BMH YAOKOA ZAIDI YA MILIONI 500 BAADA YA KUZINDULIWA KWA MTAMBO WA KUZALISHAJI HEWA TIBA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, October 26, 2022

BMH YAOKOA ZAIDI YA MILIONI 500 BAADA YA KUZINDULIWA KWA MTAMBO WA KUZALISHAJI HEWA TIBA

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa Dkt.Alphonce Chandika akielezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za hospitali hiyo na utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2022-2023 mbele ya waandishi wa habari leo Oktoba 27,2022 jijini Dodoma.

Na Okuly Julius-Dodoma

Tangu kuzinduliwa kwa Mtambo wa kuzalishaji Hewa Tiba 'Oxygen' katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa imesaidia kuokao zaidi ya milioni 500 na kuongeza mapato ya ndani ya Hospitali kwa kukusanya zaidi ya Shilingi milioni 75 ambazo Hospitali zingine zinachangia kwa kupelekewa huduma hiyo.

Mtambo huo una uwezo wa kuzalisha mitungi 400 ndani ya masaa 24, tangu mtambo huu uzinduliwe, Julai 1, 2022, jumla ya mitungi 13,467 imeshazalishwa ambapo mitungi 10,962 imetumiwa hospitali hapo na mitungi 2,505 ilisambazwa kwenye Hospitali zenye mahitaji.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo Dkt.Alphonce Chandika wakati akielezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za hospitali na utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2022-2023 mbele ya waandishi wa habari leo Oktoba 27,2022 jijini Dodoma.

Dkt.Chandika amesema kuwa wakati wa kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO-19, hospitali hiyo ilikuwa na changamoto ya upatikanaji wa hewa tiba 'oxygen' ambapo walikuwa wakitumia mitungi 200 kwa siku.

"Serikali ilitupatia Shilingi bilioni 1.1 na milioni 400 zilitokana na mapato yetu ya ndani kwa ajili ya kununua na kusimika mtambo wa kuzalishia hewa tiba, kununua mitungi 560 na gari la kusambazia hewa tiba hiyo katika Hospitali mbalimbali, jumla mradi umegharimu shilingi bilioni 1.5," Amesema Dkt.Chandika

Dkt.Chandika amesema kuwa Hospitali hiyo imejikita katika kuanzisha na kuboresha huduma za ubingwa bobezi ambapo imefanikiwa kuanzisha huduma za upandikizaji wa figo na jumla ya wananchi 31 wamenufaika na huduma hiyo, huku gharama ya huduma hiyo ikiwa ni takriban shilingi milioni 25 wakati nje ya nchi mgonjwa angetibiwa kwa takriban Shilingi milioni 100 ambapo kwa wagonjwa hao 31, Serikali imeokoa zaidi ya Shilingi bilioni 2.3

Mkurugenzi huyo amesema kuwa Hospitali hiyo imefanikiwa kutoa huduma za matibabu ya moyo ambapo kuna maabara maalum inayotumika katika kutoa matibabu ya moyo pasipo kufungua kifua.

"Hospitali hii ni ya pili hapa nchini kutoa huduma hii.Tangu huduma hii imeanza kutolewa mwaka 2019, jumla ya wananchi 715 wamehudumiwa kwa kuchunguzwa,"Amesema Dkt.Chandika

Amesema kuwa wagonjwa 39 waliobainika kuwa na matatizo makubwa ya moyo wamehudumiwa kwa kuwekewa vipandikizi na kati ya 39, wagonjwa wawili kati yao walihudumiwa kwa dharura ambapo kama ingekuwa ni kusafirishwa kwenda kupatiwa matibabu Dar es Salaam wangepoteza maisha.

"Kuna wagonjwa nane ambao mapigo yao ya moyo yanashuka sana, walihudumiwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kupandikizwa betri kwenye moyo na kupitia maabara hiyo tumeweza kuhudumia watoto 14 waliozaliwa na matatizo ya moyo,"Amesema Dkt.Chandika

Na kuongeza kuwa "Hospitali imeanza kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto waliobainika kuwa na matatizo ya kuzaliwa ya moyo ambapo tayari watoto kumi wameshahudumiwa,"Amesema Dkt.Chandika

Pia tangu mwaka 2020, Hospitali ilifanikiwa kuanzisha upasuaji wa nyonga na magoti kwa kuweka vipandikizi, hadi sasa jumla ya wagonjwa 56 wamewekewa vipandikizi hivyo kwa wastani wa gharama ya shilingi milioni 12. Gharama za huduma hii nchi za nje ni takriban milioni 35 ambapo kwa wagonjwa 56 waliohudumiwa , Serikali imeokoa jumla ya Shilingi bilioni 1.28

"Hospitali hii ndio pekee nchini imefanikiwa kuanzisha huduma ya uvunjaji wa mawe kwenye figo kwa kutumia mawimbi na miale pasipo kumfanyia mgonjwa upasuaji, huduma hii imeshatolewa kwa wagonjwa 148 kwa gharama ya Shilingi milioni 1.2 kwa mgonjwa mmoja, kwa nje ya nchi gharama ni zaidi ya milioni 7 ambapo kwa wagonjwa 148, Serikali imeokoa zaidi ya Shilingi milioni 850,"Ameeleza Dkt.Chandika

Katika jitihada za Serikali kuhakikisha inawaletea wananchi huduma za afya zilizo bora, ilidhamiria kuiwezesha Hospitali ya Benjamini Mkapa kuwa na vifaa tiba vya kisasa na vinavyotumia teknolojia ya kisasa ili iweze kukidhi adhma yake ya kuwahudumia wananchi kwa kuwapatia matibabu ya kiwango cha juu.

No comments:

Post a Comment