Na Mwandishi wetu Dar-es-salaam
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi amewataka wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania kuwa na ubunifu katika utendaji kazi utakaoleta tija kwenye Shirika na Taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo tarehe 19 Agosti, 2022 wakati wa hafla ya kuwapongeza Viongozi Pamoja na Wafanyakazi Hodari wa Shirika la Posta kwa mwaka wa fedha 2021/2022, Makao Makuu ya Shirika hilo, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo Dkt. Yonazi amesema, bidii na ubunifu ndiyo njia pekee itakayoliwezesha Shirika kufika mbali zaidi kiutendaji na ndiyo itawezesha kuongezeka kwa mapato ya Shirika yatakayoleta tija kwa Taifa
Aidha, Katibu Mkuu amewapongeza Viongozi na Wafanyakazi Hodari wa Shirika hilo kwani juhudi na bidi ndiyo iliyowapelekea kupata nafasi hizo. Hata hivyo, amelitaka Shirika kuwazingatia wafanyakazi wenye nafasi za chini ambao ndiyo wanaowawezesha Viongozi kuonekana kufanya vizuri katika utendaji wao
Vilevile, Dkt. Yonazi ametumia hafla hiyo kulipongeza Shirika la Posta kwa jitihada zake mbalimbali za kuendelea kuboresha huduma zake ili kuendana na mabadiliko ya Teknolojia Pamoja na mahitaji ya wananchi.
Sambamba na hilo Katibu Mkuu Dkt. Yonazi ametoa malekezo kwa Shirika kuhakikisha linaweka kigezo cha Ubunifu wa Biashara Mpakani (Cross Border Business) kwa Viongozi na wafanyakazi ili kuwahamasisha wafanyakazi wa Posta kuongeza bidii katika kutafuta fursa za kibiashara mpakani mwa Tanzania.
Kwa upande wake Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Ndg. Macrice Mbodo amemshukuru Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi kwa kufika katika hafla hiyo na kuahidi Shirika litaendelea kuongeza bidii katika utendaji wake ili kuendelea kuwapatia wananchi huduma bora na zinazoendana na mahitaji yao.
Viongozi na wafanyakazi hao Hodari walipatikana kupitia kikao cha Tathmini ya Utendaji Kazi wa Shirika la Posta kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kilichohusisha viongozi wote wa Mikoa na Makao Makuu mapema mwezi huu mkoani morogoro.



No comments:
Post a Comment