Na OWM-TAMISEMI , Morogoro.
Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Watoto Ulimwenguni (UNICEF) inatoa mafunzo maalum kwa Maafisa Ustawi na Maafisa Lishe wa ngazi ya mkoa na halmashauri kutoka mikoa ya Dodoma na Dar es salam, ili kuwajengea uwezo wa kuandaa vifaa vya kujifunzia na kuchezea watoto kwenye vituo vya kulelea watoto wadogo mchana vilivyopo masokoni.
Mafunzo hayo kwa maafisa hao yameanza kutolewa Aprili 13, 2026 mkoani Morogoro, kwa lengo la kuwajengea uwezo utakaoimarisha ubora wa malezi na ujifunzaji kwa watoto wadogo katika ngazi za mikoa na halmashauri.
Akizungumzia mafunzo hayo, Mratibu wa Mafunzo hayo kutoka OWM - TAMISEMI Bi Amina Mfaki amesema kuwa washiriki watapatiwa ujuzi wa kuandaa vifaa vya kujifunzia na kuchezea kwa kutumia rasilimali zinazopatikana katika mazingira yao, hatua inayotarajiwa kuongeza ubunifu, kupunguza gharama na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa rafiki kwa watoto katika vituo hivyo.
“Mafunzo yamelenga kuhakikisha waratibu wanakuwa na uwezo wa kusimamia na kuratibu kwa ufanisi shughuli za uandaaji wa vifaa hivi muhimu kwa maendeleo ya awali ya mtoto," amesisitiza Bi. Mfaki.
Ameongeza kuwa, mafunzo yataboresha mazingira ya malezi kwa watoto wadogo wanaokaa katika vituo vya kulelea watoto wadogo mchana masokoni, ambavyo vinahudumia hasa watoto wa wafanyabiashara na wajasiriamali.
Aidha, Bi. Mfaki amewataka maafisa hao kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo ili kupata ujuzi utakaowajengea uwezo kiutendaji ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kutoa elimu kwa wadau kuhusu umuhimu wa uwekezaji katika elimu ya awali.
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, inandelea na jitihada za kuimarisha huduma za maendeleo ya awali ya watoto katika mazingira mbalimbali, hususan katika maeneo yenye shughuli nyingi za kiuchumi kama masoko.










No comments:
Post a Comment