Na Shua Ndereka -Morogoro
Mtandao wa kutokomeza ndoa za utotoni Tanzania (TECMN) umeitaka serikali kutekeleza uamuzi kama ilivyoagizwa na Mahakama Kuu na kuidhinishwa na Mahakama ya Rufani kwamba umri wa chini wa kuoa na kuolewa ni miaka 18.
Hayo yalibainishwa katika mkutano wa wadau wa haki za watoto uliofanyika mkoani Morogoro na kutolewa Tamko juu kubadilishwa kwa vifungu vya sheria ya ndoa ambapo Mkurugenzi wa Chama cha wanasheria wanawake Tanzania (TAWLA) Tike Mwambipile alisema kuwa, mwaka 2016, Mahakama Kuu ya Tanzania ilitoa hukumu katika Kesi ya Rebecca Gyumi, ambayo ilifunguliwa kupinga wasichana kuolewa chini ya umri wa miaka 18 katika Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971.
“Hata hivyo serikali ilikata rufaa na mnamo mwaka 2019 mahakama ya Rufani katika kesi ya mwanasheria mkuu wa serikali dhidi ya Rebacca Gyumi ilitoa maamuzi ambayo iliitaka serikali ndani ya mwaka mmoja kubadili sheria ya ndoa na kuweka miaka 18 kama umri wa kuoa na kuolewa ambapo hadi sasa ni takriban miaka mitatu tangu kutolewa kwa hukumu hiyo na bado Serikali haijatekeleza uamuzi huo”.
Kupitia Tamko hilo ilibainishwa kuwa, Serikali izingatie mapendekezo ya Kamati ya Watalamu wa Haki za Watoto ya Afrika ya kuchukua hatua kutokomeza ndoa za utotoni kwenye shauri lilitolewa maamuzi hivi karibuni (LHRC & Centre for Reproductive Rights vs Republic of Tanzania, app. no. 0012/COM/001/2019).
Alisema Mnamo mwezi wa tisa mwaka huu, Wizara ya Katiba na Sheria ilitoa barua inayoelezea mchakato wa Serikali wa kukusanya maoni ya wananchi kuhusu ndoa za utotoni, ikiwa Mchakato huo umeleta sintofahamu miongoni mwa wadau, zikiwemo AZAKI zinazojihusisha na utetezi wa haki za mtoto.
Aidha Tike Mwambipile alisema kuwa, Taarifa za kina kuhusiana na mchakato huu hazijapatikana na kulingana na sheria za nchi ikiwemo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 wanaona kwamba, mchakato huo hauna uhalali kwa Serikali kuhusisha mchakato unaoendelea na uamuzi wa Mahakama katika Kesi ya Rebecca Gyumi, kwani Mahakama ndiyo imepewa mamlaka ya mwisho katika kutafsiri sheria.
“Maamuzi ya Mahakama ya Rufani pia yanamaanisha kwamba vifungu vinavyoruhusu ndoa za utotoni katika Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 havipo tena kisheria, na katika muktadha huo mchakato hauwezi kuhusishwa na hukumu ya kesi ya Rebecca Gyumi” Alisema Mwambipile
Naye Wakili Barnabas Kaniki kutoka Chama cha wanasheria wanawake Tanzania (TAWLA) alibainisha juu ya ukinzani wa sheria ya ndoa ya mwaka 1971 katika kifungu cha 13 na 17 kinachomruhusu mtoto kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 kwa ridhaa ya wazazi na umri wa miaka 15 kwa ridhaa ya mahakama huku sheria ya mtoto ya mwaka 2009 ikieleza kuwa mtoto ni mwenye umri chini ya miaka 18.
Alisema kuwa baada ya maamuzi ya Mahakama kuu kuelekeza katika vifungu hivyo vya sheria kufanyiwa marekebisho, ikiwa ni sababu mojawapo ya kukinzana kwa sheria ya ndoa na sheria ya mtoto 2019 hivyo kama wadau wanaendelea kufanya mashauriano na kuishauri serikali kuhakikisha inatekeleza hukumu, kama ilivyoelekeza katika kesi hiyo kwa kufanya hivyo itasaidia kuondoa huo mgongano.
“Kuhusu mila na desturi limeendelea kuwa changamoto kwa kuwasukuma mabinti wengi kuingia katika ndoa za utotoni, tunafahamu mambo haya yanayohusiana na mila, tabia za watu yanahitaji muda ili mabadiliko yaweze kutokea, lakini sisi kama wadau tunasema kwa upande wa sheria na sera tayari tumevuka huko hivyo tunaiomba serikali kubadili hivyo vifungu na sisi wadau tutakuja kushukurika na hizi mila na tabia za watu elimu zitolewe taratibu taratibu watabadilika”.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika la Agape kutoka mkoani Shinyanga John Myola alisema watoto hao wanaoolewa chini ya mika 18 bado ni wadogo na wanahitaji malezi, matunzo na ulinzi hivyo wanapoingia katika jukumu la kuwa wazazi hushindwa kuhimili na kutunza familia na hupelekea kuachika kutokana na kutokuwa na upeo wa kulea familia na wakati mwingine hufanyiwa ukatili wa kijinsia na ukatili wa kiuchumi.
Hata hivyo Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania (TECMN) ulianzishwa mwaka 2012 ukijumuisha mashirika 70 kutoka sehemu mbalimbali nchini kwa lengo la kutokomeza ndoa za utotoni nchini Tanzania huku wakihusisha juhudi za mashirika mbalimbali ya siyo ya kiserikali na kuwahusisha wadau, viongozi wa mila, wabunge, viongozi wa dini na jamii kwa kuendelea kutoa elimu ili juu kutokomeza mimba na ndoa za utotoni.
No comments:
Post a Comment