uwezo wa Chuo chetu hadi wanachuo 720 maboresho haya yametupa tija sana” Amesititiza Mkuu huyo wa Chuo.
Kwa upande wake, Mkufunzi wa Chuo cha Ualimu Mpuguso, Magdalena Mwanisawa amesema kuwa awali kulikuwa na mrundikano wa wanachuo katika madarasa hadi kufikia 70 kwa darasa moja badala ya 45 au 50.
“Mradi huu umetunufaisha kwa vile sasa hivi hakuna mrundikano wa wanafunzi madarasani wala mabwenini na sisi wakufunzi tunafanyakazi zetu katika mazingira bora na tunaishi katika makazi bora” Amesema Mwanisawa.
Ameongeza “Mradi huu umetusaidia sisi wakufunzi tumewezeshwa kwa kupatiwa ujuzi katika masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa hiyo kila mtu sasa ana uwezo wa kuandaa nukuu zake za kufundishia kwa kutumia kompyuta. Vilevile madarasa sasa yana mfumo wa miundombinu ya TEHAMA”
Chuo cha Ualimu Mpuguso ni miongoni mwa vyuo vinne vilivyomo katika Mradi wa Ujenzi na Ukarabati wa Vyuo yaani Upgrading Teachers’ Colleges ambapo mikoa mingine ni Tabora, Mtwara na Shinyanga.
No comments:
Post a Comment