Na Okuly Julius-Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewataka walimu wote Nchini kufuata muongozo wa malezi, unasihi na ulinzi wa mtoto kwa shule za Msingi, sekondari na vyuo vya ualimu wa mwaka 2020 na sehemu zenye changamoto ziwasilishwe ili kuimarisha ulinzi kwa wanafunzi.
Akizungumza Wakati wa kufungua Mkutano Mkuu wa 17 wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA),Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda,amesema kuwa walimu ni muhimu sana kwa maendeleo ya taifa hivyo watumie nafasi zao kuandaa kizazi chenye weledi.
“Tushirikiane kufanya ulinzi wa watoto, hakikisheni shuleni hawalali watoto wawili kitanda kimoja na kama kuna changamoto ya vyoo pia pigeni simu kwa mkurugenzi mueleze changamoto hizo lengo ni kuhakisha mazingira salama ya utoaji elimu na kuwalinda watoto,”amesisitiza Waziri Mkenda.
Amewataka walimu kuangalia maudhui ya vitabu vinavyoingia shuleni ili visiharibu wanafunzi lakini pia kutumia Skauti na Viongozi wa dini katika kuendeleza malezi mazuri ya watoto shuleni.
"Nitumie pia Mkutano Mkuu huu wa 17 kuendelea kuwakumbusha nafasi mlionayo katika taifa hili nyinyi ni watu wa Muhimu sana ila kuna wachache sana wanaotaka kuwachafuq kwa kufungua mitihani kuwaonyesha watoto hao tutapambana nao,"
Na kuongeza kuwa "Mitihani imekuwa ikienda vizuri kwenye Baraza la Mitihani la Tanzania isipokuwa inapokwenda shuleni wamekuwepo watu wachache sana ambao wanajihusisha na udanganyifu na kwamba Serikali haitavumilia udanganyifu huo,"Amesisitiza Prof.Mkenda
Prof.Mkenda ameongeza kuwa mtu yeyote atakayeleta udanganyifu kwenye mitihani atakamatwa na kushughulikiwa kisheria na baada ya hapo atatangazwa hadharani ili iwe fundisha kwa wengine.
"Walimu hakikisheni mnakataa kujiingiza katika udanganyifu huo na kuwa makini zaidi kwenye masuala ya mtihani,”
Na kuongeza kuwa " Kwa sasa kuna kesi zinaendelea kwa wale ambao walituhumiwa kwa kuvujisha mitahani na nawaahidi pindi hukumu zao zitakopotolewa na mahakama ,tutaweka majina yao hadharani ili iwe fundisho kwa wengine,"Ameeleza Prof.Mkenda
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Charles Msonde amewataka wakuu wa Shule kufuatilia utendaji wa walimu shuleni ili kuondoa alama F kweny masomo wanayofundisha.
“Naendelea kusisitiza kufuatilia utendaji wa walimu, lakini pia wanafunzi wanapoingia shuleni tuanze na kuhakikisha wanakuwa vizuri katika lugha, wanapoilewa na kuiandika inakuwa rahisi kwao kuelewa masomo,”amesisitiza Dkt. Msonde.
Kwa upande wake Rais wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) Frank Mahenge ameishukuru Serikali kwa namna inavyoshirikiana na Umoja huo na kuiomba pamoja na kazi nzuri wanayoifanya ya kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu nchini kujenga pia nyumba za walimu.
No comments:
Post a Comment