UTORO WA WALIMU BADO PASUA KICHWA-TSC - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, October 27, 2022

UTORO WA WALIMU BADO PASUA KICHWA-TSC

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu Mwl. Paulina M. Nkwama akizunguza na waandishi wa habari leo Oktoba 28,2022 jijini Dodoma, kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali ya Tume hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha wa 2022-2023.

Na Okuly Julius-Dodoma

Tume ya Utumishi wa Walimu imesema kuwa Katika kipindi cha mwezi Machi, 2021 hadi Septemba, 2022, Walimu 1,952 walifunguliwa mashauri ya kinidhamu ambapo katika mashauri yaliyofunguliwa 1,362 sawa na asilimia 69.8 ya mashauri yote yalihusu utoro.

Huku Mashauri 260 sawa na asilimia 13.3 ya mashauri yote yalihusu kughushi vyeti na mashauri 119 sawa na asilimia 6.1 yalihusu mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi.

Taarifa hiyo imetolewa mbele ya waandishi wa habari leo Oktoba 28,2022 jijini Dodoma na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu Mwl. Paulina M. Nkwama wakati akielezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali ya Tume hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha wa 2022-2023.

Ambapo Mwl.Nkwama amebainisha kuwa katika mashauri 1,642 yaliyoamuliwa,Walimu 919 sawa na asilimia 56 ya adhabu zilizotelewa walifukuzwa kazi, Walimu 234 sawa na asilimia 14.3 hawakupatikana na hatia, Walimu 115 sawa na asilimia 7 ya adhabu zilizotolewa walishushwa cheo, Walimu 89 sawa na asilimia 5.4 walikatwa mshahara asilimia 15 kwa muda wa miaka mitatu na Wengine 143 sawa na asilimia 8.7 walipewa adhabu ya Karipio.

"Katika mashauri 1,642 yaliyoamuliwa Walimu 919 sawa na asilimia 56 ya adhabu zilizotelewa walifukuzwa kazi, Walimu 234 sawa na asilimia 14.3 hawakupatikana na hatia, Walimu 115 sawa na asilimia 7 ya adhabu zilizotolewa walishushwa cheo, Walimu 89 sawa na asilimia 5.4 walikatwa mshahara asilimia 15 kwa muda wa miaka mitatu na Walimu 143 sawa na asilimia 8.7 walipewa adhabu ya Karipio."Ameeleza Mwl.Nkwama

Aidha Mwl.Nkwama amesema ,katika kipindi cha miaka mitatu kwa fedha (2020/2021) shilingi Bilioni 14.773 zilitengwa kwenye bajeti huku (2021/2022) iliongezeka hadi kufikia billion 14.980 ambapo (2022/2023) bajeti ya tume hiyo iliendelea kuongezeka zaidi na kufikia kiasi bilioni 15.454 ikiwa ni kutokana na juhudi za serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

"Katika kipindi cha miaka mitatu (2020/2021; 2021/2023; 2022/2023) mfululizo Bajeti ya Tume imeendelea kuongezeka kutoka shilingi Bilioni 14.773 , 14.980 na 15.454 sawia. Hii ni kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya awamu y a sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania".

Akielezea mafanikio yaliyopatikana tangu Serikali ya awamu ya sita kuingia madarakani katika kipindi cha kuanzia mwezi Machi, 2021 hadi mwezi Septemba, 2022; Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameiwezesha TSC kufanikiwa kutekeleza majukumu mbalimbali ambayo yameendelea kuboresha mazingira ya Walimu na Sekta ya Elimu kwa ujumla.

"Tangu serikali hii ya awamu sita iingie madaraka Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na Walimu 16,749 kuajiriwa,wakiwemo 8,949 wa Shule za Msingi na 7,800wa Shule za Sekondari,Jumla ya Walimu 15,802 walisajiliwa, Walimu wa Shule za Msingi walikuwa 8,512na Sekondari walikuwa 7,290 wakati Walimu 6,949 sawa na asilimia 100 walithibitishwa kazini wakiwemo 3,949 wa Shule za Msingi na 3,000 wa Shule za Sekondari,"Ameeleza Mwl.Nkwama

Pamoja na hayo Mwl.Nkwama Tume imekuwa ikishughulikia changamoto ya mwalimu mmoja mmoja kwa wale ambao wamekuwa wakilalamika kucheleweshwa kupandishwa madaraja miaka iliyopita ili kuhakikisha kwamba kila mwalimu anapata anachostahili. Zoezi hili hufanywa kwa kushirikiana na waajiri (Wakurugenzi wa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa) na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

"Jumla ya Walimu 47,158 walipandishwa cheo (Walimu 22,943 ni wa Shule za Msingi na 11,524 wa Sekondari kwa mwaka 2021/2022). Aidha kwa mwaka 2020/2021 walimu walipandishwa cheo ni 126,346,"Amesema Mwl.Nkwama

Katika hatua nyingine Mwl. Nkwama ameeleza kuwaTume hiyo imeweza kuwajengea uwezo Watumishi 58 kwa kuwawezesha kuhudhuria mafunzo ya muda mrefu na mfupi ambapo Watumishi watano (5) wanahudhuria mafunzo ya muda mrefu na mafunzo ya muda mfupi kwa kada saidizi (Watumishi 41) katika masuala ya utunzaji wa kumbukumbu, huduma kwa mteja na usalama mahala pa kazi.

"Aidha, Watumishi 12 walihudhuria mafunzo ya muda mfupi ya kitaaluma huku Mafunzo haya yote kwa ujumla wake yamegharimu jumla ya Shilingi 175,350,000.00".Amesema Mwl.Nkwama

Na kuongeza kuwa "juhudi hizi za Serikali ya awamu ya sita zina lengo la kuiwezesha Tume ya utumishi wa walimu kuwahudumia Walimu kwa weledi na kuteta ufanisi zaidi katika kazi ya kuwahudumia walimu,"Amesema Mwl.Nkwama

Hata hivyo Tume hiyo inayohudumia jumla ya Walimu 266,388 Tanzania Bara, wakiwemo 177,956 wa Shule za Msingi na 88,432 wa Shule za Sekondari imesema itaendelea kusimamia Utumishi na Maendeleo ya Walimu kwa kudumisha Maadili na Nidhamu kwa Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari katika Utumishi wa Umma na itahakikisha Walimu wenye sifa ya kupandishwa vyeo na kubadilishiwa kazi wanapata huduma hiyo kwa wakati baada ya kibali kutolewa na Mamlaka husika.

No comments:

Post a Comment