NFRA KUONGEZA UWEZO WA KUHIFADHI NAFAKA HADI KUFIKIA TANI 501,000 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, October 22, 2022

NFRA KUONGEZA UWEZO WA KUHIFADHI NAFAKA HADI KUFIKIA TANI 501,000

Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), CPA. Milton M. Lupa akizungumza na waandishi wa habari ( hawapo pichani) leo Oktoba 22,2022 jijini Dodoma kuhusu shughuli za Wakala hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha 2022/23.
Sehemu ya washiriki wa mkutano kati ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), CPA. Milton M. Lupa ( hayupo pichani) alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 22,2022 jijini Dodoma kuhusu shughuli za Wakala hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha 2022/23.

Na Okuly Julius-Dodoma

Ili kuongeza uwezo wa kuhifadhi chakula nchini,Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umesema unatekeleza mradi wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka,ambapo ukikamilika utaongeza uwezo wa kuhifadhi kutoka tani 251,000 hadi tani 501,000.

Hayo yameelezwa leo Oktoba 22,2022 Jijini Dodoma na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), CPA. Milton M. Lupa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu shughuli za Wakala hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha 2022/23.

Ambapo Lupa amesema kuwa NFRA imefanikiwa kukamilisha sehemu ya Mradi na kuongeza uwezo wa kuhifadhi kwa tani 90,000 katika kanda za Arusha (Halmashauri ya Babati) na Sumbawanga na Mpanda.

"Kukamilika kwa Mradi huo kumeongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka kutoka tani 251,000 hadi tani 341,000 na utekelezaji wa Mradi katika maeneo mengine Dodoma, Songea,Shinyanga,Songwe na Makambako umefika asilimia 85,"Amesema Lupa.

Kwa upande wa Ajira NFRA imefanikiwa kutoa ajira za muda mfupi kwa wananchi zaidi ya 3,000 zinazochangia kipato kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

"Ajira hizo zinatokana na kazi mbalimbali zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa zoezi la ununuzi wa nafaka,uhifadhi na kipindi cha uzungushaji wa nafaka na utekelezaji wa Mradi wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka,"Ameeleza Lupa

Lupa amesema ili kukabiliana na makali ya mfumuko wa bei za nafaka Wakala kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo imeongeza upatikanaji wa nafaka katika masoko ili kuleta unafuu wa maisha kwa wananchi.

"Kwa kuanzia,Wakala unahudumia Halmashauri za Bunda,Sengerema,Geita, Nzega,Liwale,Nachingwea,Longido,Loliondo na Monduli ambapo takriban tani 3,000 zimepelekwa katika maeneo hayo,"Amesema Lupa


Aidha, Mtendaji huyo amesema kuwa Wakala imejipanga kuhudumia maeneo mengine yatakayothibitika kuwa na mahitaji ya dharura au upungufu wa Chakula.

Ametoa wito kwa wananchi kujihakikishia usalama wa chakula kuanzia ngazi ya Kaya,wahifadhi akiba ya kutosha ya chakula kipindi cha mavuno na kuuza chakula pale wanapokuwa na ziada katika uzalishaji.

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ni Taasisi ya Serikali chini ya Wizara ya Kilimo iliyoanzishwa kwa Sheria ya Wakala za Serikali Na.30 ya mwaka 1997 na ulianza kazi rasmi julai 1,2008 ikiwa na jukumu la kuhakikishia nchi usalama wa chakula kwa kununua na kuhifadhi akiba ya chakula na kutoa chakula cha msaada kwa waathirika waliokumbwa na majanga mbalimbali ya kitaifa.

No comments:

Post a Comment