Na Okuly Julius-Dodoma
Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Usimamizi wa Uchaguzi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Stephen Elisante amesema kuwa wanatumia maonesho ya Nanenane kutoa elimu kwa Wapiga Kura ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mazoezi ya Uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura na uchaguzi mkuu utakaofuatia.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 7,2022 kwenye banda la Tume hiyo lililopo katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kikanda katika viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma.
Amebainisha kuwa Tume inatumia maonesho hayo kukutana na wadau wake ili kuwaelimisha kuhusu masuala ya uchaguzi, hivyo kuwepo kwao katika viwanja vya nanenane ni fursa tosha kwa kila mwananchi kufika na kupata elimu kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu uchaguzi.
Bw. Stephen amesema kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Uchaguzi Mkuu hufanyika kila baada ya miaka mitano ambapo uchaguzi wa mwisho ulifanyika mwaka 2020 na kila baada ya uchaguzi kumalizika Tume huanza rasmi maandalizi ya uchaguzi unaofuata kwa kufanya mambo mbalimbali ikiwemo maboresho ya mifumo ya uchaguzi, kufanya mapitio ya sheria, kanuni na maelekezo mbalimbali ili kuziboresha kwa kuzingatia maoni mbalimbali ya wadau.
"Tume ipo kazini kwa maandalizi ya uchaguzi unaofuata ambao unatarajiwa kufanyika mwaka 2025 na moja ya maandalizi hayo ni kutoa elimu kwa mpiga kura sasa hapa kwenye banda letu tumekuja na baadhi ya vifaa vinavyotumika kipindi cha uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura na uchaguzi kama vile mashine ya BVR, mfano karatasi za kura, fomu mbalimbali za matokeo, fomu zinazotumika wakati wa uboreshaji, masanduku ya kura na Majalada ya nukta nundu kwa ajili ya wapiga kura wenye uono hafifu na vitabu mbalimbali vinavyohusiana na uchaguzi" Amesema Bw.Stephen
Pia, amewapongeza wananchi ambao wanatembelea mabanda mbalimbali yaliyo katika maonesho hayo na kupata elimu ya musuala mbalimbali ikiwemo elimu ya mpiga kura inayotolewa na banda la Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kuongeza kuwa wapo tayari kuendelea kutoa elimu hivyo amewataka wananchi wanaotembelea maonesho hayo kuhakikisha wanatembelea banda la Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili kupata elimu ya uchaguzi itakayowasaidia kuboresha ushiriki wao katika michakato ya uchaguzi.
Vilevile, aliwasisitiza wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika tarehe 23 Agosti, 2022 kwa kuwa takwimu za sensa ni muhimu katika kupanga utekelezaji wa masuala mbalimbali yanayowahusu maendeleo ya wananchi ikiwemo masuala ya uchaguzi.
No comments:
Post a Comment