Na Shua Ndereka - Morogoro
Watoto wa kike wanatajwa kuwa hatarini zaidi na ndoa za utotoni kwa mujibu wa Takwimu za Shirika la Watoto duniani UNICEF 2012 mkoa wa Shinyanga ukiongoza kwa asilimia 59 kuwa na idadi kubwa ya ndoa za utotoni na Morogoro kwa asilimia 42 ambapo Takriban wanawake watatu kati ya 10 nchini wanaolewa wakiwa watoto, na hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya 11 duniani kwa kuwa na ndoa za utotoni.
Kwa Kuzingatia athari wanazozipata wasichana kutokana na tatizo la mimba na ndoa za utotoni, Shirika la Agape AIDS Control Programme likishirikiana na Msichana Initiative wametoa ombi kwa serikali kupitia wizara na taasisi husika kuongeza kasi kwenye jitihada za kubadili kifungu cha sheria ya ndoa namba5 ya mwaka 1971 vinavyomruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 kwa ridhaa ya wazazinamiaka 15 kwa ridhaa ya mahakama.
Akizungumza na Mwandishi wa Blog hii Wakili wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Msichana Initiative iliyopo jijini Dar es Salaam na inayojihusisha na kutetea haki za mtoto wa kike katika elimu Lucy Gidams, anabainisha kuwa mabadiliko ya Sheria ya ndoa yafanyike kwa haraka na wepesi ili kuwasiadia wasichana kubeba agenda na kufikia ndoto zao.
“Kitu cha kwanza ambacho kitasaidia kutoka katika janga hili la ndoa za utotoni ni mabadailiko ya kisheria, Mahakama ilishaamuru kwamba sheria ibadilike lakini hadi sasa ukisoma sheria ya ndoa kifungu cha 13 na 17 kinamruhusu mtoto kuolewa, sasa vifungu hivi vikiondolewa mimi ninaamini tutakuwa tumepiga hatua kubwa katika kutokomeza ndoa za utotoni”.
Wakati Tanzania ikiadhimisha siku ya mtoto wa kike oktoba mwaka huu, Waziri wa Maendeeo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima alisema Serikali, wizara za Kisekta imeanza mapitio ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 pamoja na sheria nyingine zinazogongana ili kuwasaidia watoto wa kike sambamba na sheria ya Mtoto ya mwaka 2009.
Waziri Gwajima alisema Serikali kupitia wizara za kisekta zimeshaanza kufanya mapitio ya sheria ya ndoa na sheria nyingine ambazo zimejichanganya hapo hivyo mikoa kadhaa imeshatoa maoni na timu inaendelea kupokea maoni ya wananchi kwani hata Sheria hiyo iliyotengenezwa awali ilikuwa na sababu ya msingi ila imepitwa na wakati hivyo mapendekezo yanaendelea ili kufanya mapitio ya marekebisho.
Licha ya Sheria hizo kuwepo ambazo zinalalamikiwa, bado wakazi wa Manispaa ya Morogoro akiwemo Husna Mussa na John Michael wanaamini kwamba ndoa za utotoni zinachangiwa na malezi mabovu kwa baadhi ya wazazi huku Mama Denis, anaeleza kuwa kabla ya kuingia katika ndoa ni lazima kutambua majukumu ambayo mtu anakwenda kukabiliana nayo.
“Utandawazi mbovu nao umekuwa unachochea maadili mabovu kwa vijana na kudumbukia katika mimba za utotoni….tamaa za wazazi zinachangia watoto kuolewa katika umri mdogo hivyo elimu iendelee kutolewa kwa jamii ili kutokomeza ndoa na mimba za utotoni”.
“Kwa huyu binti ambaye ameolewa chini ya miaka 18 si dhani kama anaweza kumudu mambo ya ndoa maana akili yake bado haijakomaa ya kubeba majukumu mengi ya kuangalia na kuhudumia familia pia hata katika uchumi bado anakuwa hana uwezo wa kutafuta chochote hawezi kufikiria kupika nini au kufanya biashara zaidi ya kuwaza mambo ya utoto….kutokana na kukimbilia majukumu ambayo hajayafikia hivyo ndoa za utotoni zipigwe marufuku sana maana kuna athari nyingi za ndoa za utotoni” Alisema Mama Denis
Aidha Ispekta Dhikiri Pori ambaye ni mkuu wa Dawati la jinsia na watoto kutoka Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro anasema kuwa, kwa wale wanaojifariji kwamba sheria ya ndoa 1971 inaruhusu kuolewa wakiwa chini ya miaka 18, wanajidanganya kwani sheria itashika mkondo wake kwa kuwakamata wote watakao husika na kumuozesha mtoto huyo.
“Ndoa za utotoni zimekuwa ni changamoto kwa jamii za wafugaji, kutokana na kuenzi mila potofu hivyo tulijitahidi kuzuia ndoa zizifanyike tukishirikiana na maafisa ustawi wa jamii mfano maeneo ya Lugala, Malinyi, Kilosa, Mvuha na Magubike ni maeneo ambayo tunakutana na changamoto hizo za watoto wakitakiwa kuozeshwa, jambo ambalo ni ukatili”.
Pia Mratibu wa huduma ya Afya ya uzazi na mtoto Manispaa ya Morogoro Vijan Shabani Mkuse anasema kuwa elimu ya afya ya uzazi ikitolewa ipasavyo kwa vijana itasaidia kuepusha vifo vya uzazi huku akiisisitiza jamii kuachana na mila potofu za kuwaoza watoto kwani nayo ni sababu mojawapo inayochangia vifo vya mama na mtoto kutokana na kutokomaa kwa via vya uzazi na kupoteza damu nyingi wakati wa kujifungua.
Hata hivyo katika sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kifungu cha 13 hadi 17 kimebainisha kuwa mtoto wa kike anaweza kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 kwa ridhaa ya wazazi au amri ya mahakama na Sheria hiyo pia inatenganisha umri wa kuoa kwa mtoto wa kiume anayetakiwa kuoa akiwa na miaka 18 huku Sheria ya mtoto ya mwaka 2009 inatoa ufafanuzi kuwa mtotoni mtu aliye na umri chini ya miaka 18, kwa kufanya Marekebisho ya haraka ya Mabadiliko ya sheria hizi ambazo zinakinzana kuwa umri wa kuoa au kuolewa uanzie miaka 18 na siyo chini ya hapo itasaidia watoto kufikia ndoto zao na kuepusha vifo vingi vitokanavyo na uzazi wakati wa kujifungua sambamba na familia kuhudumiwa katika malezi bora.
No comments:
Post a Comment