Shirika la Posta Tanzania kwa kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) limejipanga kimkakati katika kufikisha huduma ya vitambulisho vya Taifa kwa wananchi mahali popote walipo nchi nzima.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 06 Disemba, 2022 wakati wa mazungumzo rasmi baina ya Taasisi hizi mbili yaliyoongozwa na Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Macrice Mbodo na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Bw. Ismail Rumatila katika Makao Makuu ya Posta jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo hayo yalilenga kujadili namna bora ya kuwafikishia wananchi huduma ya upatikanaji wa Vitambulisho vya Taifa nchi nzima na hususani katika maeneo ya vijijini kupitia Mfumo wa Posta kiganjani ikihusisha mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi, lengo ikiwa kurahisisha utoaji wa huduma hiyo nchini.
Katika hatua nyingine Mamlaka wa Vitambulisho vya Taifa Tanzania (NIDA) imelipongeza Shirika la Posta Tanzania kwa maboresho ya huduma zake na imeahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha katika kufikisha huduma bora kwa wananchi.
Mazungumzo haya ni muendelezo wa ushirikiano uliopo baina ya Shirika la Posta na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) katika huduma za usafirishaji wa vifurushi vya NIDA na katika kuwahudumia wananchi kupitia vituo vya Huduma Pamoja vilivyopo katika ofisi za Posta.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano,
Shirika la Posta Tanzania
06 Disemba 2022
No comments:
Post a Comment