CCM KATA YA KILIMANI WAJIPANGA KUIKIJANISHA DODOMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, January 20, 2023

CCM KATA YA KILIMANI WAJIPANGA KUIKIJANISHA DODOMA


Na Barnabas Kisengi Dodoma.

CHAMA cha Mapinduzi CCM kata ya kilimani Jijini Dodoma January 21 2023 kinatarajia kufanya uzinduzi wa upandaji Miti katika maeneo yaliyotengwa kwaajili ya kujenga Taasisi mbalimbali za Serikali katika Mtaa wa Chinyoyo katika Kata hiyo.

Akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya siasa ya kata ya kilimani Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM kata ya kilimani Ndugu Nathaniel Chibeye amesema lengo la upandaji wa miti katika maeneo hayo ya Taasisi ni kuunga mkono juhudi za Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.SAMIA SULUH HASSAN katika utunzaji wa Mazingira ili kuikijanisha Dodoma.


Ndugu Chebeya amesema wanatarajia kupanda Miti Elfu Moja katika maeneo mbalimbali ya kata hiyo ikiwemo eneo ambalo kutajengwa shule ya msingi, Sekondari, kituo cha afya,kituo kidogo cha polisi pamoja na Ofisi za Chama hicho tawi la chinyoyo na eneo itakapojengwa ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Chinyoyo.

" Tukiangalia Kata yetu ya kilimani ni kata kongwe na wanaishi viongozi wengi wa serikali na Chama na tulikuwa hatuna shule ya msingi wala Sekondari hivyo watoto Wetu waliokuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta elimu ila Sasa baada ya kupata maeneo haya tutaweza kujenga shule zetu za kata.",amesema Chibeye.

Sanjari na hilo ameongeza kuwa kupatikana kwa huduma ya afya, soko na Polisi mara vitakapojengwa itasaidia kuondokana na adha na vitakuwa mkombozi kwao.


"Tunapenda tutoe shukurani zetu za dhati kwa Serikali ya awamu ya sita kupitia Halmashauri ya jiji la Dodoma kwa kutufanyia Mpango kabambe wa urasimishaji wa Ardhi na kuweza kuwapatia maeneo hayo ya Ujenzi wa Taasisi mbalimbali za Serikali,"amesema

Pamoja na mambo mengine Mwenyekiti Chibeye amesema katika uzinduzi huo utakaoshirikisha Wananchi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi wa mitaa yote minne ya kata ya kilimani kwa kushirikiana na wenyeviti wa mitaa yote minne katika zoezi hilo Muhimu kwa maendeleo ya Kata ya kilimani.

Ameitaja Mitaa hiyo ni pamoja na Nyerere,Kilimani,Image pamoja na Chinyoyo ambapo pia watawagawia Wananchi wote wa Kata ya kilimani miti ya vivuli na matunda kwa kila kaya ili waweze kupanda katika maeneo yao wanayoishi.

Zoezi la uzinduzi wa upandaji Miti katika maeneo mbalimbali ya Kata ya kilimani utaongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri akiongozana na kamati ya ulinzi na Usalama ya wilaya ya Dodoma, kamati ya Siasa ya Kata ya kilimani na wanachama wa CCM na Wananchi wote wa Kata ya kilimani majira ya saa Moja asubuhi katika zoezi hilo ambalo Mtaa mwenyeji ni Mtaa wa chinyoyo.

No comments:

Post a Comment