Na Okuly Julius-Dodoma
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetumia vyema Kongamano la Kwanza la Maendeleo ya Sekta ya Habari mwaka 2022 ,kwa kutoa tuzo za kutambua mchango kwa waandishi wa habari katika kuripoti habari za Sekta ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2022.
Kongamano hilo lililobebwa na kauli mbiu isemayo "Habari kwa Maendeleo Endelevu " liliwakutanisha zaidi ya Wadau 1000 kutoka Sekta ya habari Disemba 17,2022 katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, Jijini Dar-es-salaam na kufunguliwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe.Nape Nnauye.
Ambapo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa tuzo kwa waandishi waandishi watano(5) kutambua mchago wao katika kuandika na kuziripoti habari mbalimbali za Sekta ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka 2022.
Waandishi hao watano waliopata tuzo ni pamoja na Kuringe Mongi - Channel Ten,Jacob Mosenda- Citizen,Okully Julius- Okully Blog, Safina Yasir -TBC One na Mwamini Andrew -TBC Taifa Radio.
Akizungumza mara baada ya utoaji wa tuzo hizo Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknojia Sylvia Lupembe amesema kuwa tuzo hizi zitasaidia kuamsha hamasa kwa waandishi kuandika habari nyingi za sekta ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
"napenda kusema tunatambua na kushukuru waandishi wote ambao hakika wana saidia utoaji habari za Sekta, katika tukio hili la kwanza tumetambua wachache lakini wote kwetu wanastahili ." amesema Sylvia
Pia Sylvia ameongeza kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatambua vyema mchango wa waandishi na vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini hivyo wataendelea kuto ushirikiano mkubwa ili kuendelea kuijuza hadhira ya watanzania mambo mazuri yanayoendelea katika Sekta ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
"tutaendelea kushirikiana nanyi milango yetu iko wazi na tutaimarisha zaidi utoaji taarifa si tu za matukio lakini hata majibu na maelezo pale waandishi watakapohitaji. "amesema Sylvia
Akizungumza kwa niaba ya washindi hao Okuly Julius kutoka Okuly Blog ameishukuru Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kwa kumpatia tuzo hiyo huku akitafsiri kuwa ni heshima kubwa kwake na kuahidi kuendelea kuongeza kasi katika kuripoti na kutoa habari za Sekta ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia.
"Tuzo hii ni kama imeniamsha upya kwa sababu kila mwandishi angetamani kuipata ila Wizara hii kupitia Kitengo cha Mawasiliano Serikalini imeona ni vyema kuniamini na kunipatia hii ni alama sahihi ya kunifanya kuongeza bidii,kujituma na kuendeleza hapa nilipofikia,"amesema Okuly
Pia Okuly ameongeza kuwa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia inafanya kazi kubwa sana kuhakikisha Taifa linajikomboa kifikra na kuzalisha taifa lenye Ujuzi na maarifa ya kutosha katika kuleta Majawabu na masuluhisho ya changamoto mbalimbali zinazoikahili jamii.
No comments:
Post a Comment