WAZIRI MKUU AZINDUA MPANGO KABAMBE WA SEKTA YA UVUVI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, September 20, 2022

WAZIRI MKUU AZINDUA MPANGO KABAMBE WA SEKTA YA UVUVI

Waziri Mkuu akizungumza wakati alipozindua mpango kabambe wa Sekta ya Uvuvi utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka kumi na tano kuanzia 2021/2022 hadi 2036/2037, katika ukumbi wa maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Septemba 20, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizindua mpango kabambe wa Sekta ya Uvuvi utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka kumi na tano kuanzia 2021/2022 hadi 2036/2037, Kwenye ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Septemba 20, 2022. Kushoto ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki na kulia ni Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Dkt. Christina Ishengoma (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wakati alipowasili kwenye ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam kuzindua mpango kabambe wa Sekta ya Uvuvi utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka kumi na tano kuanzia 2021/2022 hadi 2036/2037, Septemba 20, 2022. Wa pili kushoto ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Na Mwandishi-Dar-es-salaam 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Sekta ya Uvuvi utasaidia kukuza sekta hiyo na kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa hadi kufikia asilimia 10 kwa mwaka kutoka asilimia 1.8 ya sasa.
 
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa mpango huo ambao utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka 15 kuanzia 2021/2022 hadi 2036/2037 unaumuhimu mkubwa katika ukuaji wa sekta ya uvuvi pamoja na Uchumi wa Buluu.
 
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wadau wote wa sekta ya uvuvi kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa ina nia ya dhati ya kuhakikisha kila mmoja ananufaika na sekta hiyo.
 
Amesema hayo leo (Jumanne, Septemba 20, 2022) wakati wa uzinduzi wa Mpango Kabambe wa Sekta ya Uvuvi, katika ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dar es Salaam. “Tutaendelea kupokea mapendekezo yenu ili tuweze kuboresha sekta hii, ubunifu wenu ni muhimu, wote tunataka tuzungumze lugha moja.”
 
Waziri Mkuu amesema kuwa mpango huo unaendana na maono ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuleta mapinduzi makubwa kwenye sekta zote ikiwemo sekta za uzalishaji. “Mpango huu utasaidia kwa kiwango kikubwa kutekeleza dhamira hiyo njema ya Mheshimiwa Rais, tunataka twende kwa kasi zaidi.”
 
Mheshimiwa Majaliwa amesema uwepo wa mipango mbalimbali katika sekta ya uvuvi utawezesha rasilimali hiyo kulindwa, kusimamiwa, kuendelezwa, kuhifadhiwa na kutumiwa kwa njia endelevu na hatimaye kuchangia kikamilifu katika kutoa ajira, kipato, chakula na lishe kwa jamii ya Watanzania kwa ujumla.
 
“Matumizi endelevu ya rasilimali ya uvuvi yanategemea sana uwepo wa mipango madhubuti ya kusimamia matumizi na uendelezaji wa rasilimali hizi.”
 
Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa utekelezaji wa mpango huo utakuwa chachu ya kuendeleza kasi ya ukuaji wa Sekta ya Uvuvi na utasaidia kuongeza kwa kiasi cha samaki na mazao ya uvuvi yaliyochakatwa na kusafirishwa nje ya nchi kwa asilimia 30.
 
“Mpango huu utakuwa chachu ya kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya uvuvi kutoka tani 473,592 hadi kufikia tani 639,092, sawa na ongezeko la asilimia 35.”
 
Aidha, Mheshimwa Majaliwa amezitaka Wizara na Taasisi zote za Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sekta Binafsi, Taasisi zisizo za Kiserikali, Madhehebu ya Dini pamoja na wadau wa maendeleo kupokea Mpango huo. “Uzingatieni mpango huu katika mipango yenu ya kisekta na kuendelea kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kufanikisha utekelezaji wake kwa maslahi mapana ya Taifa”

No comments:

Post a Comment