![]() |
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Wadau wa elimu wa Mwaka wa Tathmini ya maendeleo ya Sekta ya Elimu 2021/22 unaofanyika kwa siku mbili Disemba 6 mpaka 7 jijini Dodoma. |
![]() |
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Wadau wa elimu wa Mwaka wa Tathmini ya maendeleo ya Sekta ya Elimu 2021/22 unaofanyika kwa siku mbili Disemba 6 mpaka 7 jijini Dodoma. |
NA Okuly Julius-Dodoma
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda ametoa wito kwa Wadau wa elimu wanaoshiriki Mkutano wa Siku mbili wa Mwaka wa Tathmini ya maendeleo ya Sekta ya Elimu kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kutoa maoni yao madhubuti kwa ajili ya kusaidia Mageuzi katika sekta ya Elimu hapa nchini.
Prof. Mkenda ameyasema hayo leo Disemba 6,2022 Dodoma,katika Mkutano huo wenye lengo la kutoa fursa kwa wadau mbalimbali wa elimu kushiriki kikamilifu katika kupanga Mipango ya Maendeleo ya Elimu na programu kwa ajili ya kuleta maendeleo endelevu kwa mtu mmoja mmoja, jamii na taifa kwa ujumla.
Prof.Mkenda amesema kuwa Sekata ya Elimu nchini bado inahitaji mageuzi makubwa hivyo anaamini kupitia mkutano huo Wadau watapata nafasi ya kujadi kikamilifu namna ya kuleta maendeleo endelevu kwenye sekta ya Elimu..
"Elimu yetu inahitaji sana Kuongeza ufundi Stadi na hayo ni maelekezo ya Mhe.Rais kutaka elimu yetu iwatoe vijana wenye ubunifu na ujuzi wa kutosha pale wanapohitimu elimu,hivyo Mkutano huu wa Wadau utatusaidia ni namna gani ya kuingiza hicho kipengele katika Mitaala yetu," Amesema Prof.Mkenda
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt.Francis Michael amesema kuwa kaulimbiu ya Mkutano huo wa mwaka wa Tathmini ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu mwaka 2021/22 ni “Marekebisho ya Mifumo ya Elimu ili Kukidhi Mahitaji ya Kitaifa na Kimataifa" ,hivyo ni vyema kila mmoja aliyepata fusa ya kushiriki mkutano huu kujadili kwa kina mada zitakazowasilishwa na kutoa maoni yenye tija katika kuimarisha na kuendeleza elimu yetu nchini.
"Kaulimbiu hii inaakisi mwelekeo wa Serikali katika kuleta mageuzi katika Sekta ya Elimu kama ilivyoelekezwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,"
Na kuongeza kuwa "Mathalani, katika kutekeleza azma hiyo ya marekebisho na maboresho katika sekta, Wizara inaendelea na maboresho ya mitaala kuanzia ngazi ya Elimumsingi hadi Elimu ya juu. Aidha, uboreshaji wa Sera ya Elimu unaendelea baada ya ukusanyaji wa maoni ya wadau wa elimu nchini kote na kuendelea kuyachakata,"Amesema Dkt.Francis
Dkt.Francis ameongeza kuwa kupitia Mkutano huo wa Tathmini yamepatikana mafanikio mbalimbali yaliyopatikana, ikiwemo Ukarabati na ujenzi wa miundombinu ikiwemo madarasa, mabweni, maabara na matundu ya vyoo kwa Shule za Msingi na Sekondari,Ukarabati wa miundombinu ya Taasisi za Elimu ikiwemo Vyuo Vikuu (SUA, ARDHI, MZUMBE, UDSM, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Mafanikio mengine ni Kuajiri Walimu 11,547 (ambapo 7928 ni wa Shule za Msingi pamoja na walimu 3,621 wa Shule za Sekondari),Kutoa Mafunzo kwa Walimu 402 wanaotoa mafunzo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum;
Pia Dkt.Francis amesema Kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania imeandaa miongozo ya utoaji wa elimu kwa kutumia TEHAMA kwa elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Vyuo vya Ualimu na Kukamilisha Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Elimu 2021/22 -2025/26.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Elimu UNESCO ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wadau wa Maendeleo katika Sekta ya Elimu Tanzania Bi.Faith Shayo amesema kuwa Mkutano huo umekuja Muda Muafaka kwani Dunia kupitia Umoja wa Mataifa ipo katika mabadiliko na mageuzi katika Sekta ya elimu kuanzia Sera,Miongozo na Mitaala yake ili kuleta mageuzi yenye tija.
"Mkutano huu umekuja kipindi muafaka kwani dunia ipo katika mabadiliko na mageuzi makubwa katika sekta ya elimu ,hivyo sisi kama wadau tunapaswa kuisaidia serikali kufanikisha mageuzi haya kaa michango yetu ya mali na hali lengo likiwa ni kuendeleza sekta hii muhimu kwa taifa," Amesema Bi.Faith Shayo
Mkutano huo wenye lengo la kutoa fursa kwa wadau mbalimbali wa elimu kushiriki kikamilifu katika kupanga Mipango ya Maendeleo ya Elimu na programu kwa ajili ya kuleta maendeleo endelevu kwa mtu mmoja mmoja, jamii na taifa kwa ujumla utafanyika kwa siku mbili kuanzia Disemba 6 mpaka 7 Jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment