WAZIRI MKUU AWASILISHA BAJETI YA TRILIONI 12.5 KWA MWAKA 2026/2027 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, April 1, 2026

WAZIRI MKUU AWASILISHA BAJETI YA TRILIONI 12.5 KWA MWAKA 2026/2027


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amewasilisha Bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Ofisi ya Bunge kwa mwaka wa fedha 2026/2027, yenye jumla ya shilingi trilioni 12.5.

Akiwasilisha hoja hiyo leo Aprili 1, 2026, Bungeni Jijini Dodoma, Dkt. Nchemba alisema kuwa kati ya fedha hizo jumla ya shilingi12,502,356,160,000, shilingi trilioni 8.73 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida, huku shilingi trilioni 3.77 zikielekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Alifafanua kuwa bajeti hiyo inalenga kuimarisha utoaji wa huduma za Umma pamoja na kusukuma mbele agenda ya maendeleo katika taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge.

“Mheshimiwa Spika, ninaomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 12,502,356,160,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo,” alisema Dkt. Nchemba wakati akiwasilisha hoja hiyo.

Kwa upande wa mapato, Waziri Mkuu alilieleza Bunge kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zinatarajia kukusanya jumla ya Shilingi Trilioni 2,336,528,152,302.47 ambapo jumla ya makusanyo na maduhuli ya ofisi yake ni Shilingi Trilioni 2,411,548,152,302.47 ambazo zinatarajiwa kukusanywa.

Aidha, amebainisha kuwa kiasi cha Shilingi Trilioni 12,268,472,643,000 kitatumika mahsusi kugharamia shughuli za kawaida na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, hatua inayotarajiwa kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Katika msisitizo wa vipaumbele vya mwaka ujao wa fedha, Dkt. Nchemba amewataka Wakuu wa Mikoa kusimamia kikamilifu maandalizi ya miundombinu na huduma muhimu kwa ajili ya mapokezi ya wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2028, kufuatia utekelezaji wa Sera ya Elimu ya lazima ya miaka kumi.

Pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mifumo ya kielektroniki na mashine za kukusanyia mapato (POS), akisema hatua hiyo itasaidia kudhibiti upotevu wa mapato ya umma na kuongeza ufanisi katika matumizi ya fedha za Serikali.

Akizungumzia mafanikio ya Serikali, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameeleza kuwa katika mwaka 2025, jumla ya watumishi 12,000 wameajiriwa na kupangiwa vituo vya kazi, wakiwemo 5,000 wa Sekta ya Afya na 7,000 wa Sekta ya Elimu, jambo lililochangia kuboresha utoaji wa huduma katika sekta hizo za huduma hapa nchini.


Katika hitimisho lake, Dkt. Nchemba amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake thabiti na jitihada zake katika kuwaletea wananchi maendeleo, akieleza kuwa dira yake inaendelea kuiongoza nchi katika mwelekeo sahihi wa maendeleo chini ya kaulimbiu ya “Kazi na Utu - Tunasonga Mbele.”



No comments:

Post a Comment