NMB YAFADHILI ZIARA YA KIBIASHARA YA WAJASIRIAMALI 28 NCHINI CHINA. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, October 15, 2025

NMB YAFADHILI ZIARA YA KIBIASHARA YA WAJASIRIAMALI 28 NCHINI CHINA.

Benki ya NMB imefadhili ziara ya kibiashara ya wafanyabiashara 28, ambayo inalenga kuwapa uzoefu wa moja kwa moja wa masoko ya China na kuwaonesha fursa za biashara za kimataifa.

Ziara hii ni sehemu ya jitihada za benki hiyo kuimarisha ushindani wa wateja wake katika soko la kimataifa na kuwasaidia kupata maarifa muhimu kuhusu mnyororo wa usambazaji, mbinu za upatikanaji wa bidhaa, na kukuza ushirikiano na wawekezaji wa China.

Ili kuhakikisha ufanisi stahiki unapatikana, wajumbe wa msafara huo watatembelea maeneo mbalimbali vikiwemo viwanda, vituo vya biashara, pamoja na taasisi za Serikali na sekta binafsi, kwa lengo la kujifunza, kubadilishana uzoefu, na kuibua fursa za ushirikiano na maendeleo. 


Akizungumza katika hafla ya kuwaaga wafanyabiashara hao iliyofanyika Jumatatu jijini Dar es Salaam, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Bw. Filbert Mponzi, alieleza kuwa ziara hiyo ya siku tisa, inayotarajiwa kuanza leo, itajumuisha pia kushiriki katika Maonyesho ya 138 ya Biashara ya Kimataifa ya Canton, ambayo ni miongoni mwa maonesho makubwa na yenye mvuto mkubwa duniani.

“Ziara hii ni fursa adhimu kwa wafanyabiashara wetu kujipatia maarifa mapya, kufungua milango ya masoko ya kimataifa, na kujifunza mbinu bora na za kisasa za uendeshaji wa biashara. Ujuzi huu utasaidia si tu kukuza biashara zao binafsi, bali pia kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa taifa,” alibainisha Bw Mponzi.

Aidha, aliongeza kwa kusema: “Hii ni mara ya tano tangu mwaka 2019 kwa Benki ya NMB kuandaa na kufanikisha ziara ya kimataifa ya mafunzo kwa wateja wake. Msafara wa mwaka huu ni mkubwa zaidi kuwahi kufadhiliwa na benki yetu, jambo linalotufanya kuwa na matarajio makubwa katika kuleta matokeo chanya yatakayodhihirisha thamani ya uwekezaji huu.”

Bw Mponzi alifafanua kuwa kundi la mwaka huu lina wawakilishi 12 kutoka mnyororo wa thamani wa kilimo kutokana na umuhimu wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa, huku 16 wengine wakitoka sekta mbalimbali.

Baadhi ya wafanyabiashara walioteuliwa kushiriki katika ziara ya mwaka huu wameeleza kuwa safari hiyo si tu inawapa fursa ya kupata bidhaa zenye ubora wa kimataifa, bali pia maarifa muhimu ya kuongeza ubunifu, kuboresha mifumo ya uendeshaji wa biashara, na kuelewa kwa undani mahitaji na mwelekeo wa soko la dunia..

“NMB imetufungulia milango ya ndoto zetu. Kupata nafasi kama hii ya kukutana ana kwa ana na wazalishaji wakubwa wa China ni fursa adimu,” alisema Bw Sanjay Sumariya wa Singida Kilimo Ltd.

Bi Delfina Leon kutoka Barefoot International alisema kuwa anatarajia kujifunza zaidi kuhusu viwango vya ubora wa bidhaa, utaratibu wa kuagiza kwa wingi, na fursa za ushirikiano wa muda mrefu na kampuni za China.

Kwa upande wake, Bw Award Assah Mpandilah, aliyeshiriki kwenye ziara ya kwanza mwaka 2019, alieleza namna ilivyobadilisha mwelekeo wa biashara na maisha yake.

"Nilirejea nikiwa na mtazamo mpya kabisa wa kibiashara. Kupitia ziara hiyo, niliweza kuanzisha mahusiano ya moja kwa moja na wawekezaji, ambao hadi leo tunaendeleza ushirikiano wenye mafanikio makubwa yote haya yakiwa ni matokeo ya maono na uwekezaji wa NMB katika kuwawezesha wateja wake," alieleza.

Utaratibu huu wa NMB unaendana na ajenda ya Serikali ya kuimarisha sekta binafsi, kupanua wigo wa bidhaa na huduma za Tanzania katika masoko ya kimataifa, pamoja na kuvutia uwekezaji wa kigeni kupitia ushirikiano wa kimkakati na wenye tija.



“Kwa kutoa fursa kama hizi” alisema Bw David Mdeka wa Mafinga, “Benki ya NMB inaendelea kuonesha dhamira yake kwa kuwa taasisi ya fedha na mshirika wa kweli wa maendeleo ya wateja wake na taifa kwa ujumla.”

Mwisho

No comments:

Post a Comment